Prof. Tibaijuka: Wizi wa kura upo

 

MWANADIPLOMASIA Prof. Anna Tibaijuka, ametaja kasoro za uchaguzi kuwa ni mbinu chafu za baadhi ya wasimamizi kuchelewa kufungua vituo vya kupigia kura kwa makusudi na wizi wa kura wa wazi wazi. Anaripoti Restuta James, Dar es Salaam … (endelea).

Prof. Tibaijuka ameyasema hayo leo 14 Septemba 2024 jijini Dar es Salaam alipokuwa anazungumza kwenye kongamano la maadhimisho ya siku ya Demokrasia Duniani, lililoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Amesema baada ya kupitishwa na chama kuwania nafasi katika ngazi yoyote, mgombea ni lazima aandae vijana wa kuhakikisha kura alizopata zinaonekana kwenye matokeo ya mwisho.

“Unaweza ukapigiwa kura na wanawake au wananchi, usipolinda hutazipata, kama huna watu wa kulinda kura yaani uwe na vijana wa bodaboda wanaokimbia huku na huku kuhakikisha huibiwi, huwezi kushinda,” amesema.

Amesema kitu kingine kinachoharibu uchaguzi ni baadhi ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura kuchelewa kuvifungua kwa makusudi hali inayowakatisha tamaa baadhi ya wapigakura hasa wanawake.

“Unakuta mama amekuja kituoni na mtoto mgongoni, muda unaenda msimamizi hafungui kituo na hajapika chakula, anaona ni bora arudi nyumbani kuwaandalia watoto chakula, kwa hiyo anashindwa kupiga kura,” amesema.

Amesema ni nadra kwa waangalizi wa uchaguzi hasa wa kimataifa kubaini mbinu hizo wakati wa mchakato wa uchaguzi.

Profesa Tibaijuka amesema baadhi ya waangalizi wanazunguka kwenye vituo vichache wananchi wanapoanza kupiga kura, wanarudi hotelini.

“Wanaangalia uchaguzi gani? Huo ndio ukweli, sisemi kwamba wasiwepo, lakini sisi tunajua hali halisi ya mambo yanayotokea usiku, watu wanaokimbia na maboksi ya kura (waangalizi), wanawaona saa ngapi?”

Wakati huo huo, amesema kuna haja ya kuwa na mgombea binafsi kwenye uchaguzi, ili kupata viongozi bora na kuondoa udikteta ndani ya vyama vya siasa.

Amesema baadhi ya wagombea wanaokubalika na wananchi wamekuwa wakienguliwa na vikao vya chama; na hivyo kufungiwa milango ya kuongoza jambo linalowanyima wananchi haki ya kupata kiongozi bora.

About The Author

Related Posts