Kilwa. Wanachi wanaoishi katika Wilaya za Kilwa na Ruangwa wameiomba Serikali kuwasaidia kurejesha mawasiliano ya miundombinu ya daraja la Mto Mbwemkuru linalounganisha wilaya hizo lililoathiriwa na mvua kubwa zilizonyesha mkoani Lindi.
Akizungumza jana Septemba 15, 2024 wakati Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya alipotembelea madaraja yaliyoathiriwa na mvua hizo mkoani Lindi, mkazi wa Ruangwa, Abdallah Kawingu amesema kutokana na changamoto ya daraja hilo, baadhi ya vyakula vimepanda bei kutokana na miundombinu kuwa mibovu.
“Sasa hivi hadi unga wa kiroba cha kilo 25 tunanunua Sh50,000, awali tulikuwa tunanua Sh27,000 hadi Sh30,000, tunaiomba Serikali itusaidie urejeshwaji wa daraja hilo kwa kuwa ndiyo sehemu kubwa tunayoitegemea katika mawasiliano ya kutoka Kilwa kwenda Ruangwa na kutoka Ruangwa kwenda Kilwa,” amesema Kawingu.
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telack, akitoa taarifa kwa naibu waziri huyo, amekiri kuwepo kwa changamoto ya miundombinu, hasa madaraja ya Mto Mbwemkuru pamoja na daraja la Mto Nakiu ambayo yameharibiwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha mwaka huu ikiambatana na kimbunga Hidaya.
“Daraja hili baada ya kuharibika, wananchi walikuwa wanavushwa na mtumbwi, lakini mvua hizi zimechangiwa na maji ambayo yalikuwa yanatoka Mkoa wa Morogoro na kuja huku kwetu, lakini pia mkoa wetu una eneo kubwa la bahari,” amesema Telack.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Kasekenya amesema wizara imetenga Sh22 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa madaraja mawili yatakayoondoa changamoto zote za miundombinu hiyo.
“Hizi Sh22 bilioni zitatumika katika madaraja mawili, daraja la Mto Mbwemkuru litagharimu Sh13 bilioni na daraja la Mto Nakiu litagharimu Sh9 bilioni na ujenzi wake utakapoanza hautasimama, niwaombe wananchi wa Ruangwa na Kilwa kuwa wavumilivu kwa kipindi hiki Serikali inajua changomoto mnazopitia, zitakwenda kumalizika,” amesema Naibu Waziri.
Kasekenya amesema kwa sasa Mto Mbwemkuru daraja lake litafanyiwa marekebisho, ili kurudisha mawasiliano kwa muda huku wakiwa wanajiandaa na daraja ambalo litajengwa la kudumu.
Mvua kubwa zilizonyesha mkoani Lindi, zikiambatana na kimbunga Hidaya zilisababisha uharibu wa miundombinu mingi, ikiwemo madaraja yanayounganisha baadhi ya wilaya pamoja na kukatika kwa mawasiliano ya barabara.