Unguja. Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale kupitia Kamisheni ya Utalii imeratibu maonyesho ya utalii wa Halal yanayotarajia kufanyika Oktoba 13, 2024.
Utalii huu ambao unahusisha zaidi masuala ya kuheshimu maadili na utamaduni licha ya kwamba unafanyika katika mataifa mengine, kwa Zanzibar ni mara ya kwanza ikiwa ni sehemu ya kupanua wigo wa utalii.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Septemba 13, 2024 Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga amesema tukio hilo la kihistoria litafanyika sambamba na kongamano la Light Upon Light la ujio wa Mufti Ismail Menk aliyejizolea umaarufu kutokana na mafundisho yake.
“Soko la utalii wa Halal linakua kwa kiasi kikubwa duniani, Zanzibar ikiwa ni visiwa vinavyotegemea kipato chake kikubwa kupitia sekta ya utalii, Serikali imeona kuna haja ya kukuza na kuutambua utalii wa aina hii kwa kuwa kuna fursa zinazopatikana katika utalii huu,” amesema Soraga.
Amesema soko hilo linatabiriwa kuwa na mapato ya kimataifa yanatarajiwa kuongezeka kutoka Dola za Marekani 245.78 bilioni mwaka 2022 hadi kufikia Dola 324.96 bilioni ifikapo mwaka 2030.
Amesema kutokana na ukuaji huo, wameona ipo haja Zanzibar kujitayarisha kunufaika na soko hilo.
Maonyesho hayo amesema yamelenga kuwakutanisha wanunuzi, wauzaji, watoa huduma na wadau muhimu wa utalii wa Halal.
Amesema wamealikwa washiriki zaidi ya 30 waliobobea katika utalii wa namna hiyo.
Maonyesho hayo amesema yanalenga kuitangaza Zanzibar kama kituo cha utalii huo, na kuvutia watalii kutoka masoko mbalimbali ya kimataifa.
“Hii itaongeza shughuli za kiuchumi na ajira kupitia upanuzi wa sekta ya utalii, kuchunguza masoko na fursa mpya zinazopatikana katika utalii wa Halal na kutoa fursa kwa wafanyabiashara kunganishwa na masoko kimataifa,” amesema.
Amesema wanatarajia wanajopo 16 wataalamu waliobobea katika fani ya utalii wa aina hiyo kutoka Afrika Kusini, Uturuki, Uingereza, Indonesia, Croatia na Malta watashiriki.
Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Hafsa Mbamba amesema ripoti zinaonyesha Bara la Asia ndilo linaongoza kwa asilimia 31 kwa watalii wa aina hiyo likifuatiwa na Afrika kwa asilimia 21.
“Kwa ujumla Afrika Mashariki bado hatujalikamata soko hili ikilinganishwa na Afrika ya Kaskazini kwa hiyo hapa ndiyo tunaona kuna fursa kujitangaza,” amesema.
Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar, Mahmoud Mussa Wadi amesema ofisi hiyo inajifunza kwa mataifa ambayo yamefanikiwa katika utalii huo.
“Tumetoa timu kamili kwenda nje kuona na tumeshiriki katika vikao mbalimbali vinavyohusisha utalii wa aina hii. Tumejiridhisha kuwa ni jambo lina uzuri wake na upungufu wake, ila tumejipanga kuelekea kwenye misingi sahihi ya utalii wa aina hii,” amesema.
Mkuu wa sekta ya utalii katika Taasisi ya Kufuatilia Utendaji Serikalini (PDB), Arif Abbas amesema utalii wa namna hiyo ni moja ya vipaumbele vya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, kwa hiyo amewapa maagizo kuhakikisha wanasimamia na kupanua wigo wa utalii hivyo wanaona kama azma yake inaenda kutimizwa.