Wadau wataka elimu kwa wananchi kuhusu daftari la wakazi

Dar es Salaam. Tayari kipenga cha uchaguzi wa Serikali za mtaa kimepulizwa baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa kutangaza Novemba 27, 2024 ku­­fanyika uchaguzi huo.

Katika tangazo hilo, Mchengerwa aliwahamasisha kugombea nafasi za uongozi na kujitokeza kupiga kura.

“Tangazo hili limetolewa chini ya Kanuni ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ya mwaka 2024 pamoja na matangazo ya Serikali namba 571, 572, 573, 574 ya mwaka 2024,” alisema Mchengerwa.

Alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 145 na 146, inaeleza uwepo wa Serikali za mitaa pamoja na madhumuni yake ikiwamo kupeleka madaraka kwa wananchi.

Kwa mujibu wa kifungu cha 201(A) cha Sheria za Serikali za Mitaa, Mamlaka za Wilaya, sura namba 287 na kifungu namba 77(A), huongoza uchaguzi huo na viongozi wanaochaguliwa katika ngazi hii ni, wenyeviti wa vijiji.

Wengine ni wajumbe wa halmashauri ya vijiji, wenyeviti wa mitaa, wajumbe wa kamati za mitaa na wenyeviti wa vitongoji.

Hata hivyo, alisema katika uchaguzi huo, wagombea wote katika ngazi mbalimbali za uongozi wanatakiwa kuwa wanachama wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu.

Alisema uchaguzi wa mwisho wa Serikali za mitaa ulifanyika Novemba 2019, hivyo, uchaguzi mwingine unatakiwa kufanyika Novemba 2024, uandikishaji na uandaaji wa orodha ya wapigakura utaanza siku 47 kabla ya tukio la uchaguzi.

Kwa tangazo hilo, wananchi walihamasishwa kujiandikisha kupiga kura, kugombea na kushiriki katika uchaguzi huo ili kupata viongozi wa Serikali za mitaa kwa maendeleo ya nchi wakati kampeni zikitarajiwa kuanza Novemba 20 hadi Novemba 26.

Baada ya tangazo hilo rasmi, wadau wamekuwa wakitoa elimu kuhusiana na uchaguzi huo, ambayo pia hutolewa katika shughuli mbalimbali za kiserikali na za vyama vya siasa.

Pia, katika nyumba za ibada, viongozi wa dini wamekuwa wakiimba wimbo huo wa uchaguzi na kuwataka waumini kujitokeza kugombea muda utakapofika na kupiga kura kuchagua viongozi wanaowafaa.

Hata hivyo, inaelezwa bado idadi kubwa ya watu hawana uelewa kwamba ili kupiga kura katika uchaguzi huo itawapasa kujiandikisha katika daftari la wakazi.

Hilo linafafanuliwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo alipofanya mkutano wa kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wanaotoka kata za Buyuni, Chanika, Zingiziwa na Msongola, mkutano uliofanyika viwanja vya VDOP hivi karibuni.

Mpogolo aligusia uchaguzi huo huku akiwasihi wananchi kwenda kujiandikisha katika daftari hilo la wakazi.

“Sisi viongozi twendeni tukahamasishe watu kwenda kujiandikisha, kwenye daftari, mtu analopaswa kujiandikisha ni lile la mtaa husika,” anasema Mpogolo.

 “Tunapaswa kuwaelewesha wananchi kwamba kama unakaa mtaa mwingine huwezi kwenda kujiandikisha kwingine, pia kama hatujiandikisha katika daftari hili, basi hatutakuwa na haki ya kuchagua kiongozi.”

Diwani wa Zingizwa, Maige Maganga anasema wamekuwa wakitumia ziara hizo kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kushiriki uchaguzi huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mtaa wa Kimwani uliopo katika Kata ya Zingiziwa, Abdallah Timbaye anasema ofisini kwao wamekuwa wakikutana na makundi mbalimbali kuwapa elimu ya umuhimu wa kijiandikisha katika daftari la wakazi.

Makundi hayo ni pamoja na mama na baba lishe, bodaboda, vijana wanaokaa vijiweni, wafanyabiashara ndogondogo wakiwamo wamachinga.

“Hawa tunawafuata katika maeneo wanayofanyia shughuli zao tukijua wazi kuwa ndipo wanatumia muda mwingi, wanapokuwa mbali na majumbani mwao na kukosa muda wa kuja kwenye mikutano ya hadhara tunayoiandaa,” anasema Timbaye.

Ukiacha kuwafuata maeneo walipo, mwenyekiti huyo anasema wananchi hao wanapokwenda kupata huduma katika ofisi zao, huwa wakiwapa elimu hiyo.

“Kwa tulichokifanya mtaani kwetu, nina imani ikifika muda wa kuanza kujiandikisha, ni wazi kuwa watajitokeza kwa wingi kwa kuwa angalau elimu wanayo,” anasema mwenyekiti huyo.

Katika wito wake, anawaomba vijana wenzake kujitokeza katika uchaguzi huo na kueleza kuwa hawapaswi kuogopa, kwa kuwa kiongozi ni kuaminiwa na watu.

