Magome, mapipa yalivyounda Magomeni Mapipa

Kwa wale wataalamu wa kukisia, ni rahisi ni rahisi kwao kuunganisha maneno  haya mawili: magome na magomeni.

Hoja ikiwa pengine kwa kuwapo magome, eneo likaitwa magomeni kwa maana mahala kwenye magome.

Ni sawa na kuunganisha mkwaju na kupata mkwajuni, yaani mahala ulipo mti wa ukwaju. Au mbuyu ukapata mbuyuni. Vivyo hivyo kwa minazi ukapata minazini, mzambarau na mzambarauni. Mifano ni mingi.

Kwa mtindo huohuo wa ufundi wa lugha wa wakazi wa eneo hilo,  ndivyo neno Magomeni, ambayo ni moja ya kata maarufu jijini Dar es Salaam ilivyopatikana.

Huu ni mwonekano wa uliokuwa Mtaa wa Jaribu eneo la Magomeni Mapipa miaka ya 1950. Hapa ni katika ofisi ya TANU. Picha na mtandao

Historia inaonyesha kuwa mahala ambapo leo kunajulikana kwa jina la Magomeni, kulikuwa na miti inayotoa magome kwa wingi.

Hali hiyo ikasababisha wenyeji kupaita eneo hilo Magomeni, wakimaanisha eneo lenye magome ya miti.

Hata hivyo,  umaarufu wa kata ya Magomeni ambayo historia pia inaonyesha iliwahi kuitwa Mzimuni miaka mingi iliyopita, haunogi kama hutotaja eneo maarufu la Mapipa lililozaa neno Magomeni Mapipa.

Kifupi hujaijua au hujafika Magomeni kama hukufika Mapipa. Linaweza kuwa ndilo eneo maarufu zaidi  katika kata nzima ya Magomeni inayopakana pia na kata maarufu ya Kariakaoo kwa upande mmoja. Lakini unajua asili ya eneo hilo kuitwa Mapipa?

Mwonekano wa makutano ya barabara za Morogoro na Kawawa, eneo linalotajwa kuwa zamani kulizungushwa mapipa. Picha na Michuzi blog

Mwenyeji wa eneo hilo na msomi wa historia, Sheikh Khamis Mataka amezungumza na Mwananchi na kueleza asili ya eneo hilo kuitwa Magomeni Mapipa.

Anasema: ‘’ Jina la Mapipa lilitokana na ujenzi wa barabara ya Morogoro. Kampuni iliyokuwa ikijenga ilipomaliza ujenzi, eneo hilo ambalo sasa ni Mapipa katika makutano ya barabara za Morogoro na Kawawa walichimbia mapipa kama sita ya lami wakayaacha, ndiyo ikawa alama,’’ anasema huku akimtaja Mzee maarufu kwa jina la Shomvi aliyekuwa eneo hilo akiuza mihogo.

Jengo la soko la Magomeni kama alama muhimu ya eneo la Magomeni Mapipa kwa sasa. Picha na Michael Matemanga

Anaongeza: “Ilipokuja kampuni ya Japan ya Kajima kutengeneza barabara kwa  kipande cha Jangwani, iliyaondoa yale  mapipa.’’

Mapipa ya leo inayonakishiwa na uwepo wa barabara ya mabasi ya mwendo kasi, awali lilipambwa na uwepo wa kituo cha afya, msikiti wa Kichangani na Kanisa la KKKT na migahawa maarufu ya Shibam na Butiama. Vyote hivi vikiwa jirani na makutano ya barabara za Morogoro na Kawawa.

Sio Mapipa pekee, Magomeni ina maeneo mengine kama Makuti, Kagera, Mikumi,  Usalama na mengineyo.  Majina yote haya yana asili ama kutoka kwa wenyeji au mamlaka za kiserikali.

Mtaa mmojawapo katika eneo la Magomeni Mapipa. Picha na mtandao

Kwa wenyeji wa Magomeni Mapipa, eneo hilo lina umaarufu mkubwa katika Wilaya ya Kinondoni.

Ni eneo linalokumbukwa kwa kuwa na vijiwe maarufu kama vile kijiwe cha washairi kilichokuwa mtaa wa Magomeni nyumbani kwa mshairi Juma Mnyibwe (mtu – kitu).

Pia eneo hilo kuna nyumba ya mshairi maarufu Mohamed Selemani (Mtu Chake) na hoteli ya Butiama iliyowavutia watu kutoka maeneo mbalimbali. Kama wewe mpenzi wa pilau, Butiama ni mahala sahihi kwako.

Simulizi za Magomeni Mapipa haziwezi kunoga kama  hutotaja kijiwe cha Shibamu sambamba na mgahawa wake , uliowavutia wenyeji wengi wa Jiji la Dar es Salaam, akiwamo Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete.

Jina Magomeni hutolikuta Dar es Salaam. Pekee kuna Magomeni katika wilaya za  Bagamoyo, Kilosa na pia mjini Unguja.

Related Posts