Wakati wa ziara yake, Kansela Scholz amekutana na Rais wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev huko Astana. Viongozi hao wawili walionyesha dhamira yao ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili na kusaini makubaliano ya kuongeza kiwango cha mafuta ya Kazakhstan yanayouzwa nchini Ujerumani.
Taifa hilo la Asia ya Kati kwa sasa linachangia takriban 11.7% ya mafuta yanayouzwa nchini Ujerumani, ikiziba pengo lililoachwa na Urusi tangu uvamizi wake dhidi ya Ukraine.
Mbali na biashara, mzozo huo wa vita kati ya Urusi na Ukraine umekuwa agenda muhimu ya mazungumzo baina ya viongozi hao. Rais Tokayev, ametetea mazungumzo ya amani kuvimaliza vita hivyo, akisema kuwa Urusi haiwezi kushindwa kijeshi na akionya kuhusu matokeo mabaya ikiwa vita hivyo vitazidi kupanuka.
”Kuzidi kuchochea vita hivi kutasababisha madhara yasiyoweza kurekebishwa na jumuiya ya kimataifa, na hususan kwa nchi zinazohusika moja kwa moja,” amesema kiongozi huyo wa Kazakhstan mjini Astana.
Scholz asisitiza kuheshimu vikwazo dhidi ya Urusi
Kwa upande wake Kansela Scholz amesema atapigania kuimarika kwa biashara baina ya Ujerumani na Kazakhstan, akionya lakini kuwa sio kwa gharama yoyote, hususan iwapo biashara hiyo inaweza kutoa mwanya wa kuvunjwa kwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi.
Soma pia:Kansela Scholz atetea mipango ya pensheni katika bajeti ya 2025
”Ninashukuru kwa mazungumzo yenye kuaminiana baina yetu, ambako kutasaidia kuepusha biashara kati yetu kutumiwa vibaya, na kukwepa vikwazo [dhidi ya Urusi]”
Ziara hiyo ya Kansela Olaf Scholz imeshuhudia kutiwa saini makubaliano ya kuongeza ushirikiano kati ya Benki Kuu ya Kazakhstan na Benki Kuu ya Ujerumani, Bundesbank, kuanzisha taasisi ya sayansi na teknolojia katika Chuo Kikuu cha Kijerumani-Kazakhstan huko Almaty, na kuanzisha shule ya lugha ya Kijerumani nchini Kazakhstan.
Kazakhstan ambayo ni nchi ya kimkakati kwa ukuaji wa uchumi, inabaki kuwa mshirika muhimu zaidi wa kiuchumi wa Ujerumani katika Asia ya Kati. Hata hivyo inakabiliwa na ukosoaji kuhusu masuala ya haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na vikwazo vya uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza.
Wakati mvutano wa kimaslahi ukipamba moto kutokana na mzozo baina ya Urusi na Ukraine, ziara ya Kansela Olaf Scholz ni muendelezo wa juhudi za Ujerumani za kubadilisha vyanzo vyake vya nishati na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi katika ukanda wa Asia ya Kati.
Vyanzo: dpae, rtre