Ivo: Tulieni, tunaenda Ligi Kuu

KOCHA wa Songea United, Ivo Mapunda amesema licha ya muda mfupi waliokaa kambini kwa maandalizi ya msimu huu, lakini vijana wake wako tayari kwa Championship na Mbeya Kwanza watarajie kipigo, kwani kiu waliyonayo ni kuona mkoa wa Ruvuma unakuwa na timu ya Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Songea United inajiandaa na Championship kwa msimu wao wa kwanza baada ya mabadiliko ya jina na uongozi kutoka FGA Talents iliyokuwa jijini Dodoma na sasa makazi yao ni mkoani Ruvuma na awali ilithibitisha kumsainisha Kocha Mohamed Badru kabla ya dili kutibuka ghafla na sasa Mapunda ndiye anasimamia kila kitu wakati mabosi wakisaka kocha mkuu.

Hata hivyo, inaelezwa mazungumzo baina ya vigogo wa timu hiyo na Malale Hamsin tayari yameanza na bado anajifikiria kwa dau alilowekewa mezani.

Songea United inatarajia kushuka uwanjani kuwakaribisha Mbeya Kwanza katika mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo, utakaopigwa uwanja wa Majimaji, mjini Songea.

Mapunda alisema kwa takriban wiki nne walizokaa kambini, ameona utayari wa nyota wake kupambania timu hiyo na dhamira yao ni kuwakilisha vyema Ruvuma kupata Ligi Kuu.

Alisema usajili walioufanya ni wa kuridhisha, hivyo shughuli itaanza rasmi Septemba 21 dhidi ya Mbeya Kwanza na matarajio yao ni kushinda ili kuanza kampeni ya kuisaka Ligi Kuu.

“Vijana wako tayari, tumekuwa na muda mchache lakini wenye faida kujiweka fiti, tumecheza mechi kadhaa za kirafiki na tumefanya vizuri, tunaenda kuianza safari ya Ligi Kuu,” alisema staa huyo wa zamani.

Related Posts