Bakwata yafunguka matukio ya utekaji, Serikali yafafanua

Geita/Dar. Wakati Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) na wadau wengine wakisisitiza uchunguzi huru dhidi ya matukio ya utekaji na mauaji, Serikali imesema kwanza jamii inapaswa kujiuliza kwanini matukio hayo yanatokea kila unapokaribia uchaguzi.

Katika hoja yake hiyo, Serikali imesema ni rahisi kutupa lawama kwa Jeshi la Polisi juu ya matukio hayo, huku ikieleza badala ya kufanya hivyo ni vema wananchi waanze kutafuta jawabu la kwa nini yanatokea kila unapokaribia uchaguzi.

Akitoa salamu za Bakwata katika Baraza la Maulid lililofanyika mkoani Geita leo Jumatatu Septemba 16,2024,  Katibu Mkuu wa baraza  hilo,  Alhaji Nuhu Mruma alisema baraza hilo linaungana na Rais Samia Suluhu Hassan kulaani vitendo hivyo na wanavitaka vyombo vya ulinzi na usalama vifanye uchunguzi huru kubaini wale wote waliojitokeza kufanya uhalifu huo.

“Vyombo vya ulinzi na usalama vifanye uchunguzi huru kubaini waliofanya hivi dhamira yao ni nini na viende mbali zaidi ili kutafuta ufumbuzi na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Aliwasihi wanaofanya uchunguzi huo kutofanya upendeleo au kumkandamiza yeyote bali haki itendeke bila kujali itikadi za wanaofanya unyama huo.

“Tunaomba wananchi kuwa mabalozi wazuri wa kulinda na kuitunza amani yetu na kutokubali kutumika na yeyote kwa maslahi binafsi katika kuvuruga amani yetu,” alieleza.

Alhaji Mruma amesema: “Sisi viongozi wa dini tutakuwa mstari wa mbele kuendelea kupaza sauti zetu dhidi ya utekaji wa watu, mauaji, ukatili wa kijinsia, unyanyasaji na ukiukwaji wa haki za binadamu.”

Kilichoelezwa na Bakwata kinawiana na kilichosemwa juzi  Jumapili na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), waliolaani matukio hayo na kutaka uchunguzi ufanyike haraka.

Maaskofu hao walieleza hayo katika salamu zao zilizosomwa na Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Eusebius Nzigilwa kwenye kilele cha Kongamano la tano la Ekaristi Takatifu la Kanisa Katoliki, lililofanyika kwenye  Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

“Matukio yaliyotokea karibuni ya watu kutekwa na hata kuuawa, tunajiuliza nini kimetokea, Taifa letu limekosea wapi je, uongozi na mamlaka husika na vyombo vya ulinzi na usalama vimezidiwa nguvu na maarifa hadi kushindwa kudhibiti hali hii?

“Sisi maaskofu hatuamini kama makundi haya ya kihalifu yana nguvu kuliko vyombo vyetu ya ulinzi na usalama. Hivyo tunaviomba vyombo kutimiza wajibu wake ili kurudisha heshima yetu ya misingi ya udugu na amani,” alisema Askofu Nzigilwa.

Mbali ya Bakwata na TEC kutoa msimamo huo, Chadema, wadau wengine wa haki za binadamu na mabalozi zaidi ya 15 wanaoziwakilisha nchi zao nchini, wamelaani tukio hilo la watu kutekwa, akiwamo aliyekuwa kada wa Chadema, Ali Kibao aliyetekwa na kisha kuuawa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alikuwa mgeni rasmi kwenye baraza hilo la Maulid lenye lengo la kuadhimisha kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (Rehma na amani zimshukie), akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Katika hotuba yake, alisema badala ya kutupa lawama kwa Jeshi la Polisi kuhusu matukio hayo,  ni vema wananchi wakajiuliza kwa nini matukio hayo yanatokea kila inapokaribia uchaguzi.

Kwa mujibu wa mtendaji mkuu huyo wa Serikali, tangu awamu ya tatu hadi ya sasa,  matukio kama hayo hutokea, lakini swali linabaki kwa nini hutokea unapokaribia uchaguzi.

“Rais alitoa karipio juu ya yanayotokea ambayo hutokea kila kipindi fulani.Lazima tujiulize kwa nini yanajitokeza hasa unapokaribia uchaguzi,  nani anafanya? Ni rahisi kusema polisi, lakini muhimu tukatafakari kwa nini wakati huu na nani anafanya?” amehoji Majaliwa.

