Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imewataka wamiliki wote wa vituo vya mafuta kutoruhusu uuzwaji wa mafuta ya petroli kwenye vifaa visivyoruhusiwa kuchukulia au kuhifadhia mafuta hayo.
Hata hivyo, baada ya wananchi waliozungumza na Mwananchi wamesema Ewura inapaswa kusimamia ujenzi wa vituo vya kuuzia mafuta maeneo ya pembezoni, ili wasilazimike kupata mafuta umbali mrefu zaidi ya kilomita 30.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Andilile amesema leo Jumatatu Septemba 16, 2024 kuwa vifaa hivyo kama madumu, chupa za aina zote na vifaa vingine haviruhusiwa kisheria.
Katika taarifa yake aliyoitoa leo, Dk Andilile amesema kufanya hivyo ni kuzingatia matakwa ya kanuni namba 27.
“Kwa mujibu wa kanuni namba 27 ya kanuni zinazosimamia biashara ya vituo vya mafuta za mwaka 2022 kama ilivyochapishwa katika Gazeti la Serikali Na. 150, wamiliki wote wa vituo vya mafuta wanatakiwa kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha kuwa usalama wa afya, mali na mazingira (HSE) unazingatiwa, ili kuepusha milipuko ya moto,” amesema.
Amesema katika siku za hivi karibuni, kumekuwapo na matukio ya milipuko ya moto yanayotokana na kuhifadhi ama kuuza mafuta ya petroli kwa kutumia madumu na chupa za plastiki, kinyume na tahadhari ya HSE.
Hivyo, amesema Ewura inatoa tahadhari kwamba wakaguzi wake watafanya ukaguzi, ili kubaini kama kanuni hiyo inazingatiwa ipasavyo. “Atakayekiuka agizo hili atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria, ikiwamo kukifungia kituo husika.”
Uuazaji wa mafuta katika vidumu au chupa umeshamiri maeneo ya pembenzoni mwa miji kwa kile kinachoelezwa na wadau ni vituo vya mafuta kuwa mbali na makazi yao.
Mkazi wa Kaliua, Mkoa wa Tabora, Frank Bahati akizungumza na Mwananchi amesema maeneo ya vijijini hali hiyo ipo na kuizuia ni changamoto.
“Fikiria sisi ili kufikia kituo cha mafuta ni zaidi ya kilomita 30, sasa una bodaboda uchome mafuta hadi kuyafuata huko kweli? Hali hii ndio inawafanya wafanyabiashara kuyauza kwa njia hiyo,” amesema Bahati na kuongeza:
“Ili kulimaliza suala hili, Ewura wahakikisha wanasimamia ujenzi wa vituo vya kuuzia mafuta maeneo mengi, lakini kama hali hii ya vituo kuwa mbali na wananchi bado vitaendelea,” amesema.
Hoja ya Bahati imeungwa mkono na mkazi wa Kijiji cha Kifula, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, Fredrick Joseph anayesema kuna kipindi kulikuwa na kampeni ya watu kujenga vituo kwa kuwakopesha watu.
“Hii ingetekelezwa kwa ufanisi kwa watu kukopeshwa na ujenzi ukifanyika, itakuwa suluhu lakini kama hakuna vituo bado hali hii itaendelea,” amesema Joseph.