MEJA JENERALI MABELE:VIJANA NDIO WALINZI WA NCHI HII

Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa Meja Jenerali Rajabu Mabele amewataka Vijana wa Jeshi la Kujenga Taifa kuilinda nchi yao na wawe tayari kufa kwaajili ya nchi yao pindi itakapo wahitaji kwani sasa wao ni Jeshi la akiba la Taifa.

Meja Jenerali Mabele ameyasema hayo alipokuwa akifunga mafunzo ya Vijana wa Mujibu wa Sheria Operesheni Miaka 60 ya Muungano katika Kikosi cha Msange JKT kilichopo Mkoani Tabora

“JKT tunafundisha Vijana wenye itikadi tofauti za kidini na kikabila lakini sisi tunafundisha Utanzania hivyo mafunzo ya JKT yanawafanya muwe wamoja na kuishi kama ndugu wa tumbo moja na kuwa waaminifu kwa nchi yanu ambayo ni Tanzania hivyo Nidhamu ya kuilinda nchi yetu ikawe ni silaha kubwa sehemu yeyote mtakapoenda. Alisisitiza Meja Jenerali Mabele

Naye Kaimu Kamanda Brigedi ya Faru Brigedia Jenerali Gabriel Kwiligwa amewaasa vijana hao kutumia vyema mafunzo waliyoyapata kwani kufanya hivyo wataliheshimisha Jeshi la Kujenga Taifa na Jamii nzima ya watanzania hivyo wakawe vijana bora wakati wote kwa kujiepusha na vitendo vitakavyo wasababishia matatizo katika afya ya mwili na akili.

“Niwasihi mkawe mfano wa kuigwa mtakaporudi nyumbani au kwenda Vyuoni kwa kujitofautisha na vijana ambao hawajapata mafunzo ya JKT”. Aliongeza Brigedia Jenerali Kwiligwa

Naye Mkurugenzi wa Oparesheni na Mafunzo Jeshi la Kujenga Taifa Kanali Amos Mollo amesema mafuzno hayo yalifunguliwa rasmi tarehe 19 June 2024 na kuanza kufungwa tarehe 04 Septemba 2024 katika vikosi mbalimbali, Aidha amewapongeza wazazi kuwaruhusu vijana wao kujiunga na Mafunzo ya JKT pia amewapongeza Vijana wahitimu kukubali kujiunga na Mafunzo hayo. Amewataka Vijana hao kutambua na kuthamini umuhimu wa mafunzo ya JKT, kwani Serikali imeendelea kuliongezea JKT uwezo ili Vijana wengi wapate nafasi ya kujiunga katika mafunzo hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) Kanali Makame Daima amemshukuru Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele kwa mwaliko na kusisitiza ushirikiano uliopo wa JKT na JKU ni wakudumishwa kwani Taasisi hizo ni ndugu wa damu na nimapacha kwani Zanzibar nao wanaendesha Mafunzo hayo kama ya JKT.

Amewaasa Vijana wawe na hali kubwa ya Nidhamu na Uzalendo huku akisisitiza Kwenda kuudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hivyo wote tunatakiwa kuulinda na kuudumisha Muungano wa nchi hizi mbili na kumalizia neno lake kwa kutoa kiasi cha Tshs Milioni tano kwa Kikosi kama mchango wa Jeshi la Kujenga Uchumi wa kuendeleza Miundombinu ya Kikosi cha Msange JKT.

Akitoa taarifa ya Mafunzo hayo, Kamanda Kikosi Msange JKT Kanali Sadick Mihayo amesema kwa kipindi chote ambacho Vijana wamekuwa wakihudhuria mafunzo Kikosini hapo ndani ya majuma kumi na mbili wamefundishwa mambo mbalimbali ambayo yamewajenga kuwa na moyo wa uzalendo wa nchi yao.

Akisoma risala kwa mgeni rasmi kwa niaba ya wahitimu wenzake Service Girl Loyce Lutamingwa amewaasa wazazi umuhimu wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa na kusema bado yana umuhimu mkubwa katika kuwaandaa vijana wa Kitanzania kuitumikia nchi yao.

“Tunaamini hivyo baada ya kujifunza mengi mazuri ambayo yametujenga sana, hivyo daima yadumishwe vizazi na vizazi vijavyo kwa maslahi ya nchi yetu. Hakika kupitia mafunzo haya, vijana wengi watajitambua na kuwa tayari kuijenga nchi yetu.” Alisisitiza Service Girl lutamingwa

Mwisho aliwasihi wazazi wenye mtizamo hasi kuhusu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa, wawaruhusu vijana wao wahudhurie mafunzo hayo.

Related Posts