Dar es Salaam. Jumla ya Sh45 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu mwaka 2024/2025 Tanzania nzima.
Wanyama hao wakali na waharibifu kuwa ni tembo, simba, chui, faru, nyati, mamba na kiboko.
Hayo yamesemwa na Gideon Mseja kutoka Wizara ya Maliasili, Idara ya Maliasili Dawati la Muingiliano wa Wanyamapori na Binadamu, wakati akiwasilisha wasilisho la hatua zilizochukuliwa na wizara hiyo katika kutatua migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori (WHC) kupitia Mradi wa kutatua migongano ukanda wa Kusini.
Mseja ametoa wasilisho hilo, Septemba 12, 2024 katika mdahalo ulioandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), kwa ufadhili wa Mradi wa Kupunguza Migongano Baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania, unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).
Mseja amesema kutokuzingatia mipango ya matumizi ya ardhi katika vijiji vinavyopakana na maeneo yanayotumiwa na wanyamapori pamoja na mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaathiri makazi ya wanyamapori ni miongoni mwa visababishi vinavyochangia migongano baina ya binadamu na wanyamapori.
“Pia, uingizaji mifugo ndani ya hifadhi husababisha wanyamapori kutoka ndani ya hifadhi na kuingia kwenye maeneo ya wananchi, lakini pia ongezeko la mimea kuvamia katika maeneo yaliyohifadhiwa ni miongoni mwa visababishi vinavyochangia migongano baina ya binadamu na wanyamapori,” amesema Mseja.
Amesema kutokana na hali hiyo, Serikali imekuja na mikakati maalumu yenye malengo saba ya kutatua migongano baina ya binadamu na wanyamapori ambayo ni pamoja na kufanya utatuzi wa migongano katika ngazi ya jamii, udhibiti wa matukio ya migongano, usimamizi wa maeneo yenye muingiliano baina ya binadamu na wanyamapori pamoja na kutoa elimu ya mbinu za uhimilivu.
Mikakati mingine ni kufanya ufuatiliaji wa matukio na utafiti wa migongano na mbinu za utatuzi na faida za uhifadhi kwa jamii ili kuhimili migongano.
Amebainisha kuwa utalii unachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa na asilimia 25 ya fedha za kigeni na kwamba utalii unazalisha ajira takribani 1.6 milioni za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa mwaka.
“Pamoja na mafanikio hayo, migongano baina ya binadamu na wanyamapori imeongezeka, kwani wilaya 44 kati ya 91 zilizopo nchini zimebainika kuathiriwa zaidi na changamoto hiyo.” amesema Mseja na kuongeza
“Kwa kutambua hilo, Serikali imeamua kutenga fedha kiasi cha Sh45 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mipango na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu mwaka 2024/2025 nchi nzima.”
Hata hivo amesema kwa kuwa suala hili ni mtambuka, Wizara inatambua mchango wa wadau na itaendelea kushirikiana na Wizara za Kisekta na wadau wa uhifadhi katika utatuzi wa changamoto na kufanya tathmini ya maandalizi ya mkakati mpya.
Awali, Mshauri wa Mradi huo kutoka GIZ, Anna Kimambo alisema kuwa mradi huo umelenga ukanda wa Ruvuma na Lindi, hasa wilaya za Tunduru, Namtumbo na Liwale na kwamba mradi huo unatekelezwa hapa nchini kwa muda wa miaka mitano ambapo ulianza Februari 2022 na unatarajia kukamilika mwaka 2025.
Kimambo alisema anaamini mradi huo utaleta matokeo chanya kutoka maeneo ya mradi ambayo ni Liwale, mkoani Lindi na Namtumbo pamoja na Tunduru kutoka mkoani Ruvuma ambapo vijiji 30 vinatarajiwa kufikiwa katika Mradi huo.
Alisema Tanzania imetenga asilimia 32.5 ya ardhi yake kwa ajili ya uhifadhi wa rasilimali za maliasili na kwamba ina hifadhi za taifa 21, eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, mapori ya akiba 29, mapori tengefu 23, maeneo ya Ardhioevu manne na Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori za Jamii 38.
Clement Kamendu ni Mwenyekiti wa Baraza la Wasafirishaji Shehena (TSC), amesema kama tembo wakitunzwa vizuri wana uwezo wa kuchangia dola 25 milioni kwa mwaka, hivyo juhudi za pamoja zinahitajika katika kutunza wanyamapori ili wawe na manufaa kwa taifa.
Kamendu amesema migongano baina ya binadamu na wayamapori imesababisha athari mbalimbali ikiwe binadamu kujeruhiwa, uharibifu wa mazao, mifugo kujeruhiwa au kuuawa, uharibifu wa miundombinu pamoja na wanyamapori kujeruhiwa au kuuawa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, alisema wamefanya mdahalo huo kwa kifanya mdahalo huo lengo la kutoa uelewa wa waandishi wa habari juu ya masuala ya uhifadhi na mazingira ili kuwawezesha kuandika kwa tija na kusaidia kupunguza migogoro hiyo kupitia vyombo vya habari.
“JET imekuwa ikifanya midahalo mbalimbali kwa ajili ya waandishi wahabari ili waweze kuandika vizuri habari za migongano baina ya binadamu na Wanyamapori kwa ufasaha na weledi” alisema Chikomo.