DC Mwanga aeleza maneno ya mwisho ya Askofu Sendoro

Mwanga/Dodoma. Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Mwanahamis Munkunda, amesimulia mazungumzo ya mwisho kati yake na Askofu Chediel Sendoro kabla ya kifo chake.

Amesema katika mazungumzo hayo, Askofu Sendoro alimshauri akachukue familia yake na ailete Mwanga ili waweze kupanga namna bora ya kuwatumikia wananchi wa Mwanga.

Munkunda amesema kauli hiyo ya Askofu ilikuwa ni ishara ya uzalendo wake na mapenzi yake kwa jamii, akionyesha dhamira ya dhati ya kuendelea kuwahudumia wananchi mpaka dakika za mwisho za maisha yake.

Munkunda, ambaye alihamishiwa Wilaya ya Mwanga katika uteuzi uliofanyika Septemba 2, 2024, ameeleza hayo leo, Septemba 16, 2024, wakati akitoa salamu za Serikali katika ibada maalumu ya kuaga mwili wa Askofu Sendoro, iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Dayosisi ya Mwanga.

Ibada hiyo ambayo ilihudhuriwa na maaskofu wa KKKT na makanisa mengine yanayounda CCT, viongozi wa dini mbalimbali na wa Serikali, ilitawaliwa na vilio na simanzi kutoka kwa mamia ya waombolezaji waliofika kushiriki ibada hiyo.

Askofu Sendoro ambaye alikuwa Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Mwanga, alifariki dunia Septemba 9, 2024 kwa ajali ya gari iliyotokea eneo la Kisangiro, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro saa 1:30 usiku, baada ya gari alilokuwa akiendesha aina ya Toyota Prado, akitokea Kileo kuelekea nyumbani Mwanga, kugongana uso kwa uso na lori.

Historia inaonesha Askofu Sendoro ndiye askofu wa kwanza wa Dayosisi ya Mwanga ambaye  aliingizwa kazini Jumapili ya Novemba 6,2016 baada ya kuzaliwa kwa Dayosisi hiyo mpya iliyotokana na kugawanywa kwa Dayosisi mama ya Pare.

Munkunda amesema; “Ujumbe wa  mwisho wa Askofu Sendoro, alinitumia Jumamosi ya Septemba 7, 2024 akiniambia nenda kachukue familia uje tufanye kazi, tuje tupange namna ya kuhudumia watu wa Mwanga.” 

Amesema Mwanga wamempoteza kiongozi shupavu na watakosa busara zake na namna alivyosimama kuwahudumia wananchi na kuwakimbilia wahitaji.

“Nimempoteza kiongozi mwenzangu ambaye tulijua tutaanza naye safari hii ya kuwatumikia wana- Mwanga na siku tulipopata taarifa ya ajali, tulipata ganzi na kuwaza tutaanza vipi ukurasa mpya bila Sendoro na tukawaza namna ya kuanza kushuka kwenye jamii kama aliyokuwa akishuka kuihudumia,” amesema Munkunda.

Aidha amesema moja ya mambo aliyoyafanya Mwanga ni kuchimba visima katika Kata ya Toloha na Mwanga mjini ili kukabiliana na changamoto ya maji iliyokuwa ikiwakabili wananchi.

“Mwaka 2023 tulikumbwa na tatizo la ukame, Askofu Sendoro alitoa zaidi ya Sh352 milioni kwa ajili ya kusaidia wananchi, lakini pia Juni mwaka huu tulipopatwa na mafuriko, baba huyu aliwakimbilia wananchi na kuwasaidia mahitaji mbalimbali ikiwemo ya chakula na magodoro ili kuwawezesha kurudi katika hali zao za kawaida,” amesimulia.

Hivyo, mkuu huyo wa wilaya amesema Askofu Sendoro hakuwa kiongozi wa kiroho tu, bali aliihudumia jamii nzima bila kutazama udini, ukabili, sura wala rangi.

Mwaipaya ashindwa kujizuia kulia

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdalla Mwaipaya ameelezea namna walivyofanya kazi kwa ushirikiano na Askofu Sendoro wakati akiwa mkuu wa Wilaya ya Mwanga huku akishindwa kujizuia kububujikwa na machozi, wakati akizungumza.

“Alikuwa kiongozi mwema aliyejali wananchi na kuwasikiliza changamoto zao na kushirikiana na Serikali kuzitatua. Tumempoteza kiongozi, hata alipoondoka aliniambia nikafanye kazi Mtwara kutumikia wananchi, na kunikabidhi kwa askofu wa kule ili tushirikiane,” amesema Mwaipaya huku akibubujikwa machozi.

Akihubiri katika ibada hiyo, Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kusini Mashariki mwa Ziwa Victoria (Shinyanga), Askofu  Yohana Nzelu amesema Askofu Sendoro katika huduma yake na maisha yake hakuwahi kubagua watu na wakati wote alihakikisha anawaunganisha.

“Baba Askofu Sendoro wakati wa maisha yake aliunganisha Kanisa na kuhudumia jamii iliyomzunguka, alijua kubalance (kuweka mizania) maudhui na hadhira wakati wote alipokuwa akizungumza, hakika hakuna anayeweza kupinga msingi imara uliowekwa na Sendoro katika dayosisi hii ya Mwanga,” amesema.

Wakati huo huo maziko ya Paroko wa Parokia ya Mkula Jimbo Katoliki la Ifakara, Padri Nicholaus Ngowi yanafanyika leo katika makaburi ya Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Manyoni mkoani Singida.

Padri Ngowi alifariki dunia papo hapo Septemba 9, 2024 katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Kikuru Wilaya ya Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro.

Ajali hiyo ilitokea baada ya gari lake aina ya Toyota Prado alilokuwa akiliendesha kugongana uso kwa uso na basi la Kampuni ya Kilenga.

Padri huyo alikuwa akitokea Ifakara mkoani Morogoro akielekea kijijini kwao Marangu mkoani Kilimanjari,  kwa ajili ya shughuli ya kifamilia iliyokuwa ifanyike Jumanne Septemba 10, 2024.

Mkuu wa Shirika la Damu Azizi ya Yesu Tanzania, Vedasto Ngowi akizungumza na Mwananchi alisema kabla ya kuelekea Manyoni, walifanya ibada ya kumuombea marehemu Parokia ya Makomu, Marangu mkoani Kilimanjaro.

“Jumanne Septemba 17 misa ya mazishi itafanyika katika Parokia ya Manyoni kuanzia saa nne asubuhi. Baadaye maziko yatafanyika katika makaburi ya wamisionari wa shirika letu,”alisema.

Related Posts