Mtanzania matumaini kibao Misri | Mwanaspoti

NYOTA wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga TUT FC inayoshiriki Ligi ya Wanawake nchini Misri, Hasnath Ubamba amesema anaamini utakuwa msimu bora kwake licha ya kwamba ni mara ya kwanza kucheza nje ya mipaka ya Tanzania.

Mshambuliaji huyo alisajiliwa msimu huu kwa mkopo wa mwaka mmoja na mabingwa hao wa Misri akitokea Fountain Gate Princess inayoshiriki Ligi ya Wanawake (WPL).

Akizungumza na Mwanaspoti, Ubamba alisema anatamani kufanya vizuri akiwa na timu hiyo na kufanikisha ndoto yake ya kucheza ligi kubwa Ulaya.

“TUT sio timu ndogo ina wachezaji wazuri hivyo itanisaidia hata mimi kupata uzoefu na nashukuru tangu nimefika nimecheza mechi tatu za mashindano ya CAF,” alisema Ubamba.

Kwenye michuano ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF) kwa wanawake ukanda wa UNAF, Mtanzania huyo alicheza mechi zote na kufunga bao moja na kutoa asisti mbili kwenye mechi tatu.

Michuano hiyo ilichezwa kwenye Uwanja wa Rouiba nchini Algeria ikishirikisha timu nne kutoka ukanda wa UNAF na Mtanzania huyo akianza dhidi ya ASF Sousse (Tunisia) timu yake ikishinda mabao 7-0 akifunga bao moja na kutoa asisti, Agosti 25.

Agosti 27 alicheza tena dakika 90 dhidi ya Akbou FC (Algeria), TUT ikishinda mabao 4-2 akitoa asisti moja na kutinga fainali ambako ilifungwa bao 1-0 na AS Far ya Morocco ambayo ndio imefuzu CAF.

Related Posts