Padri Kitima alivyowapandisha madhabahuni Dk Nchimbi, Lissu na Mnyika

Dar es Salaam. Kilele cha Kongamano la tano la Ekaristi Takatifu la Kanisa Katoliki kimefana. Maaskofu 28, mapadri na watawa wa kike na kiume wameshiriki.

Kilele cha Kongamano hilo limefanyikia Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam leo Jumapili, Septemba 15, 2024 likiwa na kauli mbiu ‘Udugu huponya ulimwengu, sisi sote ni ndugu.’

Pia, viongozi mbalimbali wa kisiasa wameshiriki ambao ni Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi, Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, Waziri wa Ujenzi, Innoncent Bashungwa, MKuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na Spika mstaafu, Anne Makinda.

Moja ya tukio lililovuta hisia za watu na kuibua shangwe kutoka kwa waumini walioujaza uwanja huo ni la Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima kuwatambulisha kwa pamoja Dk Nchimbi, Lissu na Mnyika.

Padri Kitima amewaita jukwaani wote kwa pamoja na kuwasimamisha mbele ya madhabahu kisha akaanza kumtambulisha mmojammoja ambo wote kwa pamoja wamesoma seminari kwenye safari zao za kielimu. (Zaidi tazama video ya tukio hili).

Baada ya kumaliza utambulisho huo, RC Chalamila alipopata wasaa wa kuzungumza amesema mkoa huo uko salama huku akipongeza kwa kuwaona Dk Nchimbi na Mnyika wakiwa pamoja.

“Hata yale waliyoandaliwa yataishia hapahapa madhabahuni,” amesema Chalamila huku vicheko vikirindika.

Licha ya Chalamila kutokufafanua yale yaliyoandaliwa lakini Chadema imepanga kufanya maandamano ya kupinga matukio ya utekaji na mauaji Septemba 23, 2024 jijini Dar es Salaam. Polisi imeyapiga marufuku maandamano hayo.

Kwa upande wake, Rais wa TEC, Askofu Wolfgang Pisa naye amegusia uwepo wa wanasiasa hao akisema: “Leo ni mara yangu ya kwanza naona CCM na Chadema wamekaa sehemu moja. Kweli Ekaristi takatifu ni ndugu mmoja.”

Related Posts