Pia, jingine ni kuwa na uhusiano ya karibu na jamii inayokuzunguka, kujishusha, kusikiliza kero zao na sio kuwa na mali kama ambavyo watu wanadhani.

Mwenyekiti Kata ya Buyuni, Mohammed Shakur, alitaka wananchi wasihamasishwe tu kujiandikisha lakini pia kuhamasishwa kuchagua viongozi watakaoona wanawasaidia katika kutatua kero zao.

“Mfano huku mtaani kumekuwa na kero kubwa ya kuuzwa kwa maeneo yakiwamo ya wazi, baadhi ya wenzetu wamekuwa wakishiriki katika michezo hiyo. Ni wakati wa wananchi kufanya uamuzi, nani anaweza kuwasaidia katika kulinda maeneo yao,” anasema Shakur.

Pia, anasema shughuli hiyo itakuwa bora zaidi ikianzia ndani ya vyama kwa kuhakikisha inaongeza wanachama, ili itakapofika uchaguzi iwe rahisi kwa wao kuchaguliwa.

Baadhi ya wananchi, wanasema bado hawajajua kama kuna madaftari mawili katika upigaji kura huo, baadhi yao walidhani ukishajiandikisha kwenye lile la kudumu la kupigakura ndio basi.

Farida Kimweri, mkazi wa Zingiziwa anashauri elimu hii isisitizwe ili wananchi wengi waweze kushiriki uchaguzi huo.

Yunus James, anasema bado baadhi ya wananchi wanaona uchaguzi huo ni kwa ajili ya chama tawala, hivyo mwamko hata wa kusikiliza elimu yake haupo kama inavyokuwaga kwa uchaguzi mkuu.

“Nadhani viongozi ngazi za mitaa, waongezewe nguvu ikiwamo rasilimali fedha katika kuweza kutoa elimu juu ya uchaguzi huo, kwa kuwa hawa ni watu walio karibu na wananchi, wana lugha wanaweza kuzungumza wakaelewana tofauti na wanaotoka juu. Kikubwa wawezeshwe ili kuifanya kazi hiyo kwa kiwango cha juu,” anasema James.

Mchambuzi na mshauri wa masuala ya kiuchumi na Kijamii, Oscar Mkude anasema shida anayoiona ni kwamba taarifa hazitolewi za kutosha kuhusiana na daftari hilo.

Mkude anasema changamoto nyingine anazoziona ni zile asasi zilizokuwa zikitoa elimu hiyo, sasa hivi hazifanyi kwa kuwa nyingi hazina hela.

“Nadhani katika hili, Serikali isihamasishe tu asasi zinazotaka kutoa elimu ya uchaguzi kujitokeza, lakini pia ipeleke fedha huko, kwa kuwa zenyewe zinaweza kufika hata maeneo yasiyofika,”anasema Mkude.

Bila kufanya hivyo, mchambuzi huyo anasema jambo hilo wataachiwa wanasiasa wenyewe ambao hawa wamekuwa wakitumia fursa ya mikutano yao ya hadhara kutoa elimu kwa wafuasi wao, hivyo kuwaacha pembeni wananchi wasio na ushabiki wa chama chochote.

Mchambuzi wa Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie anasema kuna mambo matatu yanayosababisha watu kutoona umuhimu wa kijiandikisha katika daftari hilo la wakazi.

Moja, anasema ni historia ya nchi hii, tangu enzi za mwalimu Serikali ilionekana ndio ina mamlaka ya kufanya kila kitu, hivyo wengi linapokuja suala la uchaguzi, inaona haliwahusu ni la Serikali.

Pili, ni kukosa elimu ya uraia, baadhi yao wanashindwa kuhusisha siasa na maisha yao ya kila siku.

“Yaani mtu hajui wabunge wanapokaa pale bungeni na kuamua mikopo kwa wanafunzi, ni kwa watu fulani, hiyo ni siasa ambayo itaathiri maisha yake.

“Lakini pia suala la kupata huduma za maji na umeme, hajui kama usipojitokeza kumchagua kiongozi bora atakayeweza kukuletea huduma hii, utaendelea kulalamika kuwa ni za shida,” anasema Dk Loisulie.

Jambo la tatu anasema ni maisha bado hayajawa magumu kiasi cha kuwafanya wachukue uamuzi.

Anasema ni kawaida mtu kwenda nyumba ya pili kuomba chumvi, nyanya au kitunguu cha kupika akapewa, jambo ambalo kwa nchi nyingine haya hayapo.

“Hivyo mimi nachoona ili kufika huku ni muda tu utasema, kwani hata sasa unaona maisha yamebadilika kwa kiasi kikubwa na sio kama ilivyokuwa huko nyuma,” anasema.

Ushauri wake, mhadhiri huyo wa Udom, anataka vyama vya siasa na asasi za kiraia kuendelea kuwekeza nguvu zaidi katika kutoa elimu ya uraia bila kuchoka.

Related Posts