Afisa mkuu wa polisi katika Jamhuri ya Czech Martin Vondrasek, amesema mtu mmoja amezama kwenye mto karibu na mji wa Bruntal eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo huku mamlaka ikirekodi kupotea kwa watu saba .
Soma pia: Mafuriko yagharimu maisha zaidi mvua zikipiga Ulaya ya Kati
Nchini Poland, mafuriko yagharimu maisha zaidi huku mvua zikipiga Ulaya ya Kati. Mtu mmoja amezama na nchini Austria, mamlaka ya nchi hiyo iliripoti kufa kwa mvuvi mmoja wakati kimbunga hicho kikisababisha mvua kubwa katika maeneo la Ulaya ya kati na mashariki.
Upepo mkali na mvua kubwa katika baadi ya nchi za Ulaya
Tangu Alhamisi, maeneo ya Austria, Jamhuri ya Czech, Hungary, Romania na Slovakia yamekumbwa na upepo mkali na mvua kubwa isivyo kawaida.
Mvua hizo zimesababisha mafuriko mitaani na kuzamisha baadi ya vitongoji, huku usafiri wa umma ukikatizwa pamoja na huduma za umeme katika maeneo mengine.
Watu wawili wafariki Romania, wanne hawajulikani walipo
Nchini Romania, miili miwili iligunduliwa jana Jumapili baada ya watu wanne kuripotiwa mapema kufa na mmoja kuripotiwa kutoweka.
Watu wanne pia hawajulikani walipo nchini Czech.
Siku ya Jumapili, waziri mkuu wa Poland Donald Tusk, alisema kuwa wamepata thibitisho la kwanza la kifo kutokana na kuzama katika eneo la Klodzko lililoko kwenye mpaka kati ya Poland na Czech kusini magharibi mwa nchi hiyo ambalo limeathirika zaidi kutokana na mafuriko.
Ukraine yajitolea kuisaidia Poland
Tusk ameongeza kuwa Ukraine, inayokabiliana na uvamizi wa Urusi nchini humo kwa mwaka wa tatu sasa, imejitolea kutuma wataalamu 100 wa kukabiliana na mafurikonchini Poland, kama ishara ya mshikamano nayo kwa kuiunga mkono kikamilifu wakati huu wa vita.
Takriban watu 1,600 wamehamishwa kutoka mjini Klodzko huku viongozi wa Poland wakitoa wito kwa jeshi kuwasaidia maafisa wa zima moto.
Umoja wa Ulaya uko tayari kutoa msaada
Katika ujumbe aliochapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X, rais wa halmashauri kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen, alielezea mshikamano wa dhati na wote walioathiriwa na mafuriko makubwa nchini Austria, Jamhuri ya Czech, Hungary, Poland, Romania na Slovakia na kuongeza kuwa Umoja wa Ulaya uko tayari kutoa msaada.