Bashe atoa maagizo watumishi sekta ya kilimo

Kahama. Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Bashe ameitaka Tume ya Umwagiliaji kuhakikisha inakamilisha utekelezaji wa mradi wa Bwawa la Umwagiliaji katika Kijiji cha Malenge mkoani Shinyanga.

Mbali na hilo, Bashe amesema Rais Samia Suluhu Hassan hana deni kwa Watanzania katika sekta ya kilimo hivyo watendaji wa wizara wana wajibu wa kuhakikisha maelekezo ya  Serikali yanatekelezeka.

Amesema kwa sasa wasaidizi wa Rais akiwemo yeye wana wajibu wa kutekeleza maelekezo kwa vitendo kwenye sekta hiyo.

“Rais Samia hana deni wizara ya kilimo, anaipenda sekta hii, anatudai matokeo, amefanya mengi, lengo likiwa ni kutaka matokeo sekta ya kilimo, haijawahi kutokea bajeti kutoka Sh294 bilioni hadi Sh1.24 trilioni, sisi wasaidizi wake na watendaji tunaowajibu wa kufanya kazi usiku na mchana,” amesema Waziri Bashe.

Bashe ameyasema hayo leo Jumapili, Septemba 15, 2024 alipokuwa ziarani katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga na kutembelea bwawa hilo.

Bwawa hilo lenye ukubwa wa mita za ujazo 600,000, linajengwa kwa thamani ya Sh2.5 bilioni, huku Kampuni ya Uchimbaji Dhahabu ya Barrick ikiwa moja ya wawezeshaji.

Amesema uwepo wa mradi huo utawezesha kilimo kuwa cha uhakika, lakini wakulima watavuna hadi mara tatu kwa mwaka.

Ameitaka tume hiyo ya umwagiliaji, itoe ushauri wa zana zinazohitajika katika uzalishaji ndani ya skimu hiyo.

Katika ziara yake hiyo, amesema sambamba na bwawa katika eneo hilo pia kutajengwa kituo cha zana za kilimo na maghala ya kuhifadhi mpunga.

“Ninamuomba Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga (Anamringi Macha), ufanye kikao cha ujirani mwema na mwenzio wa Tabora ili bonde la Manonga lilindwe kwa ajili ya miundombinu ya uzalishaji wa chakula badala ya kujenga nyumba za wakazi,” amesema Bashe.

Hata hivyo, amesema dhamira ya Serikali ya kukuza sekta ya kilimo ni ya kudumu na itaendelea kuwepo ikilenga kuinua hali ya wakulima.

Katika kulifanikisha hilo, amewataka wataalamu wa sekta ya kilimo wakiwemo maofisa kilimo na ugani kuishi vijijini kuhakikisha wanasaidia jamii zilizopo huko.

Katika hatua nyingine, Bashe ametembelea shamba la Serikali la kijiji la Kisuke na kutaka lipimwe na ipatikane hati itakayosomeka ‘Eneo la kilimo Isuke na Wizara ya Kilimo.

Amesema eneo hilo, litanufaika na mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), kwa wakazi wa kijiji hicho, huku Bodi ya Pamba ikitakiwa kulifanya kuwa mradi wa kuzalisha zao hilo.

Meneja wa Mradi wa Tume ya Umwagiliaji Mkoa wa Shinyanga, Ebenezer Kombe amesema Bwawa la Shija litakuwa na mifereji mikuu na midogo ya kuingiza maji mashambani yenye urefu wa kilomita 13 na eneo litakalotengwa kwa ajili ya kunyweshea mifugo.

Related Posts