Rekodi zavunjwa mashindano ya Taifa, TSA yajivunia mafanikio

Na Winfrida Mtoi, Mtanzanja Digital

Zaidi ya rekodi 21 zimevunjwa katika mashindano ya Wazi ya Taifa ya kuogelea yaliyomalizika Septemba 15, 2024 kwenye Bwawa la kuogelea la Shule ya Kimataifa Tanganyika (IST), Masaki, jijini Dar es Salaam.

Katika mashindano hayo ya siku mbili, jumla klabu 14 kutoka nchi za Tanzania, Kenya na Uganda zimeshiriki, huku waogeleaji waliojitokeza katika michuano hiyo ni zaidi ya 200.

Akizungumzia mashindano hayo, Mwenyekiti wa Chama cha mchezo wa Kuogelea Tanzania( TSA) David Mwasyoge , amesema tayari maandalizi ya kuelekea Olimpiki 2028 yameanza, kwani ndio wanatengeneza wachezaji watakaofuzu.

“Wachezaji wameongeza muda wao, lengo letu katika mashindano kama haya ni kutengeneza timu ambayo itafuzu olimpiki, vijana hawa wa miaka 13-14 ndio wawakilishi wetu olimpiki kwani hadi ikifika 2028 ndio watakuwa katika viwango vya juu,” amesema Mwenyekiti huyo.

Aidha amesema kingine wanachofanyia maandalizi ni mashindano ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati yanayotarajiwa kufanyika Novemba nchini Burundi na wanahitaji kurejesha ubingwa waliopoteza mwaka jana.

Related Posts