NYOTA wa zamani wa Polisi Tanzania, Gerald Mathias Mdamu tabasamu la matumaini limerejea usoni mwake baada ya juzi Ijumaa kufanyiwa upasuaji na kushukuru kwa kila aliyechangia kufanikisha matibabu hayo kwa kusema ‘Ahsanteni sana’.
Mdamu ametoa kauli hiyo akiwa bado amelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akisubiri kutengemaa kwa afya yake ili kurudi kwenye shughuli zake kwa ajili ya kuitunza familia yake.
Akizungumza na Mwanaspoti baada ya upasuaji huo, Mdamu alisema anawashukuru Watanzania wote waliojitoa kuhakikisha anatibiwa, jambo analoona ni kama ndoto katika maisha yake.
Mwanaspoti ambalo limekuwa bega kwa bega na mchezaji huyo wa zamani wa Mwadui FC tangu lilipomtembelea nyumbani kumjulia hali na kuibua hali yake na wadau kujitokeza, alisema anaona tumaini jipya katika maisha yake, kwani upasuaji aliofanyiwa umeenda vyema, lakini kubwa ni kumshukuru Mungu na wote waliomsaidia hadi sasa, hususani timu ya Mwanaspoti kwa kuibua upya hali yake kiafya kwani alikuwa akiteseka.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Rais Wallace Karia liliitoa Sh1.5 milioni na Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji alitoa kiasi kama hicho, wakati Mwamnyeto Foundation iliopo chini ya kiungo wa Singida BS, Zawadi Mauya na nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto nayo ilijitolea Sh.1milioni) na watanzania wengine wamekuwa wakimtumia michango mbalimbali ya fedha kupitia akaunti yake ya lipa kwa namba.
Upendo na michango ambayo aliipokea, imefanya Mdamu kutamka kwa furaha akisema; “Watanzania hawajawahi kuniacha tangu nilipoumia kwa mara ya kwanza 2021, nawashukuru kwa moyo wao wa upendo.”
“Nashukuru sana gazeti la Mwanaspoti kwa kupaza sauti kwa Watanzania ambao wamekuwa na mwitikio wa kunisaidia, limeandika habari zangu tangu mwaka 2021, likaja kuibua hali yangu mwaka huu hadi natibiwa,” aliongeza Mdamu aliyeumia kwenye ajali ya gari la timu ya Polisi wakati timu hiyo ikiwa Ligi Kuu Julai 9, 2021 na kuvunjika miguu yote mwili kiasi cha kufanyiwa upasuaji.
Hata hivyo, hali yake ilikuwa haijatengemaa kwa maelezo alikuwa akiendelea kupata maumivu na majeraha ya mshono wa upasuaji kutoa usaha, kitu kilichofanya Dk Kennedy Nchimbi aliyempasua hapo awali kumuita tena hospitalini na kumfanyia uchunguzi upya kabla ya kueleza anahitajiwa kupasuliwa tena.
Mdamu alisema baada ya kufanyiwa upasuaji, moyo wake umepata amani, akiamini afya yake ikiimarika ataweza akafanya shughuli nyingine za kumtengenezea kipato cha kutunza familia aliyonayo.
“Hakuna kitu kibaya kukaa na wasiwasi, sitamani mtu yeyote apitie hali hiyo, ndiyo maana nakosa neno la kuwaambia Watanzania, kutokana na ukarimu wao kwangu, kunisaidia mimi wamesaidia watu waliopo nyuma yangu. Ahsanteni sana. Sina cha kuwalipa zaidi ya ahsante hii na Mungu atawalipa,” alisema Mdamu.