Dar es Salaam. Baadhi ya wanazuoni na wadau wa haki jinai, wamesema hatua ya kuibuka shutuma za jumla zinazolihusiaha Jeshi la Polisi, inawatengenezea sumu wananchi hivyo kujenga dharau na ukinzani kwa chombo hicho cha ulinzi na usalama.
Matokeo ya hali hiyo kwa mujibu wa wadau hao, ni dharau na vitendo vya uvamizi wa vituo vya polisi kutokana na kutorishwa kwa masuala mbalimbali, na hivyo kusababisha vurugu na hata vifo.
Wameeleza makosa ya askari wachache wasio waadilifu ndani ya polisi yasitumike kulichafua jeshi hilo lenye jukumu la kulinda usalama wa raia na mali zao, huku nalo likitakiwa kijitazama na kujisafisha.
Hata hivyo, wengine wanalitazama suala hilo kuwa kwamba linasababishwa na wananchi kupoteza imani na vyombo vya ulinzi na usalama na siyo kuvidharau.
Wanasema kupotea kwa imani kunatokana na utendaji usioridhisha wa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya dola, ikiwemo matumizi ya nguvu yaliyoondoa maana ya huduma kwa wananchi badala yake imekuwa kuwaonea.
Akijadili suala hilo Septemba 13, 2024, Jaji mstaafu Thomas Mihayo, amesema kitendo cha raia kuvamia kituo cha polisi ni miongoni mwa hatua mbaya kuwahi kutokea, kwa sababu wangepaswa kuona kituoni hapo ni mahali pa usalama.
Amesema Polisi ndiyo mamlaka yenye jukumu la kulinda raia na mali zao, inapotokea watu wanawadharau ni mwelekeo mbaya.
“Sisi tukiwa vijana isingewezekana mtu akimbilie kituo cha polisi halafu atokee mtu akalazimishe kumtoa, ni jambo gumu na lisingewezekana, najiuliza kwa nini haya yanatokea sasa,” amesema.
Amesema tabia hiyo itasababisha Taifa lifikie hatua ya hatari zaidi, hasa ya wananchi kuona vituo vya polisi ni maeneo ya kawaida.
Kwa mujibu wa Jaji Mihayo, hayo yote yanachochewa na kauli za baadhi ya wanasiasa kushusha lawama na tuhuma kwa Jeshi la Polisi, zikiwemo za utekaji na mauaji ya watu.
“Naanza kuona kama vile baadhi ya wanasiasa wanawafanya wananchi wasiliamini jeshi kwa kulitupia lawama kila wakati,” amesema.
“Kwa sababu polisi ni chombo chenye mamlaka ya ulinzi wa amani, si vema kulilaumu na kulituhumu hadharani kwa matendo ya wabaya wachache.
“Jeshi ni chombo kizuri isipokuwa wapo wabaya ndani yake, sasa wabaya hao wasitumike kuwachafua wengine au kulichafua Jeshi la Polisi kwa ujumla wake,” amesema.
Amesisitiza umuhimu wa wanasiasa kuepuka kauli zinazolilaumu jeshi hilo, kwa kuwa kufanya hivyo kunapandikiza sumu kwa wananchi na hatimaye wanaanza kuwadharau polisi.
“Kama wananchi wanataka kujaribu kuona umuhimu wa polisi, waache kufanya kazi kwa saa mbili tu, nchi itawaka moto,” amesema.
Amesema anakumbuka kati ya miaka saba au minane iliyopita kutokana na Polisi kulalamikiwa na kutuhumiwa kwa rushwa barabarani waliamua kuacha kuongoza magari na matokeo yake yalikuwa mabaya.
Kauli kama hiyo imetolewa pia na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi alipozungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam Septemba 13, akisisitiza kuwa mambo mabaya yanayofanywa nchini na genge la watu wachache, yanalifarakanisha Jeshi la Polisi na wananchi.
Alisema hilo linafanywa ilhali katika baadhi ya maeneo wananchi wanajenga vituo vya polisi kwa nguvu zao na wanaomba wapelekewe askari.
“Tunazunguka mikoani, mnaona wananchi wanavyojenga vituo vya polisi wenyewe na wanaomba wapelekwe askari. Ina maana kwa wananchi wa kawaida polisi wanafanya kazi yao vizuri.
“Sasa haiwezekani kukitokea polisi wawili watatu wenye matatizo, ninyi mnataka wananchi wawakasirikie polisi nchi nzima, hili halikubaliki ni jambo la ovyo kuliko yote ninayoyafahamu,” alisema.
