Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Thomas Lutachunzibwa amewataka wataalamu wa Afya kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia kiapo cha Taaluma bila kuweka mbele maslahi kwani kiapo cha taaluma hiyo ni maagano na Mwenyezi Mungu.
Dkt. Lutachunzibwa ameyasema hayo leo wakati akifunga mafunzo ya siku mbili ya kudhibiti matukio ya Sumu kwa wataalamu wa Afya Mkoa wa Dodoma yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kufanyika jijini Dodoma.
“Kwenye Taaluma ya Afya tuna viapo ambavyo vinatanguliza mbele Utu na kuwasaidia watu na sio kutanguliza pesa mbele hivyo tuchape kazi, kila mtu anajukumu la kutumia elimu hii tuliyoipata kuisaidia Jamii yetu ya Watanzania kuzuia na kupambana na matukio ya Sumu” amesema Dkt. Lutachunzibwa.
Katika Hatua Nyingine Dkt. Lutachunzibwa ameishukuru Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupitia Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu kwa kuwezesha Mafunzo hayo kwani yanawajengea wataalam wa afya uwezo wa kupambana na matukio ya sumu yanapotokea.
Kwa upande wake Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Yohana Goshashy, amesema lengo la Mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo madaktari, wataalamu wa Maabara na wauguzi kuweza kukabiliana na matukio ya dharura ya sumu.
“Katika Mkoa wa Dodoma kumekuwa na ongezeko la Matukio ya Sumu, hapo awali Dodoma haikuwa katika mikoa 10 yenye matukio ya Sumu lakini kwa sasa Dodoma imeingia kwenye orodha hiyo. Jambo hili limetusukuma kutoa elimu hii ili kusaidia kuzuia na kudhibiti matukio hayo” alisema Goshashy.
Washiriki wa mafunzo hayo, Dkt. Sister Teodora Mwasu na Dkt. Misana Yango wameipongeza Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kuwapa elimu ambayo itakwenda kuwaongezea Ufanisi maradufu katika kupambana na kudhibiti matukio ya Sumu kwa Mkoa wa Dodoma.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Thomas Lutachunzibwa (aliyesimama kulia), akifunga mafunzo ya kudhibiti matukio ya sumu kwa wataalamu wa Afya yaliyofanyika katika ukumbi wa Profesa Manyele jijini Dodoma- Septemba 13,2024.
Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu, Yohana Goshashy (aliyesimama, picha ya kwanza),akiwasilisha mada kwa wataalamu wa Afya kuhusu majukumu yanayotolewa na Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu katika mafunzo ya kudhibiti matukio ya sumu kwa wataalamu hao yaliyofanyika katika ukumbi wa Profesa Manyele uliopo Makao makuu ya Mamlaka, jijini Dodoma, Septemba 13,2024.
Meneja wa Maabara ya Sayansi Jinai Toksikolojia, Kagera Ng’weshemi (aliyesimama kulia), akiwasilisha mada kuhusu majukumu yanayotekelezwa na Maabara ya Toksikolojia katika mafunzo ya kudhibiti matukio ya sumu kwa wataalamu wa Afya yaliyofanyika katika ukumbi wa Profesa Manyele jijini Dodoma, Septemba 13,2024.
Mtumishi wa Mamlaka, Christer Mwageni (aliyesimama), akieleza hali ya matukio ya sumu nchini na kwa Mkoa wa Dodoma kwa kipindi cha miaka mitano katika mafunzo ya kudhibiti matukio ya sumu kwa wataalamu wa Afya yaliyofanyika katika ukumbi wa Profesa Manyele uliopo jijini Dodoma, Septemba 13,2024.
Wataalamu wa Afya wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa na watumishi wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika mafunzo ya kudhibiti matukio ya sumu kwa wataalamu wa Afya yaliyofanyika katika ukumbi wa Profesa Manyele jijini Dodoma, Septemba 13,2024.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Thomas Lutachunzibwa (aliyekaa katikati), akiwa pamoja na Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Kudhibiti Matukio ya Sumu,Yohana Goshashy (aliyekaa kulia), na Mratibu wa huduma za Tiba wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Misana Yango (aliyekaa kushoto), pamoja na wataalamu wa Afya mara baada ya kuhitimisha mafunzo ya kudhibiti matukio ya sumu kwa wataalamu hao yaliyofanyika katika ukumbi wa Profesa Manyele jijini Dodoma, Septemba 13,2024.