RC Tabora ataka uchunguzi wa kina kifo tata cha daktari

Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humo kufanya uchunguzi wa kina baada ya kuokotwa mwili wa daktari wa Kituo cha Afya cha Ulyankulu akiwa amefariki eneo la Kombo Masai, Malolo, Manispaa ya Tabora.

Chacha amebainisha hayo leo Septemba 15, 2024 wakati akizungumza na Mwananchi kuhusu kifo cha daktari huyo huku akisisitiza kwamba ofisi yake itatoa taarifa rasmi Septemba 17, 2024 baada ya uchunguzi kukamilika.

“Nimeagiza uchunguzi wa kina ufanyike ili tujue sababu za kifo chahuyo daktari, maana yako mengi yanasemwa lakini sisi tunataka majibu ya uchunguzi ndiyo yalete majibu sahihi, hivyo Jumanne tutatoa taarifa rasmi kama mkoa,” amesema Chacha.

Wakati hayo yakiendelea, mwili wa Dk Dismas Chami (32) unatarajiwa kuzikwa Wilaya ya  Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya taratibu za kiuchunguzi kukamilika na mwili wake kukabidhiwa kwa ndugu leo Septemba 15, 2024.

Mwili wa Dk Chami ulipatikana Septemba 13, 2024 baada ya kutowekwa kwa zaidi ya siku 11 ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, mwili wake ulikutwa eneo la Kombo Masai, kata ya Malolo mkoani Tabora.

Mwananchi limefika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora (Kitete) ulipohifadhiwa mwili huo kwa ajili ya kuzungumza na ndugu wa marehemu waliokuwepo, lakini hawakuwa tayari kuzungumza kwa madai  kuwa wao ni marafiki wa marehemu na sio ndugu.

Mwili wa Dk Chami utasafirishwa leo kutoka hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete kuelekea Ulyankulu kwa ajili ya kuagwa na ndugu, jamaa na marafiki na kisha kesho Septemba 16, 2024, utasafirishwa kuelekea Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya maziko.

Siku moja baada ya kupatikana kwa mwili huo, Jeshi la Polisi nchini limesema limeanza kuchunguza tukio hilo kwa kushirikiana na wataalamu wengine.

Taarifa iliyotolewa na Polisi leo Septemba 15, 2024 kupitia kwenye mtandao wa Instagram inasema: “Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau wengine linachunguza kifo cha Dk Chami ambaye amekutwa amefariki dunia huko Tabora eneo la Kombo Masai, kata ya Malolo mkoani Tabora.

Taarifa hiyo inaeleza kwamba daktari huyo alimuaga mkuu wake wa kazi na mke wake Septemba 2, 2024 kuwa anaelekea Tabora kushughulikia akaunti yake ya benki iliyokuwa na changamoto na angerejea Septemba 3, 2024.

Siku iliyofuata, Septemba 4, taarifa hiyo inaeleza kuwa hakupatikana kupitia mawasiliano yake ya simu. Septemba 10, 2024, daktari mkuu wa kituo hicho akiambatana na mke wake walifika Kituo cha Polisi na kutoa taarifa ya kutoonekana kwake tangu Septemba 2, 2024.

Polisi wanaeleza kwamba tarehe hiyohiyo, Dk Chami alimtumia ujumbe mke wake kwa njia ya WhatsApp unaosema: “Nisamehe sana, baada ya dakika chache sitakuwa nanyi duniani, simamia kila kitu nilichoanzisha. Pesa zote ziko akaunti ya CRDB. Simamia na watoto wasome. Kwa heri.”

Baada ya ujumbe huo, Polisi wanaeleza kwamba hakupatikana tena hadi mwili wake ulipopatikana jana Septemba 14, 2024 saa 3 usiku akiwa amefariki dunia na uchunguzi wa awali umebaini kuwa alishajaribu kujiua mara mbili.

Related Posts