Latra yatishia kufungia leseni madereva

Mbeya. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) mkoani hapa, imesema haitasita kuwafutia leseni madereva wanaokaidi kufuata sheria za barabarani, huku ikiwasihi wananchi kuzingatia usalama wao wanaposafiri.

Latra kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani humo, inaendesha operesheni maalum ya kukagua magari yenye makosa mbalimbali kama uchakavu, ukosefu wa vidhibiti mwendo na madereva wasiokidhi vigezo vya uendeshaji.

Operesheni hiyo iliyofanyika kwenye wilaya zote za mkoa wa Mbeya, imekuja ikiwa kumetokea mfululizo wa ajali  mapema mwezi huu zilizosababisha vifo vya watu 21 na kujeruhi zaidi ya 50.

Ofisa Mfawidhi wa Latra, Shaban Mdende ameiambia Mwananchi kuwa madereva wanaokaidi sheria watachukuliwa hatua kali ikiwa ni pamoja na kufutiwa leseni.

Amesema lengo la mamlaka hiyo ni kuhakikisha vyombo vya usafiri vilivyosajiliwa kisheria vinatoa huduma bora kwa wananchi. “Wananchi toeni taarifa pale mnapoona uzembe kwa dereva.”

“Kabla ya kufikia uamuzi wa kuwafutia leseni, tunaanza na kutoa elimu kisha onyo. Wale wanaokaidi zaidi ndipo hatua kali huchukuliwa. Tunataka Mbeya iwe salama na yenye usafiri bila ajali zisizo za lazima,” amesema Mdende.

Aidha, amesema kuwa operesheni hiyo haikujikita tu katika kukagua magari bali pia ilihusisha utoaji wa elimu kwa madereva, ikiwa ni pamoja na kuepuka kupandisha nauli kiholela, kutoa risiti sahihi na kuhakikisha majina yaliyopo kwenye tiketi za abiria ni halisi.

“Tumebaini baadhi ya magari yanazidisha abiria kinyume na leseni zao, kupandisha nauli kiholela na kutotoa risiti sahihi. Tumetoa elimu kwa madereva na abiria juu ya haki zao na taratibu sahihi za usafiri,” amesema Mdende.

Kaimu Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Ansgar Komba amesema jumla ya madereva watano walifutiwa leseni kutokana na makosa mbalimbali na kwa muda wa siku saba za operesheni hiyo, hakujatokea ajali yoyote.

Amebainisha kuwa magari yasiyokuwa na ubora yalifichwa kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo.

“Baada ya operesheni hii, tunatarajia kuona Mbeya yenye utulivu, madereva wanaofuata sheria na magari yaliyokidhi vigezo yakitoa huduma bora kwa wananchi,” amesema Komba.

Mmoja wa madereva, Yusuph John ameeleza kuwa changamoto si madereva kukaidi sheria, bali ni wamiliki wa magari kutozingatia baadhi ya masharti, jambo linalowalazimu kufanya makosa ili kulinda ajira zao.

“Yapo makosa tunayofanya kama madereva, lakini mara nyingi tunafuata matakwa ya waajiri wetu. Hali ya maisha ni ngumu, hatuwezi kukubali kupoteza ajira zetu,” amesema Yusuph.

Naye abiria Deborah Fumbo amebainisha kuwa wakati mwingine mazingira magumu husababisha madereva kuzidisha abiria. “Mfano leo, kutokana na siku kuu ya Maulid, kulikuwa na uhaba wa usafiri, hivyo abiria wanapanda magari bila kujali idadi ya watu ndani na hilo linakuwa faida kwa dereva,” amesema Deborah.

Related Posts