Dar es Salaam. Ni mwaka mzima sasa familia iliyoshambuliwa huku mmoja wao akijeruhiwa kwa kupigwa risasi imekuwa ikisubiri bila taarifa yoyote, rufaa ya hukumu iliyoahidiwa kukatiwa na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kupinga adhabu waliyosomewa washtakiwa.
Katika hukumu hiyo washtakiwa hao ambao ni ndugu wawili, Nahir Mohamed Nasoro na Mundhir Mohamed Nasoro, waliomshambulia Gerdat Moshi Mfyoa akiwa na familia yake huku wakimjeruhi yeye Gerdat kwa risasi, waliachiwa kwa masharti.
Pia waliamriwa kulipa fidia ya jumla ya Sh2.6 milioni, adhabu ambayo Gerdat hakuridhika nayo.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 226 ya mwaka 2023, ndugu hao walishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, iliyoko Kinondoni, kwa mashtaka matatu waliyoyatenda Februari 18, 2023, eneo la Msasani, Mtaa wa Uganda wilayani Kinondoni mkoa wa Dar es Salaam.
Shtaka la kwanza lilikuwa ni kusababisha madhara makubwa, kinyume na kifungu cha 225, cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (PC), kama ilivyorejewa mwaka 2022, lililokuwa linamkabili mshtakiwa wa kwanza pekee yake, Nahir.
Alidaiwa kuwa siku hiyo ya tukio alimpiga risasa Gerdat kwa kutumia bastola aina ya Barreta yenye namba F49369W na TZCAR 79790 , kwenye bega la kushoto na kumsababishia maumivu makali.
Shtaka la pili lilikuwa la shambulio la kusababisha madhara mwilini kinyume cha kifungu cha 241, PC, lililokuwa likimkabili mshtakiwa wa pili, Mundhir.
Alidaiwa kuwa siku hiyo alimshambulia Saleh Mfyoa kwa kumpiga katika sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia maumivu.
Shtaka la tatu pia lilikuwa la shambulio la kusababisha madhara mwilini kinyume cha kifungu cha 241, PC, ambalo lilikuwa likiwakabili washtakiwa wote wawili wakidaiwa kumshambulia Neema kwa kumpiga katika sehemu mbalimbali za mwili wake na kumsababishia maumivu.
Kwa mujibu wa barua za malalamiko ya Gerdat kwa Idara ya Upelelezi ya Jeshi la Polisi Makao makuu na NPS, siku ya tukio washtakiwa waliigonga gari yake akiwa na familia lakini wakakimbia na yeye akawafuata mpaka walipoingia nyumbani kwao.
Wakiwa bado nje ya washtakiwa walitoka na kuanza kuwashambulia huku wakiwatolea matusi kwamba wanaweza kuwaua na hakuna wa kuwafanya lolote na ndipo mmoja akampiga yeye risasi ya begani.
Kesi hiyo ilipoitwa Oktoba 23, 2023, kwa ajili ya usikilizwaji wa awali, washtakiwa waliposomewa mashtaka tena na mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Saada Mohamed walikiri kutenda makosa hayo. Hivyo walisomewa maelezo ya awali ya kesi ambayo pia waliyakiri.
Hakimu Mkazi Mkuu, Franco Kiswaga, aliyeisikiliza kesi hiyo alisema kuwa maelezo hayo yamejenga makosa waliyoshtaiwa kwayo.
Hivyo aliwatia hatiani kwa mashtaka yote kama walivyoshtakiwa baada ya kujiridhisha kuwa kukiri kwao hakukuwa na utata.
Kabla ya mahakama kusomea adhabu, wakili Saada aliieleza mahakama kuwa upande wa mashtaka hauna kumbukumbu za makosa ya jinai ya nyuma kwa washtakiwa, kisha washtakiwa walipewa fursa ya kuomba shufaa ya adhabu.
Wakiomba shufaa dhidi ya adhabu, mshtakiwa wa kwanza, Nahir aliieleza mahakama kuwa ni mkosaji wa kwanza na ana mtoto mmoja mwenye umri wa miaka miwili na kwamba mke wake ni mama wa nyumbani na wote wanamtegemea yeye.
Hivyo alidai kuwa kama atatupwa gerezani watapata shida, na akaiomba huruma ya mahakama kwa maelezo kuwa amekiri kosa na hakutaka kuisumbua mahakama.
Mshtakiwa wa pili naye alidai kuwa ni mkosaji wa mara ya kwanza na ana familia ya mke na watoto watatu, na akaomba huruma ya mahakama akidai kuwa amejutia kile alichokitenda huku akiahidi kuwa hatarudia.
Katika shtaka la kwanza kwa mujibu wa kifungu walichoshtakiwa nacho, adhabu yake ni kifungo cha miaka saba jela na kosa la pili na la tatu (yanayofanana) kwa kifungu hicho adhabu yake ni kifungo cha miaka mitano jela.
