Leo ni siku ya kumuenzi mkeo, utafanya nini kumfurahisha?

Usisubiri hadi kumbukumbu yake ya kuzaliwa au kumbukizi ya siku ya ndoa ‘anniversary’ kumwonyesha mkeo thamani yake maisha mwako, unajua ipo siku rasmi ya kuadhimisha kumuenzi mke. Kwa lugha ya kimombo inaitwa ‘Wife Appreciation Day’.

Siku hiyo inayoadhimishwa Septemba 15 (leo Jumapili), kila mwaka imeteuliwa kuwa maalumu kwa ajili ya kuhakikisha unamshukuru, kumsifu na kumpongeza kwa kazi kubwa anayoifanya kama mke.

Andiko hili halihalalishi kumpitisha mkeo katika mitihani kwa siku zote usubiri Septemba 15 ndiyo umwonyeshe thamani yake hapana, muktadha ni kuitumia siku hii maalumu kama nyenzo ya kustawisha upendo, furaha na hali ya kuaminiana na mkeo.

Katika maisha ya ndoa ni muhimu kuonyesha thamani kwa mke wako. Hii si tu inadhihirisha kwamba unamwona na kumthamini, bali pia inaimarisha mahusiano yenu na kukuza upendo wa kweli. Haijalishi umekuwa na ndoa kwa mwaka mmoja, miaka 10 au hata 50, lazima uonyeshe mke wako jinsi alivyo na thamani kwako.

Umuhimu wa kulifanya hilo, unathibitishwa na takwimu za Taasisi ya Maendeleo ya Familia ya Afrika Mashariki za mwaka 2021, zinaoonyesha asilimia 65 ya familia zilizo na msingi wa uaminifu na kuthaminiana huwa na utulivu wa ndoa kwa kipindi kirefu zaidi kuliko zile zisizo na utaratibu huo.

Kama hiyo haitoshi, utafiti wa Chuo Kikuu cha Stanford mwaka 2018, ulibaini wanandoa walioonyesha kuthaminiana waliripoti kiwango cha juu cha furaha na kuridhika kwenye ndoa zao. Asilimia 80 ya wanandoa walioshiriki kwenye utafiti huo walisema kuthaminiana ni kiungo muhimu cha kudumisha uhusiano wa furaha.

Benki ya Dunia nayo mwaka 2020, iliweka wazi kuwa, familia zenye wanandoa wanaoheshimiana na kuthaminiana zina uwezo mkubwa wa kushirikiana kwenye maamuzi ya kifedha, jambo linalowasaidia kujenga uchumi imara.

Kwa baadhi ya wanaume, kuonyesha hisia za upendo inaweza kuwa jambo la kawaida. Lakini kwa wengine, inaweza kuwa changamoto. Si kwa sababu ya dosari ya tabia au makosa yako, bali kwa sababu baadhi ya wanaume hawapendi kuonyesha hisia zao au wanapata shida kuziwasilisha.

Tunajua hali hiyo, lakini siku ya kumuenzi mke wako inatoa nafasi bora ya kuhakikisha mke wako anajua jinsi anavyothaminiwa.

Unaweza kujifunza kuadhimisha siku hii

Kwanza kabisa mwanaume wa kweli na anayejali ndoa yake huhitaji kujua miaka ya ndoa. Badala yake anapaswa kufungua milango kwa mke wake, kumpongeza kwa busu la ghafla, kumletea maua au kutumia muda mzuri pamoja ili kumfanya ajue jinsi anavyothaminika kwake.

Siku hii inahusu kuonyesha upendo wako kwa mke wako na kuthibitisha thamani yake kwako. Mara nyingi hatutoi shukurani ya kutosha kwa wale tunaoishi nao kwa karibu, hususan wake.

Wakati umekaa na mtu kwa muda mrefu, inaweza kuwa rahisi kupuuza mambo yote wanayofanya kwa ajili yako. Iwe ni kupika chakula cha jioni au kukufanya uache tabasamu kila siku, ni muhimu kutafakari jinsi mke wako anavyochangia maisha yako na kumfanya ajue kuhusu hili.

Kununua pete kwa mke wako ni mila ya zamani sio kwa ndoa tu au uchumba, bali pia kwa maadhimisho ya miaka yenu ya ndoa. Unaweza kutumia siku hii kuhuisha ndoa yenu kwa kumnunulia pete nyingine.

Kitendo cha kutoa pete kama ishara ya upendo kilifanywa na mshairi wa Kirumi wa vichekesho aitwaye Plautus. Miaka michache baadaye, katika karne ya nne, kitendo hiki kilibadilishwa kuwa cha Kikristo.

Siku ya kumuenzi mke wako ni tukio la kupendeza linalowapa waume nafasi ya kuonyesha jinsi wanavyopenda na kuthamini wake zao. Tangu ilipoanzishwa, imeorodheshwa katika kalenda ya matukio ya kila mwaka ya Chase na imekuwa maarufu sana.

Kuna mambo mengi ambayo mke mwenye mapenzi na msaada hufanya kwa mume wake, na hii ni fursa kwa waume kutazama nyuma na kukumbuka mambo makubwa na madogo ambayo huongeza thamani kwenye maisha yao.

Jinsi ya kuadhimisha siku ya kumuenzi mkeo wako

Mbali ya kumununulia zawadi ya pete mwanaume anaweza kumuagizia mkeo shada la maua analolipenda, kumfanyia sapraizi ya kuandaa mahali mtakapopata chakula cha jioni pamoja au kumpeleka kwenye mapumziko mafupi ya kimapenzi. Pia unaweza kumnunulia manukato au kitu cha kipekee ambacho kitabaki kama kumbukumbu kwa siku nyingi zijazo.

Hii haimlazimishi anayeifanya kutumia fedha nyingi, anaweza kuiandaa kulingana na mazingira na kipato chake ilimradi muhusika ambaye ni mke afurahi na kuona namna anavyothaminiwa na mumewe.

Related Posts