Zitto atia neno uwekezaji Liganga na Mchuchuma

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikiendelea kusaka mwekezaji wa mradi wa Liganga na Mchuchuma, Kiongozi mstaafu wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe, ameshauri hatua ya uchakataji kuongeza thamani ya chuma ifanyike wilayani Ludewa ili kuharakisha shughuli za maendeleo.

Zitto ametoa ushauri huo, baada ya kuonyesha wasiwasi kutokana na mradi wa chuma wa Maganga -Matitu kudaiwa uchenjuaji wake utafanyika katika Mji wa Makambako badala ya Ludewa malighafi hiyo inapotoka.

Agosti 3, 2024  Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) lilitia saini makubalianao ya uchimbaji wa makaa ya mawe na chuma katika mradi wa Maganga Matitu na Kampuni ya Fujian Hexingwang Industry Tanzania Co. Ltd itakayowekeza katika mradi huo wenye thamani ya Dola milioni 77 za Marekani.

Akizungumza leo Jumamosi Septemba 14, 2024 na wananchi wa Ludewa, Zitto amedai ukipeleka mradi wa Maganga- Matitu kwenda Makambako maana yake hata ule wa Liganga na Mchuchuma utakwenda huko ili kuongeza thamani ya bidhaa hiyo.

“Hoja yetu kila kitu kifanyike Ludewa, hakuna kitakachoenda Makambako, Serikali iachane na mpango huo kama upo kwa sababu kiuchumi haiwezekani, lakini lini Serikali imebadili sera yake ya ujenzi wa reli kutoka Mtwara- Mbambabay hadi Ludewa kwenye chuma.

“Ukipeleka Makambako (Njombe) maana yake utalazimika kuitumia reli ya Tazara ili kutumia Bandari ya Dar es Salaam badala ya Mtwara,” amesema.

Zitto amesema mradi wa Liganga na Mchuchuma ni muhimu katika kulinda na kukuza ajira kwa Watanzania, akihoji kuhusu utelelezaji wake.

Amesema mwaka 2023 akiwa ziarani Makambako aliikumbusha Serikali kuhusu umuhimu wa mradi huo.

“Serikali imejenga reli lakini chuma imeagiza nje ya nchi, wakati bidhaa hiyo ipo imelala hapa Ludewa kwa tani bilioni 2.2, ukinunua chuma nje ya nchi maana yake unazalisha ajira za mataifa husika badala ya kuzalisha nchini mwako, sijui mnanielewa wananchi wa Ludewa?” amehoji.

Zitto ambaye ni mbunge wa zamani wa Kigoma Mjini amesema: “Nikiwa na mbunge wenu wa zamani, Deo Filikunjombe (marehemu) tulifanya kazi ya kuusukuma  mradi huu upate mwekezaji, nasikia watu wamelipwa fidia jambo lililotakiwa lifanyike miaka 10 iliyopita.”

Mei mwaka 2024 Serikali iliidhinisha Sh15.4 bilioni kwa ajili ya malipo ya fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa Liganga na Mchuchuma ambao kwa sasa unatafuta mwekezaji kwa ajili ya uchakati wa malighafi hiyo.

Katika hatua nyingine, Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu amewaambia wananchi wa Kwamshemsi wilayani Korogwe mkoani Tanga kuwa chama hicho, kinaendelea kusimama na wananchi katika kuhakikisha kinatatua kero zao ili kupata maendeleo.

Pia ameitaka Serikali kuweka mifumo bora ya ardhi itakayowanufaisha wazawa siyo wawekezaji pekee wanaochukua maeneo makubwa, huku Watanzania wakibaki wakihangaika kumiliki ardhi hiyo.

“Kasi ya Serikali kutatua migogoro ya ardhi bado hairidhishi, changamoto hii ipo kila sehemu ikiwemo kwenye mashamba makubwa Watanzania wananyanyasika tofauti na wawekezaji. Ni wakati mwafaka kwa mamlaka husika kuweka mikakati bora ili kuondokana na suala hili,” amesema.

Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake wa ACT- Wazalendo, Janeth Rithe amesema chama hicho, kipo katika ziara kutembelea majimbo akisema viongozi wake wakuu wamejigawa kikanda ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.

“Tunataka kutengeneza jukwaa moja litakalosikiliza kero, na jukwaa hilo si jingine bali ni ACT-Wazalendo ambalo litakahakikisha ushindi utakaoleta mabadiliko ndani ya Taifa, CCM ipo madarakani kwa muda mrefu lakini bado kuna changamoto za maji, mbolea na barabara,” amesema.

Rithe amewataka wananchi kufanya mabadiliko katika uchaguzi wa serikali za mitaa,  kwa kuchagua mbadala wa CCM ambao ni chama cha  ACT- Wazalendo kitakachowaletea maendeleo.

“Tunatakiwa tufanye mabadiliko katika sanduku la kura kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji kwa kuiondoa CCM madarakani,” amesema Rithe aliyewahi kuwa diwani wa Kunduchi mwaka 2010/15.

Viongozi wakuu wa ACT- Wazalendo wakiwemo wastaafu na wajumbe wa kamati kuu wapo katika ziara ya mikoa 26 kwa ajili ya kuimarisha chama hicho, sambamba na kunadi sera zao ili wananchi wakichague katika chaguzi zijazo.

Related Posts