Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amewaasa Watanzania kuishi kwa kuvumiliana, kuheshimiana na kupendana kama ilivyoagizwa na vitabu vya Mungu.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Septemba 15, 2024 katika Kongamano la Tano la Ekaristi Takatifu Kitaifa lililofanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaaam.
“ Wote tuliokuja hapa tumesikia mahubiri mazuri, tumehubiriwa kuwa wamoja zaidi tukavimiliane zaidi na kuheshimiana kama Watanzania wamoja. Kuwa na mawazo tofauti kusitufanye tugawanyike Ekaristi Takatifu hii itufanye tuwe wamoja,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “ Tuwafundishe jamii tuliyonayo kuwa na huruma kwa watu wote wanaohitaji na muhimu zaidi kuwa na huruma na taifa letu la Tanzania.”
Akizungumzia kaulimbiu ya Kongamano hilo inayosema “Udugu Kuponya Ulimwengu, Ninyi Nyote ni Ndugu”, Dkt. Biteko amesema kuwa kauli mbiu hiyo ni muhimu na inawaunganisha watu pamoja.
Dkt. Biteko ameongeza “Tunapotoka hapa tuwafundishe watu, tuwe wapya Ekaristi Takatifu imetuagiza tuishi upya.
Aidha, Dkt. Biteko amewahimiza Watanzania kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Serikali za Mitaa utakofanyika Novemba 27, 2024 kwa kuchagua viongozi kulinga na sifa zao watakaosaidia kuleta maendeleo nchini.
Akihubiri katika misa takatifu wakati wa Kongamano hilo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) Askofu Wolfgang Pisa, amesema kuwa siku hiyo ni ya kuhitimisha Jubilei ya miaka 50 ya Jumuiya Ndogondogo katika majimbo yote nchini.
Askofu Pisa amesema kuwa kwa miaka mingi nchini Jumuiya Ndogondogo zimetumika kama chombo cha kuwafikia waumini wote na kuwa Ekaristi Takatifu tu ndio kiunganisho cha wakristo.
“ Hii ni sakramenti ya upendo hivyo tusibaguane kwa itikadi, rangi wala sababu zingine kwa kuwa sote tuna Mungu mmoja. Ndugu zangu twende katika sakramenti hii katika hali isiyo na dhambi, tumuombe Mungu sakramenti hii itubadilishe tuwe wapya.” Amesisitiza Askofu Pisa.
Aidha, Askofu Pisa amewashukuru waamini wa kanisa hilo kutoka majimbo mbalimbali nchini kwa kushiriki Kongamano hilo la Ekaristi Takatifu na kusema kuwa baada ya kulihitimisha Kongamano hilo la tano lilifofanyika kwa siku nne litakutana tena miaka minne ijayo katika Jimbo Kuu la Arusha.
Akitoa salama za Baba Mtakatifu, Balozi wa Vatican nchini Tanzania Askofu Mkuu Angelo Accattino amesema kuwa Kongamano hilo limeeleza umuhimu wa Ekaristi Takatifu kama kiini cha imani yao.
“Ekaristi inatuunganisha na kristo na ndugu zetu katika imani Ekaristi ina imarisha upendo wetu kwa Mungu. Naipongeza Serikali kwa kufanya matukio kama haya kwa uhuru na amani” Amesema Askofu Accattino.
Kongamano hilo limekonga nyoyo za maelfu ya waumini wa Kanisa Katoliki kutoka maeneno mbalimbali nchi nzima limehudhuriwa na mamia ya viongozi wa dini wakiwemo maaskofu, mapadre na watawa.
Ambalo limehudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. William Lukuvi, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mhe. Albert Chalamila.
Viongozi wengine ni Spika wa Bunge Mstaafu, Anne Makinda, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Emannuel Nchimbi na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhe. Tundu Lissu, Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika.