NYOTA watano wa timu ya taifa ya mpira wa Meza (Table Tennis) ni miongoni mwa waliochuana katika msimu mpya wa mashindano ya mchezo huo ya Kombe la Urafiki kati ya China na Tanzania.
Mashindano hayo yaliyofunguliwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian na Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha yalifanyika jana kwenye ukumbi wa hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam.
Miongoni mwa nyota wa timu ya taifa waliochuana ni pamoja na Neema Mwaisyula, Masoud Mtalaso na Amon Aman ambao wamewahi kuiwakilisha nchi kwenye mashindano mbalimbali ikiwamo ya Jumuiya ya Madola 2018 na mashindano ya Dunia na Afrika.
Yahya Mungilwa, akizungumza kwa niaba ya Katibu mkuu wa Chama cha Mpira wa Meza Tanzania (TTA), Agripina Habitch alisema wamekuwa wakishirikiana na China katika mashindano hayo kwa mwaka watatu sasa.
“Katika kipindi chote hicho wachezaji wetu wanapata nafasi ya kwenda China na kujifunza zaidi kuhusu mchezo huu ambao wenzetu wametuzidi, wako mbali na wanafanya vizuri kimataifa,”alisema Mungilwa
Mbali na kwenda kujifunza China, alisema pia wamekuwa wakipata vifaa vya kisasa vya mchezo huo kutoka China na wameweza kuvisambaza mashuleni ambako sasa mpira wa Meza inachezwa.
“Haya mashindano yametusaidia kuibua vipaji,” alisema.
Akifungua mashindano hayo, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian alisema yameongeza hamasa na kuendeleza urafiki wa nchi hizo mbili uliotengenezwa na viongozi wa mataifa hayo mawili tangu wakati wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“China Table Tennis inachezwa kwa kiwango bora, hapa Tanzania pia umeanza kufanya vizuri timu zake zinachuana kitaifa na kimataifa, tunaamini ushirikiano huu unakwenda kuwa chachu ya nchi hizi kufanya vizuri zaidi kwenye mchezo huu,” alisema.
Katibu Mkuu wa BMT, Neema Msitha aliyemwakilisha waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Damas Ndumbaro alisema mashindano hayo yanaongeza mshikamano na urafiki wa China na Tanzania.
“Tunapofanya mashindano kama haya, wanaonufaika zaidi ni sisi Watanzania, wenzetu wako mbali zaidi kwenye mchezo huu, hivyo tunapata mbinu na uzoefu pia,” alisema.
Zaidi ya wanamichezo 200 wa China na Tanzania wameshiriki kwenye mashindano hayo.