ALIYEKUWA mshambuliaji wa Polisi Tanzania, Gerald Mathias Mdamu ameruhusiwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu wa kulia Ijumaa iliyopita huku akibainisha kwamba sasa ana amani ya moyo.
Julai 9,2021, Mdamu alipata ajali ya kuvunjika miguu yote miwili wakati wanatoka mazoezini na basi la timu ya Polisi Tanzania katika Uwanja wa TPC kurejea kambini.
Baada ya upasuaji huo, Mdamu amewashukuru Watanzania kwa namna walivyojitolea kumchangia pesa za matibabu hadi kukamilisha jambo hilo.
“Kitendo cha kutokwa na usaha bila kukauka tangu mwaka 2021, kilikuwa kinaiharibu akili yangu, baada ya upasuaji wa kuondoa tatizo, sasa moyo wangu una amani.
“Nimeambiwa nirudi baada ya wiki mbili lakiniĀ pia nimepewa dawa za kutumia nikiwa nyumbani,” alisema Mdamu.
Katika hatua nyingine, Mdamu amelishukuru Gazeti la Mwanaspoti kwa kuibua changamoto yake ambapo wadau mbalimbali walijitokeza kumsajidia likiwamo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji, Mwamnyeto Foundation.
“Asanteni kwa kila mmoja wenu aliyehusika kunifanya amani irejee na kuona maisha mengine yataendelea, nikipona nitakuja kuwaambia,” alisema.
Kwa upande wa mke wake, Juliana alisema: “Asante sana Watanzania kwa kila jambo, Mungu awaongezee mlipotoa. Asante Mwanaspoti kwa kujitoa kwa ajili ya Jamii.”
Mwanaspoti limekuwa bega kwa bega na mchezaji huyo wa zamani wa Mwadui FC tangu lilipomtembelea nyumbani kumjulia hali na kuibua hali yake na wadau kujitokeza.
Katika kumchangia, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Rais Wallace Karia liliitoa Sh1.5 milioni na Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji alitoa kiasi kama hicho, wakati Mwamnyeto Foundation iliopo chini ya kiungo wa Singida Black Stars, Zawadi Mauya na nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto nayo ilijitolea Sh.1milioni. Pia wadau wengine wamekuwa wakimtumia michango mbalimbali ya fedha kupitia akaunti yake ya lipa kwa namba.