Madhara wanayopata wanaokaa karibu na wavuta shisha, sigara

Dar es Salaam. Kama wewe ni miongoni mwa wanaokaa karibu na wavutao shisha au sigara hasa maeneo ya starehe, anza kujitenga na maeneo hayo ili uepuke hatari zifuatazo.

Kukiwa na ongezeko la magonjwa ya mfumo wa upumuaji nchini, wataalamu wa afya wamesema kemikali inayotoka kwa mtu anayevuta shisha au sigara huwa sumu mbaya zaidi ikipokewa na mtu mwingine.

Tafiti za kisayansi zinaonyesha moshi wa sigara una kemikali zaidi ya 400 zenye athari kubwa kwa afya ya binadamu, hususan kwa anayevuta hewa yenye moshi huo uliovutwa na mtu mwingine, licha ya mtumiaji pia kuathirika.

Akizungumzia athari kiafya Mtaalamu wa tiba za michezo na mkufunzi kutoka Chuo cha American Sports Medicine ACSM, Waziri Ndonde ameiambia Mwananchi pafu moja la shisha lina athari kubwa katika afya ya binadamu.

“Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani na watafiti wengine, pafu moja ya shisha ni sawasawa na sigara sita na kukaa kama saa moja wakati unavuta shisha ni sawa na kuvuta sigara 150 mpaka 200,” amesema Ndonde.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha kwa mwaka 2023, maambukizi ya mfumo wa hewa yaliwaathiri watu milioni 4,901,844 sawa na asilimia 18.9 yakiongoza kwa magonjwa 10 yaliyosumbua Watanzania huku matatizo ya njia ya mkojo (UTI) yakiathiri watu milioni 4,095,104 sawa na asilimia 15.8.

Madaktari wameshauri kuepuka kujichanganya na watu wanaovuta shisha au sigara hususan kwenye kumbi za starehe, kwani asilimia kubwa ya wanaovuta hewa iliyotoka kwa mvutaji huathirika zaidi.

Mtaalamu wa magonjwa ya saratani kutoka Hospitali ya Ocean Road, Dk Maghuha Stephano amesema:“Ile kemikali iliyopo kwenye nikotin inayopatikana kwenye shisha na sigara mtu anapovuta, ule moshi unaotoka nje ndiyo una sumu nyingi zaidi kuliko ule unaoingia kwa mvutaji.”

Dk Maghuha amesema madhara yanayoweza kumpata mtu anayepokea moshi kutoka kwa mvutaji ni pamoja na kupata matatizo ya kawaida kwenye njia za hewa kama kupaliwa na hata magonjwa ya mfumo huo.

“Baada ya muda mrefu ndiyo anaweza kupata madhara kama ya magonjwa ya saratani za mapafu, kichwa na koo, lakini pia zile za ini na aina nyingine ikiwamo saratani ya shingo ya kizazi,” amesema.

Daktari wa wodi ya uzazi na mtoto Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya, Dk Jail Kalinga amesema mama mjamzito anapotumia sigara au kuvuta moshi wake huwa hatarini yeye na mtoto.

Ametaja madhara yanayoweza kutokea kuwa ni pamoja na mimba kuharibika, kondo kuhama mahala pake, kifafa cha mimba, saratani ya kizazi, watoto kufia tumboni, moyo kutokuwa na uwezo wa kupumua vizuri.

Ameitaja changamoto nyingine ni watoto wanaozaliwa salama pindi wanapofika umri wa miaka mitatu au minne kuugua ugonjwa wa mfumo wa hewa, matatizo ya moyo na mtindio wa ubongo unaosababisha kutokuwa na uwezo mzuri wa uelewa hasa katika masomo darasani.

Dk Kalinga amesema pia kuna kundi la mabinti nalo liko hatarini kwa ugumba kutokana na matumizi ya pombe na kuvuta sigara au shisha kupita kiasi.

Daktari Bingwa wa magonjwa ya saratani Ocean Road, Crispin Kahesa amesema kwa kawaida mtu huvuta hewa safi na ikifika ndani huchujwa na taka sumu hutoka, hivyo mvutaji anapouvuta moshi wa tumbaku ule utokao hutoka na sumu nyingi zaidi.

“Tumbaku ndiyo chanzo cha aina zote za saratani, japokuwa kuna zile ambazo athari ni kubwa zaidi kama saratani za mfumo wa hewa ikiwemo mapafu, njia ya chakula, lakini hata ikifika sehemu nyingine inaleta madhara,” amesema.

Dk Kahesa amesema waathirika wakubwa wa matumizi ya tumbaku ni wanawake na watoto kwa kuwa ikiwa baba anatumia tumbaku, atavuta mbele yao na hawawezi kuwa na namna au mamlaka ya kujitetea.

“Ukiwa mwanamume hakuna mtu atakukemea na vivyo hivyo tukija kwenye madhara, tunaona wanaopokea moshi wa sigara ndiyo wanaoathirika zaidi na hapo ndipo tunapowaweka watoto na wanawake kwenye hatari ya kupata magonjwa ya saratani,” amesema.

Amesema waathirika wakubwa ni watoto wachanga na wale ambao bado wangali tumboni.

Ripoti ya kidunia ya WHO imeyataja magonjwa ya saratani ya mapafu, kiharusi na moyo kuongoza katika vifo huku sababu kubwa ikitajwa ni uchafuzi wa hali ya hewa unaosababishwa mabadiliko ya tabia nchi.

“Uchafuzi wa hewa huathiri viungo vyetu muhimu na kusababisha vifo vitokanavyo na saratani ya mapafu kwa asilimia 36, kiharusi asilimia 34 na kusababisha magonjwa ya moyo kwa asilimia 27,” inaeleza ripoti hiyo.

Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba husababisha zaidi ya vifo milioni 3 kila mwaka, pamoja na kusababisha maambukizi ya njia ya chini ya hewa kwa asilimia 21, ugonjwa sugu wa mapafu 19 asilimia na ugonjwa wa mapafu kwa asilimia 6.

Mkuu wa kitengo cha utafiti na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Palangyo amesema ongezeko kubwa la magonjwa ya moyo linaloonekana katika nchi zinazoendelea sababu kubwa ni moshi wa tumbaku.

“Tunapovuta hewa isiyo safi tafsiri yake ina kemikali kadhaa na hizo zinajumuisha kaboni dayoksidi salfa dayoksidi na intojeni dayoksidi ambazo zinaweza kuharibu moja kwa moja mfumo wa damu, moyo na mishipa ya moyo.

“Kwanza inakwenda kufanya mishipa ya moyo inakazika, inapoteza uwezo wake wa kusinyaa na kutanuka ili iweze kusukuma damu. Kemikali zikiharibu mishipa inaifanya kuanza kuziba kwa kujaa taka na mafuta na matokeo yake kupunguza upenyo wa damu kupita. Na hivyo tunaanza kupata vifo vya ghafla na kuziba kwa mishipa ya damu,” amesema.

Related Posts