Hata hivyo, katika kutoa adhabu, Hakimu Kiswaga alisema kuwa amekubaliana na maombi yao kuwa wanastahili huruma ya mahakama.
“Kutokana na maombi ya shufaa yaliyoibuliwa na washtakiwa ambayo ninakubaliana nayo, washtakiwa wanastahili huruma ya mahakama lakini bila kuathiri sheria zinazotumika”, alisema Hakimu Kiswaga .
Hivyo alitoa adhabu ya washtakiwa wote katika mashtaka yote matatu kuachiwa kwa masharti kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Pia alimuamuru mshtakiwa wa kwanza, Nahir kumlipa Gerdat (aliyempiga risasi), fidia Sh2 milioni; mshtakiwa wa pili, Mundhir kumlipa Joseph fidia Sh300,000 huku washtakiwa wote wakiamriwa kumlipa Neema fidia ya Sh300,000.
Akizungumzia hukumu hiyo, Gerdat ameulalamikia uamuzi huo akieleza kutoridhishwa na hukumu hiyo hususan kiwango cha adhabu walichopewa washtakiwa kulingana na madhara waliyoyapata, yaani kuachiwa huru kwa masharti na kiasi cha fidia iliyoamriwa walipwe.
Amelieleza Mwananchi kuwa tayari alishaiandikia barua Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) kulalamikia uamuzi huo kuwa hajaridhika nao na NPS ikamjibu kuwa itakata rufaa.
Katika barua hiyo ya Oktoba 30, 2024 Gerdat pia alimlalamikia mwendesha mashtaka, wakili wa Serikali Saada Mohamed kuwa hakulisimamia vyema shauri hilo.
NPS katika barua hiyo iliyosainiwa na Martenus Marandu, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), ya Novemba 6, 2023, ilieleza kuwa baada ya kupata malalamiko yake imeshawasilisha Mahakama Kuu, Dar es Salaam, taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
Barua hiyo inaeleza kuwa wameshaomba kumbukumbu za rufaa yaani mwenendo na hukumu na kwamba wanaendelea kulishughulikia suala hilo na watampa taarifa kama ipasavyo mapema sana.
Hata hivyo, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu mchakato wa rufaa hiyo ulikofikia, alisema kuwa hajui kwa kuwa mpaka sasa (mwaka mmoja kasoro siku 21) hajapewa mrejesho na ofisi NPS.
Mwendesha mashtaka wa kesi hiyo, Wakili Saada alipoulizwa kuhusiana na kesi hiyo na malalamiko ya waathirika, alisema kuwa haikumbuki kwa maana huwa anakuwa na kesi nyingi na kwamba kesi ikishamalizika hawezi kukumbuka.
“Kama hukumu ikitolewa huwa wanapewa hukumu (waathirika) na kama hawakuridhika wana malalamiko huwa wanakuja ofisini kuleta malalamiko yao na kama ni rufaa inakatwa na ofisi”, alisema wakili Saada na kuongeza:
“Sikumbuki ni nini nilichokisema exactly (kwa hakika), pengine kama ningekuwa na jalada hapa ningeweza kuona ni nini hasa nilikisema wakati huo.”
Hata hivyo mawakili wa kujitegemea, Jebra Kambole na Fulgence Massawe walipozungumza na Mwananchi kuhusu adhabu ya washtakiwa, wote walikuwa na maoni yanayofanana, kuwa iko sawa.
Kwa nyakati tofauti walisema kuwa kuna makosa ambayo mahakama zina mamlaka ya uhuru wa kutoa adhabu hata ya chini ya ile iliyobainishwa kwenye kifungu husika, kutegemeana na mazingira ya kesi pamoja na maombi ya shufaa ambayo mshtakiwa huyatoa.
“Lakini bado kuna nafasi ya kukata rufaa kama hawajaridhika na hiyo adhabu.”, alisema wakili Massawe.
Hata hivyo, Massawe na Kambole walisema kuwa kwa adhabu ya kuachiwa kwa masharti mahakama, inapaswa kubainisha masharti hayo ingawa imezoeleka kuwa ni kutotenda kosa ndani ya muda uliotajwa.
Kuhusu kiwango cha fidia washtakiwa walichoamriwa kuwalipa waahithirika, walisema kuwa kwa kuwa hiyo ni kesi ya jinai basi fidia hiyo pia haina tatizo.
“Kwa hiyo katika hili wanapaswa kufungua shauri la madai kuomba kulipwa fidia kwa madhara hayo waliyoyapata. Huko ndiko wanaweza hata kuangalia gharama walizozitumia katika matibau, muda wa kazi walioupoteza na mambo mengineyo”, alisema wakili Kambole.