Benki ya CRDB yafanikisha uwekezaji wa mradi wa zaidi ya Bilioni 790 kwenye uchimbaji wa madini ya grafiti Tanzania

“Benki ya CRDB tumejikita sana katika kusaidia miradi ya kimkakati inayochochea maendeleo endelevu na kuleta matokeo chanya yanayodumu. Ushiriki wetu katika Mradi wa Grafiti wa Mahenge unaonyesha imani yetu isiyoyumba katika fursa na uwezo wa Tanzania na Afrika kwa ujumla. 

 

Kwa kushirikiana na taasisi kubwa katika masoko mbalimbali, tunachokifanya katika mradi huu ni kuwa hatuwezeshi tu mnyororo muhimu wa usambazaji wa madini kwa ajili ya utengenezaji wa betri, bali pia tunawezesha jamii za wenyeji kupitia ajira, miundombinu, na fursa za kibiashara. Mradi huu ni ushahidi wa kile kinachoweza kupatikana tukiamua kuwekeza katika mustakabali wa Afrika.” alisema Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB.

Kushiriki kwa Benki ya CRDB katika kuwezesha mradi huu ni ishara tosha ya uwezo wa benki katika kufanikisha miradi mikubwa ambayo inaimarisha dhana ya uwepo wa kampuni za kizawa katika uwekezaji wa kigeni unaofanyika nchini. Ushiriki huu pia unadhihirisha uimara wa mashirikiano kati ya Benki ya CRDB na taasisi nyingine za fedha katika ukanda wa Afrika na Kimataifa.

Mradi huu unajumuisha pia taasisi nyingine mbili kutoka nchini Afrika ya Kusini ambazo ni

· Benki ya Maendeleo ya Afrika Kusini (DBSA) ambao watachangia Dola za Kimarekani milioni 59.6 katika uwezeshaji wote

· Shirika la Maendeleo la Viwanda (IDC) ambao watachangia Dola za Kimarekani milioni 53.4 katika uwezeshaji wote.

Uwezeshaji wa pamoja kupitia muungano huu wa taasisi hizi tatu unaofikia Dola za Kimarekani milioni 179, unasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza hatari ya Mradi wa Grafiti wa Mahenge kwa taasisi moja na hivyo kuonyesha imani kubwa na dhamira ya taasisi zinazoshiriki kusaidia miradi ya kimkakati inayochochea maendeleo endelevu na ukuaji wa uchumi.

“Tunafurahi sana kukamilika kwa mchakato wa kusaini makubaliano ya uwezeshaji wa Mradi wa Mahenge na wakopeshaji wa kiwango cha juu kama hawa. Kukamilika kwa mchakato huu ni hatua kubwa Black Rock kuelekea kuwekeza kikamilifu katika uendelezaji wa Mradi wa Grafiti wa Mahenge. Tunatarajia kufanya kazi pamoja na Benki ya CRDB, DBSA na IDC ili kuendeleza Mahenge kwa manufaa ya wadau wote,” alisema John de Vries, Mkurugenzi Mtendaji wa Black Rock ambao ni wamiliki wakuu wa Faru Graphite Corporation wakiwa na hisa za asilimia 86.

Mradi wa Faru Grafiti wa Mahenge unatarajiwa kuwa moja ya miradi ya aina yake, ukitarajiwa kuleta manufaa makubwa ya kiuchumi na kimazingira kwa nchi na dunia nzima kwa ujumla. Hii ni kutokana na kuwa madini ya graffiti yanatoa malighafi muhimu katika utegenezaji wa betri jambo litakalosaidia sana katika kupunguza uzalishaji wa kaboni duniani.

Mradi huu unatarajiwa kuunda zaidi ya ajira 500 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, kuchochea ujenzi wa njia ya umeme yenye kilovolti 220 kutoka Kituo cha Umeme cha Ifakara hadi eneo la Mahenge, ambapo pia utapeleka umeme kwa vijiji vya karibu katika wilaya za Mahenge na Ulanga. Mradi huu pia utaleta fursa kubwa za kibiashara kwa wasambazaji wa ndani, watoa huduma, na makandarasi katika mkoa wa Morogoro.

Related Posts