WINGA Mtanzania anayeichezea Hua Hin City FC inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Thailand, John Mgong’os amesema atakuwa nje ya uwanja kwa wiki akiuguza jeraha la paja.
Nyota huyo alicheza kwa dakika zote 90 dhidi ya Hua Hin Maraleina ambapo timu yake ilifungwa bao 1-0 Septemba 08 ikiwa ni raundi za awali za michuano hiyo maarufu kama Thai League Cup.
Mgong’os alisema wiki ijayo Ligi inaanza na kwa mujibu wa daktari anaweza kupona na ndani ya wiki hizo huenda akawa sehemu ya kikosi.
“Wiki zilizopita tulicheza League Cup lakini kwa bahati mbaya nilishtua nyama za paja katika dakika za mwisho, nilivyofanyiwa vipimo nikaambiwa nimeshtua msuli wa paja na nitakaa nje kwa wiki moja naamini wiki hii nitarudi maana ligi pia ndio inaanza.
“Tunaomba Mungu timu yetu ya taifa ifuzu na sisi tunaweza kuwa moja ya sehemu ya historia nyingine kwa sababu hatujawahi kuchezea Stars.”
Winga huyo kwa misimu tofauti alicheza Ligi Daraja la Kwanza Tanzania 2021, Afrika Kusini Daraja la Tatu (2022), Falme za Kiarabu UAE Daraja la Pili (2023) na sasa Thailand.