RAUNDI ya nne ya Lina PG Tour ambayo itachezwa mwishoni mwa mwezi katika viwanja vya Moshi Gymkhana, Kilimanjaro ni mahsusi kwa ajili ya kuenzi chimbuko la mlezi wa gofu ya wanawake nchini, Lina Nkya ambaye alianzia gofu katika viwanja hivyo.
Haya yalielezwa jana na Mkurugenzi wa mashindano haya, Yasmin Challi ambaye alisema raundi ya nne itachezwa katika viwanja ambavyo Lina Nkya alianzia kucheza gofu na hivyo kuifanya raundi hii kuwa na uzito mkubwa kwa familia yake na famila ya wacheza gofu kwa ujumla.
“ Raundi ya nne inachezwa katika viwanja vilivyo karibu na nyumbani kwa Lina Nkya. Alianza hapo kabla kuanza kuchochea maendeleo ya gofu nchini na Afrika nzima, hiyo ni kama tutakuwa naye siku hiyo,” alsema Challi, ambaye pia ni katibu wa chama cha gofu ya wanawake nchini, TLGU.
Lina PG Tour ni mashindano ya raundi tano yanayojumuisha viwanja vitano tofauti nchi nzima.
Raundi ya kwanza ilifanyika katika viwanja vya TPC mkoani Kilimanjaro kabla ya viwanja vya Morogoro kuwa mwenyeji wa raundi ya pili mwezi Mei mwaka huu.
Raundi ya tatu ilipigwa Arusha Gymkhana mwezi Julai mwaka huu kabla ya kuipeleka raundi ya nne mjini Moshi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa michuano hiyo raundi ya nne itapigwa mkoani Kilimanjaro kutoka Septemba 26 hadi 29 mwaka huu.
Kuelekea raundi ya nne ya mbio za ubingwa wa Lina PG Tour, Ali Isanzu wa TPC ndiye anaongoza licha ya kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wachezaji wa Arusha na Dar es Salaam ambao walimpa wakati mgumu katika michuano ya raundi ya tatu jijini Arusha.
Kufuatia matokeo mengine ya raundi za kwanza na pili, tishio kubwa kwa Isanzu ni Isiaka Daudi ambaye ameshika nafasi ya pili nyuma ya Isanzu katika raundi mbil za awali kabla ya kumuacha Isanzu kwa nafasi moja katika raundi ya tatu ya jijini Arusha.
Nuru Mollel haonekani kuwa presha kubwa kwa upande wa gofu ya kulipwa baada ya kuuwaacha mbali wapinzani wake wa karibu, Fadhil Nkya na Hassan Kadio wa Dar es Salaam.
Mpaka kufikia mwisho wa raundi ya tatu, Mollel amechukua ushindi katika raundi mbili na kushika nafasi ya pili katika raundi moja.
Mshindi wa jumla wa raundi tano za Lina PG Tour atakata tiketi ya kucheza katika mashindano ya gofu ya dunia katika Falme za Kiarabu na hivyo kuyapa mashindano haya jina la ‘The Road to Dubai’.