Katika mazingira hayo, amesema mafanikio ya ulinzi wa Taifa hayatafanikiwa kwa kuwategemea polisi pekee, badala yake kila mwananchi awajibike kuifanya kazi hiyo.

Ameejenga hoja yake hiyo kwa kurejea mwaka 2021, akisema kulikithiri matukio hayo mkoani Mtwara na Rais Samia aliunda tume ambayo matokeo yake ikawa ni kuundwa kwa Tume ya Haki Jinai.

Kwa sababu mkuu wa nchi ameshaelekeza, Majaliwa alisema Watanzania wanapaswa kuiamini Serikali kwa kuwa iko macho na imara.

Amesisitiza Serikali haitafumbia macho wanaolichokoza Taifa kwa matukio ya utekaji na mauaji, akisema hatua kali zitachukuliwa dhidi yao, huku akiwataka wananchi waendelee kuwa na imani.

Katika nyakati hizo, amesema yeyote atakayeona viashiria vya uvunjifu wa amani katika maeneo awe mstari wa mbele kutoa taarifa, kwani kinachohitajika sasa ni ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, amewataka wazazi na viongozi wa dini kutimiza wajibu wao katika malezi ya watoto ili Taifa liwe sehemu salama.

“Kila mmoja ana wajibu,  iwe taasisi za elimu au dini. Moja kati ya ajenda muhimu ni kuhamasisha Watanzania kulea jamii katika maadili mema ili kuepuka maovu yote,” amesema Majaliwa.

Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zubeir amewataka Waislamu kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa, huku wakiweka elimu mbele na kuilinda amani.

Katika hotuba yake hiyo, alisisitiza umuhimu wa maadili kwa mtu mmoja mmoja, akisema mwonekano wa mtu  unatosha kutafsiri  ni mwadilifu kiasi gani.

“Unakuta mtu mzima mwanaume anavaa bukta anazurura huku na kule anashangaa tunamcheka. Tunamcheka kwa sababu amevaa vazi lisilopaswa kuvaliwa naye,” amesema.

Sambamba na hayo, amesisitiza tabia za kujidhuru na kudhuru wengine ni kinyume na matakwa ya dini ya Kiislamu na maelekezo ya Mtume Muhammad (Rehma na amani zimshukie).

Baadhi ya waumini wakizungumzia matukio ya utekaji nchini walisema yanayotokea sasa ni ishara watu wameacha kumuamini Mungu na kuamini ushirikina.

Walisema ni jukumu la viongozi wa dini kuendelea kutoa elimu ya dini ili watu wamrudie Mungu.

Jumapili Hussein, amesema watu wamehamisha imani zao kutoka kwenye imani ya dini na kuamini ushirikina, ndio chanzo cha mauaji na matukio mabaya yanayokithiri  nchini kwa sasa.

Tukio la mwisho la utekaji watu lililoamsha hisia za wengi ni la mjumbe wa sekretarieti ya Chadema, Ali Kibao aliyekamatwa jioni ya Septemba 6, mwaka huu akiwa katika usafiri wa umma na siku moja baadaye mwili wake ukaokotwa Ununio jijini Dar es Salaam akiwa amefariki.

Kibao alitekwa na watu wenye silaha ndani ya basi ya Tashrif, eneo la Kibo Complex, Tegeta jijini Dar es Salaam akiwa safari kwenda nyumbani kwake mkoani Tanga.

Katikati ya kelele za wadau wakiwemo Chadema kuitaka Serikali kueleza yupo wapi kiongozi wake, mwili wake uliokotwa Ununio, ukiwa umeharibika na usoni akimwagiwa tindikali.

Mwili huo ulipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala kwa uchunguzi wa kitabibu na hadi sasa ripoti ya uchunguzi huo haijawekwa wazi.

Tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza uchunguzi wa haraka wa tukio hilo alilosema ni baya na matukio mengine na taarifa apelekewe.

Hatua hiyo ilisababisha Chadema iitake Serikali kuwatoa watu wote waliopotea kufikia Septemba 21 na isipofanya hivyo,  wataandamana kuanzia Septemba 23, katika Jiji la Dar es Salaam.

Hata hivyo, tayari Jeshi la Polisi limeshapiga marufuku juu ya maandamano hayo.

Kama una maoni kuhusu habari hii tuandikie kupitia Whatsapp 0765864917

Related Posts