Dar es Salaam. Utata umegubika tukio la kifo cha tabibu, Dk Dismas Chami aliyekuwa akifanya kazi katika kituo cha afya cha Ulyankulu wilayani Kaliuwa Mkoa wa Tabora, baada ya mwili wake kukutwa eneo la Kombo Masai Kata ya Malolo mkoani humo, pembeni yake kukiwa na sindano.
Inaelezwa kuwa, Dk Dismas Chami (32), mkazi wa Ulyankulu aliondoka nyumbani kwake (Ulyankulu Kaliua) Jumatano ya Septemba 2, 2024 akimuaga mkewe kuwa anakwenda Tabora mjini kikazi na angerejea kesho yake. Hata hivyo hakurejea na simu zake hazikupatikana, mpaka mwili wake ulipookotwa Septemba 13, 2024 saa 3 usiku.
Jeshi la Polisi kupitia msemaji wake, David Misime limesema linashirikiana na wataalamu wengine wa uchunguzi kufuatilia kifo hicho.
Hata hivyo, Misime amesema katika taarifa hiyo kuwa marehemu alishajaribu kujiua mara mbili.
“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa, alishajaribu kujiua mara mbili,” amesema.
Katika taarifa hiyo, Misime amesema daktari huyo alimuaga mkuu wake wa kazi na mke wake Septemba 2, 2024 kuwa anaelekea Tabora kushughulikia akaunti yake ya benki iliyokuwa na changamoto na angelirejea Septemba 3, 2024.
“Septemba 4, 2024 hakupatikana kupitia mawasiliano yake ya simu. Septemba 10, 2024 Daktari Mkuu wa Kituo hicho cha afya akiambatana na mke wa Dk Dismas Chami walifika katika Kituo cha Polisi na kutoa taarifa ya kutokuonekana kwake toka Septemba 2,2024.
“Tarehe hiyohiyo Dk Dismas Chami alimtumia ujumbe mke wake kwa njia ya WhatsApp unaosema: nisamehe sana baada ya dakika chache sitakuwa nanyi duniani. Simamia kila kitu nilichoanzisha pesa zote zipo akaunti ya CRDB simamia na watoto wasome kwa heri,” amesema Misime.
Amesema baada ya ujumbe huo hakupatikana tena hadi alipopatikana Septemba 13,2024 saa tatu usiku akiwa amefariki dunia.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi, rafiki wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Elinaza Msuya amesema tukio hilo lina utata kwa sababu marehemu alikuwa ni msiri na hakupenda kuchangamana na watu.
Msuya aliyezungumza akiwa Moshi mkoani Kilimanjaro alikokwenda kuuguza ndugu yake, amesema amekuwa akiwasiliana na mke wa Dk Chami tangu alipotoweka.
“Awali hatukufikiria kwamba mambo yatafika huko, tukadhani labda huko alikokwenda Dk Chami kulikuwa na changamoto ya mtandao.”
“Ilipofika Jumapili (Septemba 8), tukajua atarudi kwa sababu Jumatatu ni siku ya kazi, lakini nayo hakutokea. Ikabidi Jumapili niwasiliane na mkewe nikamshauri akaripoti Polisi, kweli wakaenda wakapewa RB.
“Ilipofika Jumatano kuna meseji zilitumwa kwa namba yake, meseji ya kwanza ikasema “Nisamehe sana baada ya dakika chache sitakuwa nanyi duniani, simamia kila kitu nilichokianzisha.”