Novatus Miroshi achekelea namba Uturuki

BAADA ya kumaliza majukumu ya timu ya taifa, Taifa Stars, mchezaji kiraka wa Goztepe ya Uturuki Mtanzania Novatus Miroshi amerejea kujiandaa na Ligi nchini humo akichekelea kupata namba kwenye kikosi cha kwanza.

Miroshi alitambulishwa na klabu hiyo Julai 23 mwaka huu akitokea Shakhtar Donetsk ya Ukraine ambako alifanikiwa kucheza michuano ya UEFA Champions League.

Akizungumza na Nje ya Bongo, Miroshi alisema anapambana kuhakikisha anapata muda mrefu wa kucheza katika kikosi cha kwanza.

“Nashukuru nimefika salama Uturuki, ukisajiliwa katika klabu mpya inakuwa ngumu kupata nafasi, itategemea na uliowakuta wana uwezo gani, lakini ukipambana unaaminiwa na kocha,” alisema Miroshi na kuongeza:

“Goztepe tumecheza mechi nne za ligi hadi sasa japo nimekuta tayari wamecheza mechi moja hivyo mechi tatu zilizosalia nimecheza ingawa moja niliingia nikitokea benchini.”

Miroshi tangu atue kikosini hapo amecheza mechi tatu, mbili kwa dakika 90 kila moja dhidi ya Antalyaspor 0-0 Agosti 10, Fenerbahce 2-2 Agosti 17 na Alanyaspor 2-2 ambayo alianzia benchini akicheza kwa dakika 58.

Related Posts