Mvungi aongoza Joggin kuhitimisha mazoezi ya Shimiwi 2024

 

MKURUGENZI wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Abdallah Mvungi, leo tarehe 14 Septemba 2024, ameziongoza timu za Wizara hiyo katika jogging ya kilometa tisa iliyofanyika katika eneo la Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ikiwa ni hitimisho la maandalizi ya timu hizo kuelekea Mashindano ya SHIMIWI 2024. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Akizungumza mara baada ya jogging hiyo, Mvungi alisisitiza umuhimu wa mazoezi kwa watumishi, akisema yanasaidia katika kuboresha afya na akili, pamoja na kukuza ushirikiano ndani ya timu.

“Mazoezi ni njia bora ya kuhimiza uwiano kati ya kazi na maisha binafsi. Mazoezi haya yanawapa wafanyakazi fursa ya kufanya kitu kinachoweka miili yao na akili zao katika hali nzuri,” amesema Mvungi.

Aliongeza kwamba, “Mazoezi ya pamoja kama jogging yanaweza kusaidia kujenga mahusiano bora kati ya wafanyakazi, kuongeza ushirikiano, na pia, kuboresha mawasiliano kazini.”

Aidha, Mvungi aliwapongeza wanamichezo wa timu hiyo kwa jitihada zao za kuhudhuria mazoezi kwa ajili ya mashindano hayo, huku akisisitiza kuwa mazoezi hayo pamoja na jogging kama hiyo zitakuwa endelevu hata baada ya mashindano.

Kwa upande wake, Katibu wa timu hiyo, Patrick Kutondola, alisisitiza umuhimu wa kudumisha ari waliyonayo wachezaji, huku akitoa taarifa kwamba wanatarajia kuondoka kuelekea mashindano hayo tarehe 16 Septemba 2024. Aidha, Amewataka wachezaji hao kuendelea kujiandaa kwa kuweka miili yao na akili sawa kwa ajili ya mashindano.

Naye Mratibu wa timu hiyo, Getrude Kassara, amewataka watumishi hao kuendeleza nidhamu na kujiandaa kwa mashindano ili kuhakikisha wanapata ushindi na kuiletea wizara heshima.

Akizungumza kwa niaba ya Wachezaji, Kapteni wa Timu ya Kamba, Juma Ramadahani amesema wao kama wachezaji wako tayari kwa ajili ya mashindano hayo ambapo wameahidi ya kuwa watapambana kwa uwezo wao wote kuhakikisha wanailetea wizara makombe.

About The Author

Related Posts