Dk Nchimbi alisema polisi ni miongoni mwa watumishi wanaotoa maisha yao kwa ajili ya wananchi kuliko inavyodhaniwa.
Alisema takwimu za miaka mitano kuanzia 2017 hadi 2023 zinaonyesha polisi 42 waliuawa katika mapambano na majambazi, huku 141 wakijeruhiwa.
“Tafakari kwa dakika moja tu, hivi polisi wote wakisema wamechukua likizo kwa saa 24 itakuwaje katika nchi hii,” alisema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe amesema utamaduni wa baadhi ya wananchi wa kujichukulia sheria mkononi na hasa kuvamia vituo vya polisi, si sahihi.
Amesema ni hatari zaidi kwa wananchi kukosa imani na Jeshi la Polisi, ambalo kimsingi lipo kuwalinda wao na mali zao.
“Turudi kwenye misingi ya utawala wa sheria ambapo ni Mahakama tu yenye mamlaka ya kusema nani mwenye kosa na nani hana.
“Tukianza kuchukua sheria mkononi tutabomoa Taifa letu wenyewe, kitu ambacho si sawa. Haya ndiyo madhara ya kulidharau Jeshi la Polisi,” amesema.
Amesema inawezekana wananchi wana hoja ya msingi juu ya hatua wanayochukua, lakini kuchukua sheria mkononi na kuvamia vituo vya polisi haiwezi kuwa njia bora ya kutatua tatizo.
“Polisi wana silaha na wanapozitumia kujihami dhidi ya raia waliowavamia madhara ni makubwa zaidi,” amesema.
Hata hivyo, amesema vitendo hivyo ni ishara kwamba kuna mahali Taifa limeteleza kwa kudharau utawala wa sheria na kutotimiza wajibu kama raia na upande wa polisi pia.
Amesema kuna matukio mengi ambayo Jeshi la Polisi linatuhumiwa kutotenda haki, jambo linalowafanya wananchi wawe na hasira hadi kujichukulia sheria mkononi.
“Yapo matukio mbalimbali yanayoashiria polisi kujihusisha na siasa, kitu ambacho ni kinyume cha sheria zetu. Haya yote yanawafanya wananchi wapate taswira tofauti ya Jeshi la Polisi,” amesema.
Ili kujiepusha na hilo, amependekeza kurudi kwenye misingi ya ujenzi wa Taifa na kuiishi, ikiwemo utawala wa sheria.
Amependekeza polisi wawajibike kwa mujibu wa sheria na kanuni zao zilizojengwa kuwahudumia wananchi kwa kuwalinda wao na mali zao.
Kwa upande wa wananchi, amesema wanapaswa kutii sheria bila shuruti, wawajibike kushirikiana na polisi katika kutimiza majukumu yao.
“Jeshi la Polisi liendelee kutoa elimu kwa wananchi juu ya haki na wajibu wao katika kulinda usalama wa nchi na watu wake. Bila polisi hakuna usalama,” amesema.
Kwa mtazamo mwinmgine, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Sabatho Nyamsenda, amesema kilichopo siyo wananchi kulidharau jeshi hilo, bali wamekosa imani nalo.
Kukosa Imani, anasema ndiko kunakowafanya waamue kujichukulia sheria mkononi.
Amesema ukosefu wa imani unatokana na jeshi hilo badala ya kutoa huduma, askari wake wanaonekana wakitumia nguvu zaidi kulinda usalama wa raia.
“Kwa ujumla mara nyingi linatumia nguvu na linaonekana lipo kwa ajili ya kuwanyanyasa na siyo kuwatumikia. Wananchi wanaona halitoi huduma bali linawanyanyasa,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Nyamsenda, mazingira hayo yameondoa uhusiano mzuri kati ya polisi na wananchi.
“Kilichotokea Geita ni kwamba wananchi waliona Jeshi la Polisi halitoi majibu sahihi juu ya kupotea kwa watoto na hata walipoandamana jeshi lilitumia nguvu kiasi cha kupoteza uhai wa raia.
Amesema kuna haja ya kuliangalia upya jeshi hilo, kama linaonekana kwenda kinyume cha misingi ya kuanzishwa kwake, lifumuliwe.
Amesema kwa sababu jeshi hilo limeundwa na Watanzania, halitakuwa jambo gumu kulibadili kuwa namna ambavyo jamii ingetamani liwe.