KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua jijini Tripoli, Libya tayari kwa mechi ya mkondo wa kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku mastaa wote waliokuwa timu za taifa wakiwa wameshatua huko kumalizana na Al Ahli Tripoli.
Kitu cha kuvutia ni Simba imetua Libya bila kukutana na figisu zozote kwa mujibu wa Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, huku kikosi kikiwa kamili baada ya nyota waliokuwa timu za taifa kuwahi mapema kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa kesho Jumapili Uwanja wa wa Juni 11, jijini Tripoli.
Ahmed alisema kitu pekee cha tofauti ni hali ya joto kali waliyokutana nayo Tripoli, lakini aliwatoa hofu mashabiki, Simba imeshaenda kucheza mechi za CAF katika nchi zenye joto kali huko huko Afrika Kaskazini, lakini wakatoka salama na hata kesho mambo yatakuwa hivyo.
Simba inakutana kwa mara ya kwanza na Al Ahli, iliyoitoa Uhamiaji ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 5-1, ikiwa mziki wote chini ya Kocha Fadlu Davids aliyetamba yupo tayari kwa mchezo huo ili kupata matokeo mazuri yatakayowarahisisha kazi mchezo wa marudiano wiki ijayo jijini Dar es Salaam.
Kutua mapema kwa makipa Ally Salim na Moussa Camara sambamba na Edwin Balua, Steven Mukwala na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ waliokuwa na timu za taifa za Tanzania, Guinea na Uganda, imemuongezea nguvu zaidi kocha Fadlu aliyeajiriwa hivi karibuni kutoka Raja Casablanca ya Morocco.
Nyota hao walikutana na wenzao waliotokea Dar es Salaam na jana walianza mazoezi rasmi ya mchezo huo ambao Simba inasaka nafasi ya kutinga makundi ya michuano hiyo kwa mara nyingine baada ya mwaka 2021-2022 na kufika robo fainali baada ya awali kung’olewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Taarifa nzuri kwa Simba ni wenyeji watamkosa kipa namba moja mwenye uzoefu mkubwa wa michuano ya kimataifa, Mohammad Nashnoush aliye majeruhi na nafasi yake ikichukuliwa na Suleiman Al Tihar. Nashnoush mwenye umri wa miaka 36 atakosa mechi zote, huku yenyewe Simba haina majareuhi kwani Joshua Mutale na Jean Ahoua wote wamesharejea kuongeza nguvu kikosi cha Msimbazi.
Rekodi inaonyesha Simba imekuwa na kismati cha kupata ushindi mechi za hatua ya mtoano ugenini, licha katika hatua za makundi au robo fainali imekuwa ikichemsha.
Kupata matokeo mazuri ugenini kwa mechi za mtoano kama iliyopo sasa inachoweza kumpa jeuri kocha Fadlu aliyesema mapema mchezo wa kesho atashambulia mwanzo mwisho na kujilinda kwa akili ili kuumaliza mchezo ugenini kabla ya kurudiana wiki ijayo.
“Haitakuwa mechi rahisi, lakini tumejiandaa vya kutosha kuhakikisha tunapata ushindi ugenini, Al Ahli Tripoli sio timu ya kudharauliwa, ndiyo maana tunajipanga kuikabili kwa tahadhari kubwa lakini tupate matokeo ya kutubeba tukirudi nyumbani,” alisema Fadlu. Mabeki wa Simba watakuwa na kazi ya kumchunga zaidi Agostinho Crustovao Paciencia ‘Mabululu’ ambaye ni tishio zaidi katika eneo la ushambuliaji akiwa mmoja ya wachezaji wa timu ya taifa ya Angola, japo Mnyama wanajivunia kuwa na mastaa wakali wa eneo la ulinzi kuanzia kipa Camara, Aishi Manula na Salim mbali na mabeki Che Fondoh Malone, Chamou Karaboue na Abdulrazak Hamza.
Pia Simba ina wakali wengine wa eneo la kiungo akiwamo Debora Mavambo, Augustine Okejepha, Fabrice Ngoma, Mzamiru Yasin, huku eneo la mbele likihesheni majembe ya maana.
Katika mechi tano zilizopita za Simba katika michuano ya CAF ikiwa ugenini imepoteza mbili dhidi ya Wydad AC ya Morocco na Al Ahly ya Misri, huku nyingine tatu ikilazimisha sare tofauti, ikiwamo ile ya 1-1 na Ahly katika mechi za Ligi ya Afrika (African Footbal League), kisha 0-0 na Asec Mimosas ya Ivory Coast na Jwaneng Galaxy ya Botswana mechi zote za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita. Simba itarudiana na Al Ahli Tripoli yenye rekodi ya kucheza mechi karibu 24 nyumbani za ligi ya ndani na kimataifa bila kupoteza Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na mshindi wa jumla atatinga makundi kuanza kusaka ubingwa unaoshikiliwa kwa sasa na Zamalek ya Misri.