MIKUMI imeishinda tena Ngorongoro kwa mikimbio 11 katika mechi ya mwisho ya majaribio kwa nyota wa timu ya taifa wanaonolewa kwa ajili ya michuano ya kufuzu kombe la dunia inayoanza jijini wiki hii.
Dar es Salaam imeandaa michuano hiyo inayoshirikisha timu kutoka mataifa sita ya kiafrika kwa ajili ya kutafuta kucheza fainali za kombe la dunia kwa kriketi ya mizunguko 20, maarufu kama T20.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Chama cha Kriketi Tanzania (TCA), Atif Salim, Wachezaji nyota wa timu ya Taifa wamecheza mechi tano za majaribio wakijigawa kwa majina ya Mikumi na Ngorongoro.
Kwa kushinda mchezo wa mwishoni mwa juma, Mikumi wanakuwa wameshinda michezo minne huku Ngorongoro wakishinda mara moja.
“Yalikuwa ni majaribio mazuri ambayo yamewaandaa vyema wachezaji wetu kwa mechi zote za kufuzu,” alisema msemaji huyo wa TCA.
Katika mchezo wao wa mwisho, Mikumi ndiyo walioshinda kura ya kuanza na kufanikiwa kupiga mikimbio 155 huku wakidondosha wiketi 6 baada ya kumaliza mizunguko yote 20.
Timu ya Ngorongoro ilipigana kiume kujaribu kuzifikia alama za wapinzani, lakin haikuwezekana baada ya jitihada zao kugota kwenye mikimbio 144, wakipoteza wiketi 6 baada ya kumaliza mizuguko yote 20.
Amal Rajeevan ambaye alicheza bila kutolewa(not out) alikuwa bora katika mechio hiyo baada kutengeneza mikimbio 49 kwa timu ya Mikumi
Tanzania itaanza kampeni yake ya kufuzu kwa kucheza na Mali katika katika uwanja wa Dar Gymkhana.
Uwanja wa Leaders Club jijini pia ulikuwa na mazuri mwishoni mwa juma baada ya kushuhudia timu ya wasichana ya Chama cha kriketi chini ikiwazamisha wavulana wa Lions Academy kwa wiketi 8 katika mchezo wa Ligi ya Kriketi kwa vijana waliochini ya miaka 19.
Timu ya Lions Academy ndiyo waliopata kura ya kuanza na kufanikiwa kutengeneza mikimbio 127, walipoteza wiketi 5 baada ya kumaliza mizunguko yote 20 ya mchezo.
Kwa kutumia mizunguko 16 kati ya 20, wasichana wa TCA walifaulu kuwazidi wapinzani wao kwa kutengeneza mikimbio 131 huku wakipoteza wiketi 2 tu na hivyo kuandika ushindi wa wiketi 8.
Ingawa uhodari wao haukuisadia timu ya Lions kuwashinda madada wa TCA, Johnson David aliyetengeneza mikimbio 40 na Rehani Atil aliyeiongezea Lions mikimbio 37, walionyesha uwezo mkubwa katika upigaji wa mipira.