Simba mkao wa kula leo Afrika

Dar es Salaam. Dakika 90 za mchezo wa ugenini dhidi ya Al Ahli Tripoli leo kwenye Uwanja wa Juni 11, Tripoli, Libya zinapaswa kutumiwa vyema na Simba ili ijiweke katika mazingira mazuri ya kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Kupata ushindi au hata sare katika mechi hiyo itakayoanza saa 2:00 usiku kutairahisishia Simba kazi kwenye mechi ya marudiano ambayo itachezwa Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kinyume na hapo, Simba itakuwa na mlima mrefu wa kupanda nyumbani wiki ijayo ili itimize lengo la kwanza ambalo ni kuingia hatua ya makundi.

Simba inasaka tiketi ya kuingia hatua ya makundi kwenye mashindano ya klabu Afrika kwa mara ya tano mfululizo baada ya kufanya hivyo katika misimu ya 2020/2021, 2021/2022, 2022/2023 na 2023/2024.

Kwenye Kombe la Shirikisho, Simba ilitinga hatua ya makundi mara moja ambapo ni msimu wa 2021/2022 iliposhia hatua ya robo fainali ambayo ilifungwa kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi baina yao.

Uimara wa kitimu ambao Simba imeanza kuupata mwanzoni tu mwa msimu hapana shaka unaipa matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika mchezo huo wa leo dhidi ya Ahli Tripoli.

Hilo linathibitishwa na mechi za kimashindano ambazo Simba imeshacheza msimu huu ambapo imekuwa hairuhusu nyavu zake kutikiswa kirahisi lakini pia yenyewe imekuwa ikipachika mabao.

Katika mechi nne za kimashindano ambazo imecheza msimu huu, Simba imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu ikiwa ni wastani wa bao 0.3 kwa mchezo.

Na imefunga mabao nane katika mechi hizo nne ikiwa ni wastani wa mabao mawili kwa mechi.

Wakati Simba ikionekana kuwa imara pande zote, Al Ahli Tripoli yenyewe inaonekana kuwa dhaifu katika safu ya ulinzi.

Katika mechi 10 zilizopita za mashindano tofauti, Al Ahli Tripoli imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10 ikiwa ni wastani wa bao moja kwa kila mchezo.

Kudhihirisha kwamba timu hiyo imekuwa na makosa yanayojirudia kwenye safu ya ulinzi, ni mechi moja tu kati ya hizo 10 ambayo ilimaliza bila kuruhusu bao (clean sheet) lakini nyavu zake zimetikiswa katika mechi tisa mtawalia.

Hata hivyo, Simba inapaswa kuwa imara katika ulinzi kwani silaha kubwa ya Al Ahli Tripoli ni safu yake ya ushambuliaji ambayo imekuwa moto wa kuotea mbali katika kufumania nyavu za timu pinzani na kwenye mechi hii inaweza kumtegemea mshambuliaji, Agostinho Cristóvão Paciência, maarufu kama Mabululu ambaye amekuwa akiitumikia timu ya Taifa ya Angola kutokana na kiwango cha juu na uzoefu ambao amekuwa nao kwenye michuano ya kimataifa Afrika.

Idadi ya mabao 16 ndio imefungwa na timu hiyo ya Libya katika mechi zake 10 zilizopita ikiwa ni wastani wa bao 1.6 kwa mchezo.

Al Ahli Tripoli ni miongoni mwa timu ambazo zimekuwa zinautumia vizuri uwanja wa nyumbani kwenye mechi za kimataifa ambapo mara nyingi imekuwa ikipata matokeo ya ushindi na huwa nadra kupoteza.

Mechi 10 zilizopita za mashindano ya kimataifa ambazo Tripoli imecheza nyumbani, imeibuka na ushindi mara saba, kutoka sare mbili na kupoteza mchezo mmoja, ikifunga mabao 18 na kufungwa mabao saba.

Simba imekuwa haina historia nzuri na mechi za ugenini kwenye mashindano tofauti ya klabu Afrika na kudhihirisha hilo, mechi 10 zilizopita ambazo Simba haikuwa nyumbani, imepata ushindi mara moja tu, kutoka sare nne na kupoteza mechi tano, ikifunga mabao matano na kufungwa mabao 11.

Ardhi ya Kaskazini mwa Afrika ndio imekuwa ngumu zaidi kwa Simba pindi iendapo kucheza mechi huko kwani imekuwa ni jambo gumu angalau hata kupata matokeo ya sare.

Katika mechi 10 zilizopita ambazo Simba imecheza dhidi ya klabu kutoka Kaskazini mwa Afrika, haijapata ushindi hata mara moja, ikitoka sare mbili na kupoteza michezo nane mtawalia huku ikifunga mabao mawili tu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids na wachezaji wa Simba wamesema kuwa wamejiandaa vizuri kwa ajili ya mechi ya leo ugenini.

“Nimewaambia wachezaji wangu kuwa, hii mechi ya leo wanatakiwa kutumia nafasi, kwani ni mechi ambayo haitawapa upenyo wa wao kuchezea au kupata fursa ya kufunga kirahisi.

“Lakini pia wapinzani wetu wana wachezaji wenye uzoefu mkubwa, hivyo ni lazima wachezaji wangu watumie kila nafasi na ikiwezekana tuanze kufunga sisi kwanza,” alisema Davids.

Beki wa kulia Kelvin Kijili alisema kuwa, wamefanya mazoezi ya kutosha na wanachokisubiri kwa sasa ni mechi tu.

“Mpinzani wetu yuko vizuri ila hatuna shaka na hilo kwa sababu Simba ni timu kubwa na ina wachezaji wenye uwezo pia.

“Kocha ametutoa hofu na kutuonyesha kuwa anatuamini bila kujali tuna uzoefu wa kiasi gani katika michuano ya kimataifa na kiukweli tunaamini tutafanya makubwa,” alisema Kijili.

Related Posts