Samia ampongeza Profesa Karim Manji tuzo ya Harvard

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amempongeza Profesa Karim Manji wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) aliyechaguliwa kuwa miongoni mwa washindi wa tuzo ya muhitimu bora wa Chuo Kikuu cha Harvard.

Profesa Karim Manji ameokoa maisha ya watoto wengi wachanga pamoja na waliozaliwa kabla ya wakati na wenye uzito mdogo yaani ‘njiti’ katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) miaka 30 iliyopita.

Rais Samia ametoa pongezi hizo leo Jumapili, Septemba 15, 2024 kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

“Pongezi za dhati kwa Profesa Karim Manji, bingwa, mkufunzi na mtafiti katika eneo la tiba ya watoto na afya ya vijana, kwa ushindi wa tuzo ya Alumni Award of Merit kutoka Shule ya Afya ya Chuo Kikuu cha Harvard (Harvard T.H. Chan School of Public Health).”

“Kwa zaidi ya miaka 30, Profesa Manji amekuwa daktari, mkufunzi na mtumishi wa kupigiwa mfano katika Hospitali ya Taifa na Chuo Kikuu cha Afya na Tiba Shirikishi, Muhimbili. Tunajivunia kujitoa kwako kwa nchi yetu, utafiti, ushauri, utumishi na malezi yako kwa mamia ya wanafunzi ambao sasa ni madaktari katika eneo hili muhimu la afya kwa nchi yetu,” ameandika Rais Samia.

Tuzo hiyo inayotambulika kwa jina la ‘Harvard T.H Chan School of Public Health Alumni Merit Award 2024’ hutolewa kwa aliyewahi kuwa muhitimu wa chuo hicho mashuhuri kwa wanafunzi ‘vipanga’ duniani na aliyejitoa kwa ajili ya afya ya jamii.

Profesa Manji akiwa Mtanzania wa kwanza kupata tuzo hiyo, ataipokea Septemba 27, 2024, mjini Boston, Marekani.

Related Posts