Watu wafa katika mafuriko Ulaya ya Kati – DW – 15.09.2024

Mfumo wa shinikizo la chini unaoitwa Boris umesababisha mvua za siku kadhaa na mito kupasua kingo zake kuanzia Poland hadi Romania, ambapo idadi ya vifo iliongezeka hadi watano Jumapili. Mvua zaidi na upepo mkali unatabiriwa hadi angalau Jumatatu.

Baadhi ya maeneo ya Jamhuri ya Czech na Poland yalikabiliwa na mafuriko mabaya zaidi katika kipindi cha takriban miongo mitatu, huku miji ikiwahamisha maelfu ya wakaazi. Robo milioni ya nyumba katika Jamhuri ya Czech zilikatikiwa umeme.

Askari wa zima moto wa Austria aliuawa wakati akikabiliana na mafuriko kusini mwa nchini hiyo, alisema Naibu wa Kansela Werner Kogler, huku mamlaka ikiutangaza mkoa unaozunguka mji mkuu, Vienna, kuwa eneo la janga.

Mafuriko Austria
Barabara iliyofunikwa na maji Austria juu.Picha: Daniel Scharinger/IMAGO

Daraja liliporomoka katika mji wa kihistoria wa Poland wa Glucholazy karibu na mpaka wa Czech. Vyombo vya habari vya ndani vilisema nyumba moja ilisombwa na daraja kuporomoka katika mji wa mlima wa Stronie Slaskie, ambapo bwawa lilipasuka, kulingana na taasisi ya hali ya hewa ya Poland.

Wakazi katika baadhi ya maeneo yaliyofurika walikuwa wakijiandaa kwa hali kuwa mbaya.

Soma pia: Watu kadhaa wamekufa kutokana na mafuriko Ulaya ya kati

“Yumkkini itakuwa mbaya zaidi, kwa sababu walitoa taarifa kwamba maji yanatoka kwenye milima ya Jizera. Mvua ikinyesha huko, itafika hapa baada ya saa tano au sita,” alisema Ferdinand Gampl, mwenye umri wa miaka 84 mkazi wa eneo hilo. Kijiji cha Czech cha Visnova, kilomita 138 kaskazini mwa mji mkuu, Prague.

Polisi wa Czech walisema walikuwa wakiwatafuta watu watatu waliokuwa kwenye gari lililotumbukia kwenye mto Staric siku ya Jumamosi karibu na Lipova-lazne, kijiji kilichopo umbali wa kilomita 235 mashariki mwa Prague. Mvua katika eneo hilo imefikia takriban milimita 500 (inchi 19.7) tangu Jumatano.

Picha za shirika la habari la Reuters zilionyesha maji ya mafuriko yakitiririka Lipova-lazne na mji jirani wa Jesenik, na kuharibu baadhi ya nyumba na kubeba uchafu.

“Hatujui kitakachofuata,” alisema Mirek Burianek, mkazi wa Jesenik. “Mtandao wa intaneti haufanyi kazi, simu hazifanyi kazi … Tunasubiri nani atajitokeza (kutusaidia).”

Slovakia | Mafuriko
Mkazi akitembea katika barabara iliyofurika maji katika mji wa Stupava, ulioko kilomita chache magharibi mwa Bratislava, Slovakia, mnamo Septemba 15, 2024.Picha: Tomas Benedikovic/AFP/Getty Images

Mkazi wa Lipova-lazne Pavel Bily aliiambia Reuters mafuriko yalikuwa mabaya zaidi kuliko yale yaliyoonekana mwaka 1997. “Nyumba yangu iko chini ya maji, na sijui kama nitarejea tena,” alisema.

Soma pia: Ulaya ya Kati yakumbwa na mafuriko

Askari polisi na wale wa zimamoto walitumia helikopta kuwaondoa watu waliokwama katika wilaya hiyo. Kwa ujumla, zaidi ya watu 10,000 walikuwa wamehamishwa nchini humo, mkuu wa huduma ya zima moto aliambia televisheni ya Czech.

Mbaya kuliko kabla

Mkabala tu mpaka wa Poland, mtu mmoja alikufa katika kaunti ya Klodzko, ambayo Waziri Mkuu Donald Tusk alisema ndio eneo lililoathiriwa zaidi nchini humo baada ya kukutana na maafisa katika mji mkuu.

Mji wa Klodzko ulikuwa chini ya maji baada ya mto wa eneo hilo kuvuka viwango vya rekodi vilivyorekodiwa mnamo 1997, wakati mafuriko yalipoua watu 56 nchini Poland.

Jamhuri ya Czech | Mafuriko Prague
Lango maalum la kuzuwia mafuriko likijengwa mjini Prague, Jamhuri ya Czech, Septemba 13, 2024.Picha: IMAGO/CTK Photo

Maafisa katika eneo la karibu la Glucolazy waliamuru uhamishwaji wa mapema Jumapili ingawa juhudi za kulinda miundombinu ya mji huo zilishindwa kuzuia daraja kuporomoka.

Soma pia: Vifo kutokana na mafuriko Ulaya vyapindukia 150

Katika mji mkuu wa Hungary, Budapest, maafisa walitabiri mto Danube kuongezeka katika nusu ya pili ya wiki hii hadi zaidi ya mita 8.5 (futi 27.9), ukikaribia rekodi ya mita 8.91 (futi 29.2) mnamo 2013.

“Kulingana na utabiri, mojawapo ya mafuriko makubwa zaidi ya miaka iliyopita yanakaribia Budapest lakini tumejitayarisha kukabiliana nayo,” meya Gergely Karacsony alisema.

Related Posts