Kijana unafanya mazoezi au unasubiri ‘Six Pack’ baa?

Dar es Salaam. Ingawa kwa baadhi yetu mazoezi ni jambo la kila siku, wale wenzangu na mie angalau ifanye leo iwe siku itakayouchangamsha mwili wako kwani ndiyo maalumu kwa ajili ya mazoezi.

Msingi wa muhtasari huo ni uhalisia kuwa, leo Septemba 16 dunia inaadhimisha siku ya mazoezi kwa vijana, kwa lugha ya wenzetu ni ‘Teenager Workout Day’ ambayo huadhimishwa kila mwaka.

Siku hii ni maalumu kwa kuangazia umuhimu wa mazoezi ya mwili na kuwahamasisha vijana kuishi maisha yenye afya kupitia shughuli za kimwili.

Haijalishi utayafanya wakati gani iwe jioni au asubuhi, lakini usisahau kuwa leo ni siku maalumu ya mazoezi kwa vijana.

Haujapangiwa ni kijana wa jinsia gani utafanya naye mazoezi, zingatia ni siku yenu vijana.

Ripoti ya Tanzania Youth Well-being ya mwaka 2022, inaonyesha asilimia 40 ya vijana nchini hawafanyi mazoezi ya kutosha.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kutofanywa mazoezi kunaenda sambamba na ongezeko la matatizo ya uzito kupita kiasi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo kisukari na shinikizo la damu.

Ripoti hiyo inaonyesha karibu asilimia 20 ya vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 wana uzito uliopita kiwango kinachokubalika kiafya, jambo linaloashiria tatizo la mtindo wa maisha usiohusisha mazoezi ya kutosha.

Aidha, katika utafiti uliofanywa mwaka 2022 na Global Health Observatory (GHO), ilibainika asilimia 80 ya vijana duniani kote hawafanyi mazoezi ya kutosha kwa kiwango kinachopendekezwa.

Siku ya mazoezi kwa vijana ilianzishwa na mkufunzi wa mazoezi, Greg Bouskila, mwaka wa 2018, ikiwa ni suluhisho la changamoto la ongezeko la unene kupita kiasi miongoni mwa vijana na kupungua kwa kiwango cha shughuli za kimwili.

Siku hii inakumbusha umuhimu wa mazoezi kwa vijana na inalenga kupambana na unene wa kupita kiasi, kadhalika kukuza tabia bora za kiafya zinazodumu maisha yote.

Katika ulimwengu ambao maisha yasiyo na shughuli za mwili na ulaji usio sahihi unazidi kuongezeka, siku ya mazoezi kwa vijana ni ukumbusho si tu wa kupambana na unene kupitiliza, bali pia kuipa akili afya kwa kuushughulisha mwili.

Mazoezi ya mara kwa mara yameonyesha kupunguza msongo wa mawazo, kuboresha kumbukumbu, kudhibiti tabia zisizofaa, kupunguza wasiwasi na kuongeza kujiamini.

Wataalamu wa afya akiwamo Mhadhiri wa Utafiti wa Afya na Mbinu za Ubora Emma-Louise, ‘Emmilie’ kutoka Chuo Kikuu Havard, wanakubaliana kuwa mazoezi ni muhimu kwa vijana.

Kujihusisha na shughuli za mwili husaidia kujenga uvumilivu, kuipa nguvu misuli, afya ya moyo na mapafu. Aidha, inachangia afya ya akili kwa kutoa homoni ya endorphins ambazo hupunguza viwango vya msongo wa mawazo.

Inashauriwa kwa vijana kufanya shughuli za mwili kwa angalau dakika 60 kwa siku, ikijumuisha mchanganyiko wa mazoezi ya arobiki, mazoezi yanayokaza misuli na mazoezi yanayokaza mifupa. Kuanzisha tabia hizi mapema husaidia kujenga msingi mzuri wa maisha yenye afya hadi utu uzima.

Siku ya mazoezi kwa vijana ilianzishwa ili kupambana na kuongezeka kwa kiwango cha unene kupita kiasi miongoni mwa vijana.

Katika mwaka 2017, vifo vinavyohusiana na unene kupita kiasi viliripotiwa kuwa zaidi ya milioni nne duniani, ikionyesha dharura ya kushughulikia tatizo hili.

Kwa karibu asilimia 20 ya watoto na vijana wa Marekani kati ya umri wa miaka miwili hadi 19 kuwa na unene kupita kiasi kati ya mwaka 2017 na 2018, juhudi za Greg Bouskila zilikuja wakati muafaka.

Related Posts