Dar es Salaam. Mara nyingi tukisikia kuhusu watoto wanaovunja sheria, wengi huhusisha na watoto wa mitaani au wale wasio na makazi maalumu. Lakini taarifa zinasema hata watoto walio kwenye familia huangukia kwenye changamoto hii.
Hiyo ni matokeo ya malezi duni yanayochochewa na kukosekana kwa uangalizi wa karibu wa familia, kunakotajwa kuwa sababu ya watoto kuingia katika makundi mabaya na mwisho kujikuta mikononi mwa sheria.
Ripoti ya Hali ya Uhalifu iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi inaonesha kesi 648 zilifunguliwa mwaka 2023 katika mahakama mbalimbali za watoto nchini, ikiwa ni ongezeko la kesi 393 kutoka kesi 255 zilizokuwepo hadi Disemba 2022.
Ripoti hiyo inaonesha mwaka 2023, jumla ya kesi 903 zinazohusisha watoto zilishughulikiwa na kati ya hizo, kesi 695 zilimalizika, huku nyingine 208 zikiwa bado zinaendelea.
Mkoa wa Mwanza unaonekana kuwa kinara katika mahakama za mikoa ya kipolisi, ukiwa na kesi 66, ukifuatiwa na Tanga wenye kesi 58, Pwani 51, Kilimanjaro 45 na Temeke 39.
Wakati hali ikiwa hivyo kitaifa, kwa upande wa Dar es Salaam, watoto wanaopokelewa katika mahabusu ya mkoa idadi yake imekuwa ikipanda na kushuka mwaka hadi mwaka.
Mfano mwaka 2019/2020 walikuwa 123, mwaka 2020/2021 walikuwa 103, 2021/2022 walikuwa 138 huku mwaka 2022/2023 wakiwa 144.
Kwa mujibu wa mmoja wa maofisa katika mahabusu ya watoto jijini Dar es Salaam ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, wavulana ndio wanaoongoza kwa kutiwa nguvuni kutokana na makosa mbalimbali ikilinganishwa na wasichana.
Makosa ambayo yamewatia nguvuni ni unyang’anyi wa kutumia silaha, mauaji, wizi, kuingia nchini bila kibali, bangi, ubakaji na ulawiti, wizi wa mifugo, kutotii amri ya mahakama.
“Makosa mengine ni kujeruhi, kuvunja na kuiba, kukutwa na nyara za Serikali, uzembe na uzururaji, lugha ya matusi, kuingiza mifugo shambani na kupanga wizi,” anasema ofisa huyo.
Hata hivyo, anaweka wazi kuwa tofauti na ilivyo kwa watu wazima, hakuna mtoto anayefungwa gerezani, bali huchukuliwa hatua mbalimbali, ikiwemo kuunganishwa na familia zao, kupewa dhamana, kulipishwa faini, kupelekwa shule ya maadili na kuwekwa chini ya uangalizi.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya makosa kama wizi yanatajwa kuchangiwa na umasikini, kwa sababu baadhi ya watu hulazimika kutumia njia zisizo halali ili kujipatia kipato.
Tofauti na matarajio ya wengi, watoto wanaofikishwa kwenye mahabusu hiyo ni wale waishio nyumbani ikiinganishwa na wale wa mitaani.
Sasa tukirudi katika maadili, adha hii si ya wazazi pekee, bali hata baadhi ya viongozi wa dini nao wananyooshewa kidole, huenda wamesahau kuhubiri juu ya tabia njema na kuwafundisha watoto kuacha dhambi na badala yake wamejikita katika kuaminisha watu katika miujiza ya watu kupata fedha.
Mwanasaikolojia John Ambrose anasema miongoni mwa sababu ya kuwapo kwa matukio haya ni mwingiliano wa tamaduni na desturi za watu tofauti zilizoshindwa kudhibitiwa.
Hali hiyo inafanya vijana kujiingiza katika vihatarishi vingi vinavyochochewa na matumizi ya teknolojia na kuweka watu katika hatari zaidi ya kufanya matendo yanayokinzana na sheria.
“Kuna kuathirika kwa mila kunakotokana na mabadiliko ya kiteknolojia yaliyoathiri jamii kwa kiasi kikubwa na jamii zilizopo zinashindwa kuboresha yale yaliyoharibiwa na teknolojia,” anasema Ambrose.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi kupitia ripoti hiyo, limeweka bayana mikakati yake, ikiwemo kuhamasisha jamii, hususan vijana kushiriki katika shughuli halali, hasa za ujasiriamali ili waweze kujipatia kipato.
“Pia kuzishawishi taasisi za fedha ziweze kupunguza urasimu wa upatikanaji wa mikopo nafuu na kupunguza riba kubwa zinazotozwa katika mikopo hiyo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo, ilipokuwa ikizungumzia matukio ya makosa ya kuwania mali.
Hilo linaenda sambamba na kuhamasisha kuwepo kwa mipango endelevu ya utoaji elimu kwa umma, hususan ya ujasiriamali.
Pamoja na umasikini kutajwa kuwa sababu ya kuwapo kwa baadhi ya matukio kama wizi na unyang’anyi, Profesa Abel Kinyondo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema jambo hilo halina uhusiano wa moja kwa moja, kwa kuwa kuna wakati mtoto anaweza kutoka kwenye familia bora lakini akafanya vitendo hivyo.
“Ni kweli kuwa watoto kutoka familia maskini wanafanya matendo ya kiovu, lakini haimaanishi kuwa maskini ndiyo unatakiwa kufanya vitendo hivyo.
