Unguja. Wakati eneo la Paje Mkoa wa Kusini Unguja likizidi kuwa maarufu kutokana na shughuli kubwa za utalii, kasi ya ongezeko la vijana, maarufu ‘Beach boy’ kelele za muziki na ujenzi holela, vinaelezwa huenda vikaanza kuathiri shughuli hizo kwa kuwakera wageni.
Hivi Karibuni mkuu wa mkoa huo, Ayoub Mohmaoud Mohamed alisema kumekuwapo na malalamiko ya mara kwa mara kuhusu vijana hao ‘Beach Boy’ kupora wake za wageni na kuwalaghai kufanya nao mapenzi jambo linaloleta taswira mbaya katika utalii.
‘Beach Boy’ ni vijana ambao hukaa maeneo ya fukweni na kutembeza watalii.
Kauli kama hiyo imetolewa tena leo Jumapili Septemba 15, 2024 na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga wakati akifungua hoteli ya nyota tano Samawa katika eneo la Paje.
Soraga amesema sekta ya utalii Paje imekuwa na mwamko mkubwa wageni wengi hupenda kutembelea katika eneo hilo lakini kuna changamoto ya Beach boy, kelele na baa zinazochipukia bila kufuata utaratibu mambo yanayohatarisha sekta hiyo.
“Tunatakiwa kusimamia nidhamu katika sekta hii lakini kwa Paje kuna changamoto nyingi ambazo tunatakiwa kushirikiana na Serikali kuzipatia ufumbuzi. Paje imekuwa kelele za muziki, baa zinazochipukia bila utaratibu imekuwa kawaida, Beach boy wameongezeka,” amesema.
Amewataka viongozi wa mkoa kushirikiana na wa wilaya, masheha wa shehia wakae vizuri kuyaweka sawa mambo hayo kwani kadhia hizo zikiachwa zikaendelea kwa muda mrefu hazina afya katika sekta ya utalii ambayo inahitaji utulivu na ukarimu.
“Ikiwa mgeni anakuwa anasumbuka kwa sababu ya Beach Boy au kwa sababu ya kelele ya muziki kwa kweli inaweza kufikia hatua wageni wakakataa kuja kwenye kisiwa hiki,” amesema Soraga.
Kuhusu ujenzi holela amesema umeongezeka na ndio maana kumekuwapo matukio mengi ya moto katika hoteli nyingi kwenye eneo hilo.
Katika kipindi cha mwaka jana zaidi ya hoteli tano zilizoezekwa kwa makuti zimeungua katika eneo hilo la Paje na baadhi ya watalii kuunguliwa vifaa vyao. Hata hivyo hakuna aliyeumia wala kupoteza maisha.
Pia ametumia fursa hiyo kuwataka wawekezaji nao kuwajibika kuhakikisha wanafuata taratibu kanuni na miongozo ya uwekezaji.
“Usianze ujenzi bila kibali tukifuata mipango miji inavyotakiwa itapendeza na itazidi kuvutia wawekezaji na wageni wengi.”
Amesema kadri wanavyoongezeka wageni lazima kuwe na miundombinu ya kutosha kama hoteli za kutosha na vyumba vya kutosha kwa ajili ya kuwalaza wageni ambalo bado ni changamoto kwa Zanzibar.
“Kwa hiyo hii ni jambo muhimu kuona wawekezaji wanaendelea kuongeza mahoteli hapa na Serikali itaendelea kufanya kila jitihada kuweka mazingira mazuri ya kikodi na yasiyo ya kikodi,” amesema.
Soraga amesema kwa sasa wapo kwenye hatua za kuandaa sheria mpya ya utalii ambayo itazidi kuweka mazingira bora zaidi kwa wawekezaji.
Mwekezaji wa hoteli hiyo, Riad Welly amesema ametumisha wastani wa Dola za Marekani 3 milioni (sawa na Sh8.192 bilioni) na ujenzi wake umetumia zaidi vifaa vya asili kutoka visiwani humo.
Amesema amevutiwa kuwekeza katika kisiwa hicho kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji, lakini ushirikiano anaoupata kutoka serikalini na jamii inayozunguka eneo hilo.
“Zanzibar ni sehemu moja nzuri katika uwekezaji, mipango yangu ni kuendelea kuwekeza kwani kuna ushirikiano mkubwa na wananchi wake wanaonyesha upendo,” amesema.
Naye Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii, Hafsa Mbamba amesema ujenzi wa aina hiyo wa hoteli bado haujawa katika maeneo mengi Zanzibar.
“Inaendana na dira nzima ya utalii endelevu kwa hiyo tunakaribisha miradi kama hii ambayo imezingatia mazingira na utamaduni wa Kizanzibari kwa sasa tumetoa kipaumbele katika ujenzi huu,” amesema.