Stendi Simu2000 yafungwa rasmi kupisha ujenzi karakana ya mwendokasi

Dar es Salaam. Kituo cha Daladala Simu2000 kimefungwa leo Septemba 14, 2024 kupisha ujenzi wa karakana ya mabasi yaendayo haraka maarufu mwendokasi.

Karakana hiyo ni kwa ajili ya mradi wa mabasi hayo awamu ya nne.

Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kupitia Mkuu wa Idara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji, Mary Mwakyosi akizungumza na Mwananchi ameeleza hayo.

Julai 8, 2024 wafanyabiashara katika stendi hiyo waligoma wakipinga eneo hilo la soko kugeuzwa karakana.

Hata hivyo, Julai 13 Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alifanya mkutano na wafanyabiashara hao akawaeleza manufaa ya mradi huo, akiwaahidi watatengenezewa mazingira mazuri ya kuendelea na biashara zao wakati wa ujenzi wa mradi huo.

Awamu ya nne ya mradi huo inahusisha mabasi yatakayotoka Tegeta, Mwenge hadi Ubungo kupitia Barabara ya Sam Nujoma. Karakana hiyo inatarajiwa kukamilika ujenzi wake Machi, 2025.

Katika eneo hilo, Mwananchi imeshuhudia maandalizi ya kuifunga stendi hiyo yakiendelea.

Jirani na mageti ya kuingia na kutokea daladala kumewekwa utepe mwekundu.

Pia kumekuwa na mabadiliko ya uingiaji na utokaji wa magari kwenye stendi hiyo.

Shughuli za kuandaa kambi ya ujenzi na kuweka vifaa vya ujenzi vya mkandarsi anayejenga karakana hiyo zinaendelea, huku ulinzi ukiwa umeimarishwa na askari wa Jeshi la Polisi ambao baadhi walionekana wakiwa na silaha za moto.

Kwenye kuta za stendi kumebandikwa matangazo yenye saini ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ubungo yakitaarifu kuhusu kusitishwa kwa huduma katika stendi hiyo.

Akizungumzia hilo, Mary amesema tayari wafanyabiashara walishataarifiwa, hivyo wanalijua na kinachofanyika sasa ni kuendelea kurekebisha maeneo mbadala ya kufanya shughuli upande wa sokoni.

“Hapo stendi wafanyabiashara waliopo wenye vibanda hawazidi 15 hao tutawahamishia sokoni ambako kunatarajiwa kujengwa vibanda 800 vya wafayabiashara wakati wa utekelezaji wa mradi. Pia tuna maeneo ambayo yalikuwa hayana watu,” amesema.

“Wafanyabiashara wengine waliobaki ni wale wanaouza karanga, na wenye meza na miavuli ambao wote hawa watapewa maeneo,” amesema Mary.

Mawe yakiwa na utepe mwekundu yakiashiria kufungwa kwa stendi ya mabasi Simu2000

Kuhusu daladala, Meneja wa Mipango ya Usafirishaji wa Wakala wa Mabasi yaendayo haraka (Dart), Mohammed Kuganda amesema zitahamishiwa nje ya stendi  ambako upande mmoja wa barabara ya kuingilia stendi utatumika kama eneo la maegesho ya magari na wakati wa kutoka watazungukia kwenye mzungoko uliopo mwisho soko hilo.

Kwa upande wa wafanyabiashara amesema wameongezewa eneo kutoka mita za mraba 6,000 hadi kufika mita za mraba 11,900 hivyo wana imani kila mmoja atapata eneo la kufanyia biashara.

“Tunajua kipindi cha ujenzi kuna changamoto za hapa na pale zitajitokeza na sisi tupo tayari kuzibeba kwani hata hivyo vibanda 800 ni sisi tunavijenga,” amesema Kuganda.

Kwa upande wao, wafanyabiashara baadhi wanakiri kuwa na taarifa, huku wengine wakieleza hawakuna nazo.

Mwakilishi wa wafanyabiashara hao, Musa Mbwani amesema walishirikishwa kwenye vikao vyote, akisema wanaolalamika wana ajenda zao nyingine.

Mfanyabiashara Samwel Marite amesema tangazo wameliona jana Septemba 13 na leo wameambiwa waondoke huku hawajawa na maandalizi yoyote na hawajui wapi wataenda.

“Hapa mimi nina kibanda nimejenga kwa gharama ya Sh1.3 milioni, mali zilizopo ndani siyo chini ya Sh300,000 hivyo unaponiambia leo niondoke naenda wapi na eneo hujanitengea, wanataka familia zetu ziishije,” amehoji. Dereva wa daladala zinazofanya safari kati ya Temeke na Simu2000, Juma Mohammed amesema wao hawana eneo la maegesho ya magari na hwajui kwa nini imefanywa haraka pasipo maandalizi.

Jumanne Patrick, kiongozi wa madereva wa daladala, amekiri kuwepo tatizo hilo na kueleza stendi hiyo ilikuwa ifungwe jana Ijumaa saa sita usiku lakini kwa kuwa mpango wa kuegesha magari nje bado haujakaa vizuri waliomba kuendelea kuingia ndani kwa leo, huku wakisimamia kwa karibu uingiaji na utokaji wake.

Related Posts