“Wanaofanya makosa si maskini tu, bali wapo pia watoto wa matajiri, kuwa na kipato au kutokuwa nacho si sababu ya kufanya shughuli za kihalifu, badala yake maadili ndiyo sababu,” anasema Profesa Kinyondo na kuongeza:
“Analelewa vipi pale nyumbani, wengine wanalelewa na mzazi mmoja, hii inafanya watoto wanakuwa katika mazingira ambayo si mazuri, kukosekana kwa mzazi akiwa ndani au hayupo inategemeana na yeye anashughulikia vipi watoto wake,” anasema Profesa Kinyondo.
Anasema zamani nyumba za ibada zilikuwa zinasisitiza maadili na kufundisha watu kufuata hilo, lakini baadhi ya nyumba za ibada zinazungumzia hela kwa kuwaambia watu watakuwa matajiri kwa kupaka mafuta, maji.
“Zamani watu walikuwa wakiambiwa acha dhambi, kuwa mtakatifu, badilika, watu walikuwa wanaambiwa fanya hiki, sasa nyumbani kuna shida na kwenye nyumbani za ibada nako kuna shida zaidi, hili limekuwa tatizo,” anasema Profesa Kinyondo.
Anasema hiyo ndiyo sababu ya kuwapo kwa matukio hayo na ikiwa malezi anayopata mtoto hayampeleki kwenye uadilifu, ni rahisi kufanya makosa makubwa.
“Siyo umasikini unamfanya awe hivyo, umasikini unamharakisha kufanya hivyo kwa sababu hajapata yale malezi yaliyokuwa mema,” anasema Profesa Kinyondo.
Suala la malezi linasisitizwa pia na Ofisa Elimu Taaluma wa shule za Awali na Msingi katika Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, Asia Amas, anayewataka wazazi kutimiza jukumu lao la malezi kwa kuhakikisha wanazungumza na watoto wao.
Anasema uwepo wa mazungumzo ya mzazi na mtoto yanasaidia kuwaandaa kwa changamoto zinazowakabili, badala ya kuacha jukumu hilo kwa walimu pekee.
“Niwaombe wazazi, hawa watoto baada ya muda mfupi tutatengana nao lakini mnapokuwa mnawaandaa kwa ajili ya kwenda ngazi ya sekondari, zungumza na mtoto wako, kuwa karibu naye, mnasihi sana kwa sababu atakaa mbali na wewe hutaelewa anachokifanya kwa zaidi ya miezi sita au mitatu akiwa nje ya familia aliyolelewa, muda huo ni mkubwa sana kwa mtoto kubadilika kitabia.
“Kwa hiyo ni wajibu wetu sisi wazazi kuzungumza nao sasa, wakafanye wanachokiendea huko na si kwenda kuiga yaliyo kinyume, dunia ya sasa imebadilika, tunasikia matukio ya ajabu
yanayotokea hasa kwa watoto,” anasema Asia.
Agosti 31, 2024 wakati wa mahafali ya darasa la saba Shule ya Msingi Tabata, Mkuu wa Kituo cha Polisi Tabata, David Mwakinyuke alitoa wito kwa wazazi kuwa makini na matendo wanayoyafanya mbele ya watoto wao, hususan kwa kipindi hiki ambacho wamehitimu elimu yao ya msingi wanasubiri matokeo.
Anasema watoto mara nyingi hujifunza kutokana na kile anachokiona kwa watu alionao karibu, wakiwamo wazazi au walezi.
“Wazazi kwanza wanatakiwa kuhakikisha wao wenyewe wanakuwa kiigizo chema kwa watoto wao kwa kufanya yale yanayokubalika mbele yao na jamii, kwa sababu maadili ya mtoto kwa kiasi kikubwa yanategemea malezi anayoyapata ndani ya familia,” anasema.
Ili kuondokana na hali hiyo, Ambrose anashauri kufanyika kwa mapitio ya mila na desturi na kuziwekea mpango kazi na mkakati ili kwenda sambamba na mabadiliko yanayotokea.
“Kuongeza elimu kwa wazazi na walezi ili wajue wajibu na majukumu yao katika makuzi, malezi kwa jamii husika na kutoa elimu kwa jamii ambayo wanapaswa watoto kulelewa,” anasema Ambrose.
Mtafiti wa elimu, Muhanyi Nkoronko anasema elimu ni moja ya njia zinazoweza kutumika kuwaepusha watoto kuingia katika vitendo viovu.
Anasema moja ya kazi kubwa ya elimu ni kuchangia kuwakuza watoto kiakili, kimwili, kijamii na kihisia kwa kuwa na mwenendo mwema kwa maisha yake ya kila siku.
Kupita dhana hiyo, elimu rasmi inawapa watoto mifano chanya ya kuigwa, fursa za mwingiliano wa kijamii inayowaonyesha haiba njema na maadili.
“Hii inaweza kusaidia kuunda tabia zao na kupunguza uwezekano wa kujihusisha na tabia mbaya,” anasema Nkoronko.
Anasema ubora wa elimu anayopokea mtoto unasaidia kumuundia mazingira chanya na wezeshi kwa ajili ya kujifunza, yatakayomsaidia kukuza tabia chanya na kuepuka kufanya mambo maovu.
Maneno ya Nkoronko yanaungwa mkono na Kassana Salehe, mwalimu mstaafu anayesema ufuatiliaji mzuri wa watoto, hasa wanapokuwa shuleni husaidia kukabiliana na vitendo hivyo viovu.
“Kumpeleka shule na kuhakikisha amefika ni suala la kwanza, je, wazazi ni kwa kiasi gani wanafuatilia mienendo yao, wengine hata vikao vya shule hawahudhurii, inakuwa ngumu,” anasema Kassana.