Na. Peter Haule na Chedaiwe Msuya, WF, Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Mashariki na Kusini, wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bi. Sara Mbago-Bhunu ambapo wamejadili kuhusu kuimarisha uhimilivu wa mifumo ya upatikanaji wa chakula nchini.
Akizungumza katika Mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma, Dkt. Mwamba alisema kuwa, mradi wa Kuimarisha Uhimilivu wa Mifumo ya upatikanaji wa Chakula unachangiwa na wadau mbalimbali ikiwemo IFAD, inayochangia dola za Marekani milioni 40.
Alisema mkutano kati yake na Bi. Bhunu, utaendelea kuimarisha ushirikiano na IFAD katika kujenga uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu kwa kuboresha hali ya maisha, utawala wa Sheria na kujenga uchumi imara.
“Tumejadili pia kuhusu mradi wa kuendeleza Kilimo na Uvuvi ambao unatekelezwa Tanzania Bara na Visiwani na unalenga katika kuimarisha Uchumi wa Bluu ambapo mradi huo unahusisha ununuzi wa Meli za uvuvi lakini pia kutoa mafunzo kwa wavuvi kuhusu ufugaji wa Samaki kupitia mabwawa na uzalishaji wa Samaki wachanga”, alisema Dkt. Mwamba
Vilevile alisema kuwa pande hizo mbili zinaendelea na mazungumzo kuhusu dhamana kwa wakulima watakao wezeshwa kimitaji kupitia wadau wa maendeleo kupitia programu mpya ya Partial-Credit Guarantees (PCG) inayolenga kutoa suluhisho la kifedha kwa wakulima wadogo kwa miradi ya maendeleo vijijini.
Aidha, Aliishukuru IFAD kwa kuendelea kuisaidia Serikali katika kutekeleza ajenda ya Taifa ya Maendelea kwa Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuongeza fursa za masoko ya mazao ya kilimo, uvuvi na ufugaji.
Aliiomba IFAD kuendelea kutoa msaada kwa Serikali katika juhudi zake za kuboresha sekta ya kilimo kuwa ya kisasa, kibiashara na yenye ushindani kwa maendeleo ya watu hususani wenye hali ya chini.
Dkt. Mwamba alisema kuwa, ugeni huo kutoka IFAD unaongeza matumaini kwa wakulima na wadau wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi nchini katika kuboresha maisha na kuongeza uzalishaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Mashariki na Kusini, wa Shirika la IFAD, Bi. Sara Mbago-Bhunu, alieleza mipango ya Shirika hilo ikiwa ni pamoja na kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika Sekta za kilimo, mifugo na uvuvi ili kuimarisha uzalishaji.
Aidha, alieleza kuhusu programu mpya ya Partial-Credit Guarantees (PCG) inayolenga kutoa suluhisho la kifedha kwa wakulima wadogo na kwa miradi ya maendeleo vijijini ambayo itaanza kutekelezwa baada ya kukamilika kwa nijadala mbalimbali.
Bi. Bhunu, alipongeza jitihada za Serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Shirika hilo hivyo kutoa hamasa ya kuendelea kutoa msaada kupitia wadau mbalimbali wa maendeleo.
Ujumbe wa IFAD uliambatana na Kaimu Mkurugenzi Mkazi Mpya wa IFAD, Bw. Mohamed El-ghazaly, ambaye alikuja kujitambulisha na Bi. Jacqueline Machangu-Motcho ambaye ni Afisa Programu Mashariki na Kusini mwa Afrika, ambapo kwa upande wa Wizara ya Fedha uliambatana na Mchumi Mkuu wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. John Kuchaka na Afisa Mwandamizi wa Idara hiyo, Bw. Isaya Ntalugela.
Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akieleza kuhusu manufaa ya kiuchumi katika undelezaji wa Sekta za uzalishaji ili kuwainua wananchi kiuchumi, wakati wa Mkutano kati yake na Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Mashariki na Kusini wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bi. Sara Mbago-Bhunu (hayupo pichani), jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Mashariki na Kusini wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Bi. Sara Mbago-Bhunu, akieleza kuhusu programu mpya ya Partial-Credit Guarantees (PCG) inayolenga kutoa suluhisho la kifedha kwa wakulima wadogo na kwa miradi ya maendeleo vijijini wakati wa Mkutano na Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, jijini Dodoma.