PAMOJA na Singida Blac Stars kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa sasa ikiwa pia ni moja ya timu yenye mabao mengi kwa sasa, lakini kocha wa timu hiyo, Patrick Aussems ameonyesha kutoridhika kabisa na kuwataka washambuliaji kubadilika na kutumia nafasi wanazopata watakapovaana na Pamba Jiji.
Singida inatarajiwa kuvaana na Pamba kesho Jumanne kuanzia saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza na Aussems alisema angependa kuona wachezaji wa timu hiyo hawarudii makosa ya michezo iliyopita ya kutotumia nafasi inazotengeneza kupata mabao mengi zaidi.
Pamba iliyotoka suluhu na Azam FC juzi usiku ikiwa ni mechi ya tatu mfululizo tangu irejee Ligi Kuu msimu huu, itakuwa na kibarua kizito cha kuwazuia nyota wa Singida ambao katika mechi tatu zilizopita wamefunga jumla ya mabao sita na kufungwa mawili tu na kuifanya timu iongoze msimamo na alama tisa.
Aussems alikuwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi wakati Pamba ikicheza na Azam FC na kupata wasaa wa kuisoma vya kutosha, huku akisema mchezo wa kesho utakuwa mgumu kutokana na wenyeji wao kuwa katika presha ya kusaka ushindi wao wa kwanza katika ligi.
“Tumekuwa na kipindi kizuri cha mazoezi hapa Mwanza, na tumeimarisha sehemu muhimu kama safu yetu ya ushambuliaji. Tunahitaji kuwa na wastani mzuri wa kutumia nafasi, kwani si kila mchezo utatoa nafasi nyingi,” alisema Aussems na kuongeza;
“Nimezungumza na wachezaji wangu na tumekuwa na mipango maalumu ili kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa. Tunapaswa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na hatupaswi kuridhika na jinsi tulivyofanya vizuri katika michezo yetu mitatu ya mwanzo. Safari yetu bado ni ndefu.”
Huu utakuwa mchezo wa kwanza kwa Pamba Jiji na Singida BS kukutana katika ligi. Kwa kuangalia viwango vya timu zote mbili katika michezo mitatu ambayo kila mmoja amecheza, Aussems anakutana na wapinzani ambao ni wagumu kufungika, hawajaruhusu bao katika michezo hiyo.
Kocha wa Pamba, Goran Kopunović, alisema: “Tunatakiwa kuendelea kuwapa wakati mgumu wapinzani wetu kwa kuzuia kwa pamoja huku tukijitahidi kutatua changamoto ya upachikaji mabao. Sioni kama washambuliaji wangu wanashindwa; wanafanya kazi nzuri na mabao yatakuja.”
Mbali na mchezo huo wa mapema kesho, pia kutakuwa na pambano jingine litakalopigwa saa 10:00 jioni wakati Wagosi wa Kaya, Coastal Union itakapokuwa wenyeji wa Namungo Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam, huku timu zote zikiwa hazijaonja ushindi hadi sasa.
Namungo imepoteza mechi zote tatu za awali, wakati Coastal ilianza kwa sare ya 1-1 dhidi ya KMC na kufumuliwa 1-0 na Mashujaa, hivyo kufanya pambano hilo kuwa la aina yake kwa vile makocha Mwinyi Zahera na msaidizi wake, Ngawina Ngawina kuwahi kuinoa Coastal kwa vipindi tofauti.