Maofisa mawasiliano wataka kuthaminiwa ndani ya EAC

Dar es Salaam. Nafasi ndogo wanayopewa wataalamu wa uhusiano na mawasiliano  wa nchi za Afrika Mashariki kuwashauri viongozi wa Serikali na taasisi za umma, imetajwa kuchochea kauli kinzani zinazoibua migogoro baina ya nchi moja na nyingine.

Imeelezwa kuwa, licha ya taaluma walizonazo kuhusu masuala ya uhusiano na mawasiliano, kwa bahati mbaya hawatumiki kushauri viongozi namna ya kuwasiliana kwa masilahi ya Taifa au kikanda.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Septemba 16, 2024 na Chama cha Maofisa Uhusiano na Mawasiliano Tanzania (PRST), kilipozungumza na Mwananchi kuhusu maandalizi ya mkutano wa kujadili nafasi zao ambao utafanyika Tanzania.

Katibu Mkuu wa PRST, Ndege Makura amesema taaluma zao kuingiliwa na wanasiasa ni jambo lingine linalowaweka kwenye nyakati ngumu,  hivyo kuathiri mawasiliano na uhusiano.

Kutokana na mazingira hayo, wanataaluma hiyo kutoka nchi za Afrika Mashariki watakutana kwa wiki moja jijini Arusha kuanzia Septemba 23 hadi 27, mwaka huu, kujadili nafasi zao na namna watakavyoshirikishwa kwenye masuala ya mawasiliano ndani ya jumuiya hiyo.

Huo utakuwa mkutano wa tatu wa wanataaluma hao, wa kwanza ulifanyika Mombasa nchini Kenya na mwingine Jinja nchini Uganda.

Makura  amesema kwa sehemu kubwa kauli kinzani, hotuba zinazoibua utata na migogoro baina ya nchi na nchi ndani ya jumuiya hiyo, zinakosa utaalamu wa mawasiliano.

Kukosekana kwa utaalamu huo, kunatokana na kile alichoeleza kuwa, wataalamu wa uhusiano na mawasiliano wapo, lakini hawatumiki kutekeleza majukumu hayo.

“Kwa sababu hiyo, tunataka msimamo wa kitaaluma ndani ya jumuiya hiyo na kupata nafasi ya kuwa waangalizi wa mawasiliano.

“Ajenda kuu ni nafasi ya maofisa uhusiano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), lakini changamoto za kimawasiliano zinazoikabili jumuiya hii na kupendekeza suluhisho lake,” amesema.

Makura amesema pamoja na mambo mengine, wanataka katika migogoro inayoendelea ndani ya EAC nafasi ya wanataaluma hiyo itambulike katika kusaka suluhu au kushauri.

Amesema mkutano huo pia, unalenga kuhakikisha elimu kuhusu jumuiya hiyo inatolewa kwa wananchi wa mataifa yote wanachama.

“Tunacholenga ni kuwa na mijadala mbalimbali, mitazamo inayoendana na mikakati madubuti ya kuhakikisha wananchi wanajua umuhimu na manufaa ya kuwa na jumuiya,” amesema.

“Hata kauli za viongozi wa jumuiya hizo juu ya kurushiana lawama na kugombana wakati mwingine zinatokana na wanataaluma hii kutopewa nafasi ya kutekeleza majukumu yao vema,” amesema.

Amesisitiza dhamira yao ni kuwa na nguvu ya pamoja katika kushauri masuala ya kimawasiliano ndani ya jumuiya hiyo.

Mjumbe wa Bodi ya PRST, Loth Makuza amesema katika mkutano huo watazindua chama cha wanataaluma hiyo cha ukanda wa Afrika Mashariki.

“Ili tuwe na uwezo wa kusukuma ajenda na zifanyiwe kazi katika ukanda wote,” amesema Makuza.

Amesema wanafahamu mafanikio ya mipango hiyo hayawezi kufikiwa haraka, wanachokifanya ni kuendeleza juhudi hadi wafikie kunakotarajiwa.

Hata hivyo, ameweka wazi kuwa kuna mafanikio yaliyoshuhudiwa katika mataifa mbalimbali baada ya mikutano miwili iliyofanyika Kenya na Uganda.

Amesema kwa sasa angalau mataifa wanachama yameanza kufanyia kazi sera zinazowatambua wanataaluma hiyo ndani ya taasisi za umma na Serikali Kuu kwa jumla.

Related Posts