Mabalozi wa mataifa zaidi ya matano  kushiriki kongamano Zanzibar

Unguja. Wakati likitarajiwa kufanyika tamasha la wajasiriamali Zanzibar, mabalozi kutoka mataifa makuu zaidi ya matano duniani wanatarajia kushiriki katika kongamano maalumu litakalojadili namna bidhaa kutoka visiwa hivyo  zinavyoweza kupata masoko kutoka nchi hizo.

Tamasha hilo lenye kauli mbiu ‘Fahari ya Zanzibar, kuimarisha uwezeshaji kidijitali’, linaangazia umuhimu wa matumizi ya kidijitali katika biashara ambalo litakuwa na vipengele kadhaa likiwemo kongamano la kimataifa litakaloshirikisha mabalozi kutoka Marekani, China, Oman, Singapore na nchi za UAE. 

Akizungumza kuhusu tamasha hilo, leo Jumapili, Septemba 15, 2024 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Sharif amesema tamasha hilo la wiki moja kuanzia Septemba 20 hadi 27, limeandaliwa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (Zeea) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TanTrade).

“Kongamano hili ambalo litafanyika siku ya ufunguzi wa tamasha, litajadili jinsi gani bidhaa kutoka Zanzibar zinaweza kufaidika kwa kupata masoko kutoka nchi hizo,” amesema.

Tamasha hilo litafanyika katika viwanja vya maonyesho ya biashara Dimani Zanzibar, mgeni rasmi katika ufunguzi utakaofanyika Septemba 20, 2024 anatarajiwa kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

Kwa mujibu wa Shariff sekta mbili muhimu za utalii na biashara zinatarajia kunufaika moja kwa moja kwani wadau watajadili namna bora ya kuboresha masoko ya bidhaa na huduma kutoka Zanzibar kupitia sekta hizo.

Jambo lingine litakalofanyika katika tamasha hilo ni maonyesho kwa mikoa ambapo kila mkoa wa Zanzibar utaonyesha fursa za masoko na uwekezaji zilizopo katika maeneo yao.

“Maonyesho haya yatatoa nafasi kwa bidhaa kutoka Zanzibar kuonekana na kutangazwa kupitia jukwaa hili maalumu, zikilenga soko la kitaifa na kimataifa.”

Pia  kutakuwapo na mafunzo maalumu kutoka taasisi mbalimbali zitakazomuwezesha mjasiriamali na mwananchi kupata elimu kuhusu fedha, masoko, mifuko ya hifadhi ya jamii, ubora wa viwango na urasimishaji wa biashara.

Faida nyingine itakayopatikana na kuzindua nembo ya bidhaa zinazotoka Zanzibar ili kuzitambua.

Kuzitangaza bidhaa na huduma zinazopatikana Zanzibar ili kuvutia masoko mapya na kukuza uchumi, kuunganisha wajasiriamali wa Zanzibar na Tanzania Bara ili kushirikiana kukabiliana na changamoto na kupata suluhisho za changamoto yatakuwa miongoni mwa mambo yatakayopata fursa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Airpay ambayo ni mdhamini mkuu wa tamasha hilo, Yasmin Chali amesema wataimarisha uwezeshaji wa kidijitali katika utoaji wa huduma.

“Tunatambua na kuthamini jitihada za kuwawezesha wajasiriamali na kukuza biashara zao ushirikiano wetu ni kuhakikisha mifumo ya kifedha inakidhi mahitaji,” amesema. 

Naye Mkurugenzi wa Zeea, Juma Burhan amesema wameshafikia zaidi ya watu 180 waliojitokeza hivyo watauza na kupata fursa ya kujitangaza kimataifa.

Related Posts