Mtumbwi wazama Ziwa Victoria, mmoja apoteza maisha, sita hawajulikani walipo

Bunda. Watu sita wanahofiwa kufa maji, huku mwili mmoja ukiopolewa baada ya mtumbwi waliokuwa wakisafiria kuzama ndani ya Ziwa Victoria.

Watu hao walikuwa wakitoka kwenye harusi Kijiji cha Mwiruruma, kuelekea katika kitongoji cha Bulomba Kijiji cha Igundu wilayani Bunda Mkoa wa Mara.

Mkazi wa Kijiji cha Igundu, Mapambano Kasala ameiambia Mwananchi Dijital kwa simu leo Jumatatu Septemba 16, 2023 kuwa tukio hilo lilitokea jana Septemba 15, 2024, saa moja jioni.

Amesema mtumbwi huo ulikuwa umebeba watu zaidi ya 20 na baada ya kuanza safari ulizama baada ya kuzidiwa uzito.

“Mwili mmoja uliopolewa jana hiyohiyo ukiwa umenasa kwenye nyavu za nanga, wengine wameokolewa wakiwa hai, ila wengine zaidi ya sita bado hawajapatikana hadi sasa,” amesema Kasala.

Amesema watu hao baada ya kumaliza sherehe kwa upande wa bibi harusi, walikuwa wakirudi nyumbani kwa ajili ya maandalizi ya harusi kwa upande wa bwana harusi, sherehe ambayo ilipangwa kufanyika leo.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Dk Vicent Naano amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema yupo njiani kueleka eneo la tukio.

Dk Naano amesema mtumbwi uliohusika kwenye ajali unadaiwa kuwa ulibeba watu 16 na baada ya tukio, watu tisa wameokolewa wakiwa hai, huku mwili mmoja ukiopolewa na watu sita mpaka sasa hawajapatikana.

“Kinachoendelea kwa sasa ni kuwatafuta hao watu sita, mwili mmoja uliopolewa jana baada ya ajali kutokea na watu tisa waliokolewa wakiwa hai. Kwa sasa nipo njiani naelekea eneo la tukio,” amesema Dk Naano.

Julai 30, 2023 watoto 14 wakiwamo wanafunzi 13 wa Shule ya Msingi Bulomba katika Kijiji cha Igundu, walifariki dunia baada ya mitumbwi miwili waliyokuwa wamepanda wakitoka kwenye ibada Kanisa Takatifu la Mungu wa Kiroho (KTMK), kuzama ndani ya Ziwa Victoria, eneo la Kijiji cha Mchigondo.

Katika tukio hilo la mwaka jana, watu 14 waliokolewa wakiwa hai, huku chanzo cha tukio kikielezwa kuwa ni mitumbwi hiyo kuzidisha uzito.

Related Posts