Ushetu watoa maua yao kwa Bashe kwa kuishi kwa vitendo maono ya Rais

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Wananchi wa Halmashauri ya Ushetu na Wilaya ya Kahama wamemlaki kwa maelfu na shangwe za kishindo Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe (Mb) na kujivunia kuwa wao ni wakulima na wako tayari kuendelea kutafsiri maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Akimkaribisha Waziri Bashe kuhutubia Mkutano wa hadhara Septemba 15, 2024 katika kijiji cha Mbika, Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha amesema kuwa nyumba za mfano 4 za Maafisa Ugani zimefika mkoani kwake Pamoja na sare za nguo kwa Maafisa Ugani, pikipiki, vishikwambi na vifaa vya kupimia afya ya udongo.

Mkuu wa Mkoa pia amewasisitizia wananchi kuhakikisha wanachagua viongozi bora wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa; huku Viongozi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wamepongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuleta miradi mikubwa ya sekta mbalimbali yenye thamani ya mabilioni ya fedha ili kuinua maisha ya wana-Shinyanga. 

Aidha, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Emmanuel Cherehani “asali ya Ushetu” amemuomba Waziri Bashe kuangalia zao la tumbaku, hususan tozo za miti ambazo zinamgharimu mkulima hivyo asaidie tozo hizo ziwe kwa wanunuzi.  Ameomba jimbo la Ushetu wapatiwe mradi mkubwa wa maji ili wananchi nao wanufaike na Kilimo cha umwagiliaji; pamoja na suala la vyama vya ushirika vinahitajika ili wananchi wajisajili jimbo la Ushetu.

Naye Waziri Bashe amesema kuwa kwenye tasnia ya tumbaku tumepiga hatua.  “Serikali imetenga shilingi bilioni 2 kuanza kujenga mabani kwa wakulima na makampuni watachangia kila kiko wanayonunua shilingi 40 ili kujengea wakulima mabani ya kudumu,” amesema Waziri Bashe.  Amesisitiza kuwa hiyo shilingi 40 hatozwi mkulima, na yeyote atakayejisajili kama mnunuzi wa tumbaku atachangia gharama hiyo.

“Mhe. Rais Dk. Samia msimu uliopita ametoa shilingi bilioni 13 ambapo zitatumika kwa mbolea ya ruzuku ya NPK ambapo Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) watatoa kufuatia usajili wa wakulima na mahitaji halisi,” amefafanua Waziri Bashe. Ameeleza zaidi kuwa na utararibu huo utaendelea kwa miaka mitatu.

Related Posts